Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akilakiwa kwa
furaha kijijini Bwanga wakati akielekea nyumbani kwake Chato mkoani Geita leo
Agosti 1, 2016.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi
wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa nchini kufuatilia matumizi ya
fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo
la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Agosti, 2016 katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa Katoro
na Buseresere Mkoani Geita.
Katika agizo
hilo Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa
kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata
mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi
ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu
mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo
baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili
kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi kama
wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi
hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja wagawane.
"Napenda
nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta
matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja na
agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa
kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo
katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa
kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi
atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na
wadhifa alionao.
"Na
nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi,
Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, kila mmoja awe na
idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela
ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi"
Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais
Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na
Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya
pia amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea
wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza
ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, Dkt.
Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji,
Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya
Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya
fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika Halmashauri husika.
"Hivi
kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na mashine za
kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji Dkt. Magufuli na kuongeza
kuwa;
"Tena
mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa wananchi
wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata kuwaonea huruma"
Rais
Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza ziara yake
ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na yupo
nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
01 Agosti,
2016
|
No comments:
Post a Comment