|
Benki ya Exim ya China
imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16 za
kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati hapa
nchini kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) unaotarajiwa kuanza katika mwaka
huu wa fedha.
Rais wa Benki ya Exim
ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli jana tarehe 20 Julai, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino
Mkoani Dodoma, kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa
kilometa 2,190 za reli ya kati benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu
katika ujenzi na uendeshaji wa reli.
Pamoja na kukubali
kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli
na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea nchi maendeleo ikiwemo
kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa
ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya
maendeleo.
“Kuhusu huu mradi wa
reli ya kati tuna mtazamo chanya, tunauona ni mradi mzuri na tutatoa
ushirikiano wowote utakaohitajika. Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na serikali
ya Tanzania mchakato wa utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na
kwa kuzingatia muda” Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais
Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang kwa kukubali
kutoa fedha hizo na amemuhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi
huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa
kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika
bajeti.
Rais Magufuli
amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania
na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na
Congo.
“Kwa hiyo kukubali kwao
ambako ilikuwa ni kitu kikubwa, inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda
haraka haraka zinakubalika kimataifa, na wenzetu hawa wachina wana pesa nyingi.
“Na kule kuaminika
kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu ni
mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha, tutaendeleza
reli yetu na bandari zetu” Amesema Rais Magufuli.
Mradi wa ujenzi wa reli
ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge)
kutoka Dar es salaam-Tabora-Isaka-Mwanza, Tabora-Mpanda-Kalemela,
Tabora-Uvinza-Kigoma na Isaka-Keza-Msongati.
Mazungumzo kati ya Rais
Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China
hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof.
Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
20 Julai, 2016
|
No comments:
Post a Comment