Matokeo mabaya waliyoyapata wanafunzi waliohitimu kidato
cha nne mwaka 2012 yamesababisha shule za sekondari za serikali kukosa
wanafunzi 10,000 waliopaswa kuanza masomo Julai 29, mwaka huu.
Kutokana na upungufu huo serikali imeamua kusitisha
usajili wa shule za sekondari za serikali na imewaagiza wakurugenzi wa
halmashauri zote nchini kuboresha shule zilizopo kwa kuhakikisha zinakuwa na
miundombinu bora kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo,
ndiye aliyetangaza upungufu huo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa
ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano katika shule za
sekondari za serikali na vyuo vya ufundi.
“Mwaka jana tulisajili shule mbili za kidato cha tano na
sita, ambazo ni Miono iliyopo Bagamoyo na Tandahimba ya Mtwara… tumekubaliana
mwaka huu hatutaongeza shule nyingine, tuboreshe zilizopo kwanza,” alisema
Mulugo.
Mulugo alisema kutokana na uchache huo wa wanafunzi wenye
sifa za kujiunga na kidato cha tano, hasa wa masomo ya Sayansi ya Jamii,
serikali imeamua kutoongeza idadi ya shule za sekondari kama inavyofanya kila
mara kulingana na idadi ya wanafunzi wenye sifa za kujiunga na shule husika.
Mulugo alisema watahiniwa 34,213 kati ya 431,650
waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 wamechaguliwa kujiunga na
kidato cha tano na watakaokwenda kwenye shule 207 zilizopo hapa nchini.
Mulugo alisema idadi ya waliofaulu inajumuisha wanaokwenda
kwenye vyuo vya ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.
Kwa mujibu wa Mulugo, watahiniwa binafsi 193 walifaulu na
kati yao watahiniwa 76 waliokuwa na sifa za kwenda kidato cha tano
hawakuchaguliwa, kwa sababu mbalimbali, ikiwamo umri zaidi ya miaka 25 huku
mmoja wao akiwa si raia.
“Waliochaguliwa ni 34,213, kati yao wanaokwenda kidato cha
tano ni 33,683 na ufundi ni 530, ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 8.9
ikilinganishwa na wanafunzi 31,423 waliochaguliwa mwaka 2012.
“Kati ya hao wanaokwenda sekondari wasichana ni 10,300 na
wavulana ni 23,383, hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 2,824, sawa na
asilimia 9.15 ikilinganishwa na wanafunzi 30,859 waliochaguliwa mwaka 2012,”
alisema Mulugo.
Kuhusu ufaulu wa masomo ya sayansi, naibu waziri huyo
alisema wavulana wameongezeka, ambapo kati ya 23,383 waliochukua masomo ya
sayansi ni 13,708 sawa na asilimia 58.62 wakati waliobaki walichaguliwa
kwenye msomo ya sayansi ya jamii.
|
Waziri
Shukuru Kawambwa.
|
Mulugo alisema kati ya wasichana 10,300 waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha tano, wasichana 5,038 sawa na asilimia 48.91
walichaguliwa kwenye masomo ya sayansi huku 5,262 sawa na asilimia 51.09 wakipelekwa
kwenye masomo ya sayansi ya jamii.
Kwa upande wa vyuo vya ufundi, Mulugo alisema waliofaulu
ni 530, kati yao wavulana ni 416 na wasichana ni 114, na kusema idadi ya
wasichana imeongezeka kutoka 47 mwaka jana, sawa na asilimia 142.55.
Akifafanua zaidi, alisema kuanzia mwaka huu wamerejesha
utaratibu wa wanafunzi wanaoingia kidato cha tano wataanza masomo wiki ya
tatu ya Julai, badala ya Aprili kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita.
Chanzo:Tanzania Daima.
|
No comments:
Post a Comment