|
Katika magonjwa
yanayosumbua wanawake wengi na watoto nchini hivi sasa ni ugonjwa unaoathiri
njia ya mkojo U.T.I (Urinary Tract Infection).
Wakati wanawake wengi
wanaougua ugonjwa huu wakihangaika kila siku kupata tiba yenye usahihi,
wataalamu wa afya wanasema unapojiimarisha mwilini kwa muda mrefu huathiri
figo.
Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk
Cyriel Massawe anasema, tatizo hili
hujitokeza pale mlango wa njia ya haja ndogo unaposhambuliwa na bakteria ambao
husambaa na wasipotibiwa mapema, huenea hadi kwenye figo na athari zake ni
mbaya.
“Bakteria hawa
hupatikana ndani ya sehemu za siri za mwanamke, bakteria hao wakiwa ndani ya
uke hawana madhara kabisa, lakini pindi uke unapopata mchubuko bakteria hawa
huanza kuathiri kibofu cha mkojo na mtu kuanza kupata madhara,” anasema na
kuongeza:
Wanawake wanapata UTI
kwa urahisi sana kuliko wanaume kwa sababu
mirija ya mkojoya mwanamke ni mifupi ambayo huruhusu bacteria kuingia
kwa urahisi tofauti na ya mwanaume.
Vyanzo vya UTI
Dk Masawe anasema kuna
vyanzo vingi vinavyosababisha ugonjwa huu, ikiwamo matumizi ya maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga huweza
kuweka bakteria kwa urahisi na mwanamke kupata UTI.
Uchafu wa vyoo umetajwa
kuwa sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza
kusababisha mwanamke kupata UTI kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria wengi
ambao wanaweza kusababisha UTI.
Anasema kufanya ngono
mara kwa mara ni tatizo kubwa ambalo ndilo linafanya wanawake wengi kupata UTI
siku hizi, kwani wakati wa ngono msuguano huwa mkubwa ambao hufanya bakteria
kutoka kupitia majimaji ya ukeni na kuingia katika njia ya mkojo.
“Mwanamke ambaye
anafanya ngono mara kwa mara yuko kwenye hatari ya kupata UTI kuliko yule ambaye
hafanyi ngono mara kwa mara. Pia matumizi ya nguo za ndani za mitumba bila
kufua husababisha kwa urahisi mwanamke kupata UTI,” anasema.
Hata hivyo anasema
tatizo kubwa limetajwa kuwa kemikali, “kemikali zinawaathiri wanawake wengi
siku hizi, kutumia sana kemikali hasa
kwenye vipodozi ambavyo kemikali hizi kwa kuwa ni sumu huenda hadi kwenye
kibofu na kuchubua kibofu na hapo ndipo tatizo hilo huanza.”
Wataalamu wamesisitiza
kwamba wengi wamekuwa na tabia ya kubana mkojo kwa muda mrefu, lakini matokeo
ya tabia hii ni kupata UTI.
Dalili za UTI
Dalili za ugonjwa huu
ni pamoja na mtu kusikia haja ya kukojoa kila wakati na kusisimka wakati wa
kujisaidia, kusikia maumivu, kutoa mkojo mchafu na hata kutoa haja ndogo
iliyochanganyika na damu.
Mwili kuchoka mara kwa
mara, homa za mara kwa mara, kichwa kuuma mara kwa mara, kubanwa na mkojo
halafu ukienda kukojoa unakuta mkojo kidogo, maumivu wakati wa kukojoa na kiuno
kuuma.
Unaweza kuikinga UTI
kwa njia mbadala
Mkurugenzi wa Kituo cha
huduma ya ushauri nasaha, lishe na afya COUNSENUTH, Mary Materu anasema, kwa
kawaida kila ugonjwa una tiba mbadala, siyo lazima kwenda hospitali.
