|
Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kupanda kwa bei ya
mafuta kuanzia leo kutokana na mabadiliko ya bei katika Soko la Dunia.
Bei hizo za
jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote ya petroli, dizeli na taa zimepanda,
ikilinganishwa na bei zilizotolewa mwezi uliopita.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei za reja reja, zimeongezeka kwa Sh
17 kwa lita moja ya petroli sawa na asilimia 0.88, dizeli Sh 90 kwa lita sawa
na asilimia 5.24 na mafuta ya taa Sh 72 kwa lita, sawa na asilimia 4.28
ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.
Kwa upande
wa bei za jumla, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema pia zimeongezeka kwa petroli,
dizeli na mafuta ya taa, ambapo bei mpya za jumla zitakuwa Sh 16.56 kwa lita
moja ya petroli sawa na asilimia 0.93, dizeli Sh 90.20 kwa lita sawa na
asilimia 5.59 na mafuta ya taa Sh 72.29 kwa lita sawa na asilimia 4.58 .
Ngamlagosi
alisema kuongezeka kwa bei hizo katika soko la ndani, kwa kiasi kikubwa
kumetokana na kuongezeka kwa bei katika Soko la Dunia, na gharama za
usafirishaji wa bidhaa hiyo kuja nchini.
Pamoja na
mabadiliko hayo yanayoihusu nchi nzima, alisema bei hizo mpya, hazitauhusu mkoa
wa Tanga ambapo vituo vya mafuta mkoani humo vimeagizwa kutopandisha bei mwezi
huu.
Alisema
hatua hiyo inatokana na mkoa huo, kutokupokea mafuta mapya mwezi Julai, na
kufanya bei za Agosti kuendelea kutumika kama ilivyokuwa kwa mwezi Julai.
“Mamlaka
(Ewura) inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika,
zinapatikana vilevile kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na
kisha kufuata maelekezo, ambapo huduma hii ni bure na inapatikana kupitia
mitandao yote ya simu za mkono nchini,” alisema.
Alisema kwa
mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli
zitaendelea kupangwa na soko.
Alisema Ewura
itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za
mafuta na kuongeza; “ Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya
maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.”
Alisema
kampuni za mafuta, zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya
ushindani, mradi tu bei hizo ziwe chini ya bei kikomo, kama ilivyokokotolewa na
fomula iliyopitishwa na Ewura.
Alisema
vituo vyote vya mafuta, vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika
mabango, yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya
biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo
inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo
vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kuhamasisha. Ni kosa kuuza mafuta
bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” alisema.
Mkurugenzi
Mkuu huyo alisema adhabu kali, itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza
matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika. Alishauri wanunuzi kuhakikisha
kuwa wanapata stakabadhi ya malipo, inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya
mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Alisema
stakabadhi hiyo ya malipo, itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta,
endapo kutajitokeza malalamiko au kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei
kikomo ; au atauziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
|
No comments:
Post a Comment