|
JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA,
WIZARA YA
MAMBO YA NDANI YA NCHI
Kama
inavyofahamika, tangu mwezi Aprili mwaka jana 2015, nchi yetu imekuwa ikipokea
raia toka Burundi wanaoingia nchini kuomba hifadhi ya ukimbizi kutokana na hali
ya machafuko iliyotokea nchini mwao.
Hadi kufikia
tarehe 10 Februari, 2016, kiasi cha wakimbizi 129,210 toka nchini Burundi
wamepokelewa nchini.
Kati ya
hawa, wakimbizi 79,290 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu
mkoani Kigoma.
Wengine 45,487 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nduta
iliyoko wilayani Kibondo na 4,543 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya
Mtendeli iliyoko wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine imekuwa ikitoa huduma muhimu kama vile
za afya, chakula, maji na ulinzi ili kuhakikisha kuwa wakimbizi hawa wanaishi
kwa usalama.
Hata hivyo,
ukiacha wakimbizi hawa walioanza kuingia nchini mwezi Aprili 2015, Tanzania
bado ina wakimbizi wengine ambao wapo katika Kambi ya Nyarugusu.
Katika kambi
hiyo kuna Wakongo 61,887, Wasomali 150 na wengine 189 toka nchi mbalimbali.
Hii
ina maana kuwa hadi kufikia tarehe 10 Februari, 2016 nchi yetu ilikuwa na jumla
ya wakimbizi 191,436 ambao wamehifadhiwa katika makambi.
RAIA WA NJE
WALIOOMBA HIFADHI NCHINI.
Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi pia imeendelea kushughulikia raia wa nchi za nje ambao
baada ya kuingia hapa nchini wameomba kupatiwa hifadhi ya ukimbizi.
Hadi sasa
maombi 815 ya waomba hifadhi yameshashughulikiwa na Kamati ya Kitaifa ya
Kuwahoji Waomba Hifadhi (NEC).
Kati ya
hawa, 735 wametoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 25 wametoka nchini
Burundi, 14 wametoka nchini Rwanda na 15 wametoka nchini Yemen. Wengine 18
wametoka nchini Syria, 3 Iran, 2 Kenya na 3 wametoka nchini Eritrea.
Hawa wote
maombi yao yameshashughulikiwa na matokeo yatatolewa hivi karibuni baada ya
uchambuzi yakinifu kukamilika.
Maombi
mengine 147 pia yamepokelewa na hivi karibuni Kikao cha NEC kitakaa kujadili
maombi yao.
Kati ya hawa
raia 24 wametoka nchini Yemen, 13 Syria, 3 Somalia, 6 Rwanda na 18 kutoka DRC.
Wengine 2 kutoka Uganda, 1 kutoka Sudan Kusini na 80 kutoka nchini Burundi.
Kundi hili
la waomba hifadhi ni wakimbizi ambao waliingia nchini kabla ya mwezi Aprili,
2015.
Pamoja na
kuwafahamisha wananchi na wadau wengine kuhusu hali ya wakimbizi nchini,
Taarifa hii pia inatolewa ili kuweka sawa habari potofu zilizoandikwa katika
ukurasa wa kwanza wa gazeti la This Day toleo la tarehe 15 Februari, 2016 kuwa
Tanzania ina wakimbizi 1,960,000 na kuwa 63,000 kati ya hawa, wengi wao kutoka
Syria na Yemen, wameomba hifadhi Tanzania. Taarifa za gazeti hili sio za kweli.
IMETOLEWA NA
ISAAC J NANTANGA
MSEMAJI -
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI.
Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari kwa WhatsApp +255789925630 Or +255756830214.
|
No comments:
Post a Comment