“Unaweza kuudhibiti au
kuponya ugonjwa huu kwa kunywa maji mengi pamoja na juisi itokanayo na matunda
halisi, iwapo utawahi kabla tatizo halijawa sugu. Kwa maana nyingine, unaweza
kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila
siku. Ukinywa maji ya kutosha yatakufanya uende haja ndogo kila mara na kwa
njia hiyo wale bakteria watakuwa wakitoka na hatimaye kuisha kabisa,” anasema
Materu.
Aidha, anasema njia
nyingine ya kuudhibiti ugonjwa huu ni kunywa maji mengi au kwenda haja ndogo
mara baada ya kufanya tendo la ndoa, kitendo hiki husaidia kuwaondoa mapema
bakteria wote ulioambukizwa wakati wa kujamiiana na mwenzio.
“Katika hali ya
kawaida, ugonjwa wa UTI hutoweka ndani ya siku tatu mara baada ya kuanza
kutumia tiba asili ya kunywa maji mengi na juisi ya matunda halisi, iwapo
ugonjwa utaendelea kuwepo baada ya siku hizo, hiyo itakuwa na maana ugonjwa
wako umeshakomaa na hivyo hauwezi kutibika kwa tiba hii ya nyumbani,” anasema
na kuongeza:
“Katika hali kama hii,
utakuwa huna njia nyingine isipokuwa kwenda hospitalini na kuonana na daktari
ambaye atakufanyia uchunguzi na kukupatia dozi sahihi ambayo utatakiwa
kuizingatia bila kukosa. Uamuzi huu ni muhimu hasa kama unasikia maumivu makali
ambayo yanaweza kuwa yanasababishwa na kuathirika kwa figo,” anasema Materu.
Dk Massawe anasema kwa
kawaida tiba ya kidaktari kwa ugonjwa huu huhusisha matumizi ya dawa kali za
‘antibiotics’, ambazo watu wengi wanazikimbia kutokana na athari zake za
baadaye (side effects).
Lakini ni muhimu
kufuata ushauri wa daktari na kumaliza dozi ili kuepuka uwezekano wa kurejea
kwa ugonjwa, tena kwa kasi kubwa.
Unaweza kujikinga na
UTI
Mkurugenzi kutoka Kituo
cha Afya Tiba cha Neema Herbalist & Nutritional Foods Clinic Dk Africanus
Boniface anasema, ili kujiepusha na ugonjwa huu, suala la usafi na kuwa na
tabia ya kunywa maji ya kutosha ni jambo muhimu sana.
“Hakikisha unajisafisha
vizuri mara baada ya kwenda haja na kubadilisha mara kwa mara nguo yako ya
ndani, hasa kwa akina mama,” anasema na kuongeza: “Vile vile usikae na haja
ndogo kwa muda mrefu, nenda kajisaidie mara nyingi kadri unavyosikia kufanya
hivyo.
Kitu cha mwisho cha kuzingatia kwa mgonjwa wa UTI ni kupunguza unywaji
wa pombe na vinywaji vingine vyenye sukari, kwa sababu sukari ni chakula cha
bakteria hivyo kwa kuendelea kunywa kinywaji chenye sukari kutaifanya hali
kuendelea kuwa mbaya, “ anasema Dk Boniface.
Anasema ugonjwa huu ni
rahisi kuuepuka kwa mtu anayependa kunywa maji ya kutosha na kunywa juisi
halisi kila siku.
Vyakula vinavyokukinga
na UTI
Dk Boniface anasema,
katika kuudhibiti ugonjwa huu, pendelea kula vyakula au vinywaji vyenye kiwango
kikubwa cha vitamini C, ambayo utaipata kwenye matunda ya aina mbalimbali
yakiwemo machungwa, mboga za majani n.k.
“Jiepushe na ulaji wa
vyakula vya ‘kupaki’ kama vile ‘chizi’, chokoleti na bidhaa nyingine
zilizotengenezwa kutokana na maziwa.
Pia jiepushe na ulaji wa vyakula vyenye
viungo vingi kama pilau, epuka vinywaji vyenye ‘caffeine’, kilevi na sigara na
mwisho achana na vinywaji kama soda na vinavyofanana na soda,” anasema.
|
No comments:
Post a Comment