Mchezo wa
soka ni moja ya michezo maarufu sana duniani na ni biashara kubwa sana katika
ulimwengu wa michezo na ukitaka kuamini hili angalia makampuni yaliyowekeza
katika kudhamini soka – ni makampuni makubwa makubwa yenye hadhi ya kitaifa na
kimataifa.
Kwa kuzingatia aina hii ya wadhamini, waendeshaji wa mchezo wa soka,
wameweka kanuni na miongozo ya kufuatwa ili kuhakikisha kuwa wale wanaowekeza
pesa zao wanaona thamani ya uwekezaji wao.
Kwa hiyo soka kama ilivyo katika
michezo mingine inazo kanuni na tutajadili kanuni moja baada ya nyingine kama
zilivobainishwa katika muongozo wa FIFA unaojulikana kwa jina la Law of the
Game.
Sheria Namba
1: UWANJA/DIMBA.
==============
NYASI
Uwanja au Dimba la soka litakuwa la nyasi asilia au bandia kulingana na kanuni za
masindano na nyasi hizo lazima ziwe za rangi ya kijani.
Kwa dimba la nyasi
bandia na kama mchezo unaochezwa utakuwa wa kutambuliwa na FIFA, basi nyasi
hizo bandia lazima zikidhi viwango maalumu vya FIFA.
ALAMA
MBALIMBALI
Uwanja/Dimba la soka litakuwa la umbo la mstatili na michoro mbalimbali
ya mistari.
Mistari hii ni kwa ajili ya maeneo husika ambamo imechorwa.
Kuna
mistari miwili mirefu inayojulikana kama mistari ya pembeni na mingine miwili
mifupi inayoitwa mistari ya goli.
Kiwanja kimegawanywa katika pande sawa mbili
kwa mstari unaoitwa Mstari wa Katikati – mstari huu hugawa mistari ya pembeni
katika pande mbili zilizo sawa.
Pia kipo kitovu cha uwanja ambayo ni sehemu ya
katikati kabisa ya uwanja. Kitovu hiki kimezungukwa na duara la kipenyo cha
mita 9.15.
VIPIMO.
urefu wa
mstari wa pembeni lazima uwe mkubwa kuliko urefu wa mastari wa goli.
Urefu wa mstari wa pembeni ni mita 90 (yadi 100) au 120 (yadi 130).
Urefu wa mstari wa goli ni mita 45 (yadi 50) au 90 (yadi 100)
Mistari yote itakuwa na upana ulio sawa usiozidi sentimeta 12.
Kwa mechi za
kimataifa, upana na urefu wa dimba utakuwa kama ifuatavyo:
Urefu: mita 100 (yadi 110) mpaka 110 (yadi 120)
Upana : mita 64 (yadi 70) mpaka 75 (yadi 80)
ENEO LA GOLI
Eneo la goli litaundwa na mistari miwili iliyochorwa pembe-mraba na na mstari
wa goli umbali mita 5.5 (yadi 6) kutoka kila mlingoti wa goli.
Mistari hii
itaingia ndani ya eleo la uwanja kiasi mita 5.5 (yadi 6) kisha mistari hii
itaunganishwa na mstari uliochorwa sambamba na mstari wa goli.
ENEO LA
PENATI
Eneo la penati litaundwa na mistari miwili iliyochorwa pembe-mraba na mstari wa
goli kiasi mita 16.5 (yadi 18) kuelekea ndani ya uwanja na itaunganishwa na
mstari uliochorwa sambamba na mstari wa goli.
Kwa kila eneo la penati, kutakuwa
na kitovu cha kupigia penati ambayo itakuwa ndiyo alama ya kuweka mpira kwa
ajili ya kupiga tuta – alama hii itachorwa eneo usawa wa kitovu cha goli na
itakuwa umbali wa mita 11 (yadi 12).
Mstari wa upinde wa duara la mita 9.15
(yadi 10) utachorwa kutoka kitovu cha kupigia penati kuelekea upande wa nje ya
eneo la penati.
VIBENDERA
VYA KONA
Kutakuwa na vibendera vya kona vyenye kimo cha takribani mita 1.5 (futi 5)
visivyo na ncha-kali sehemu ya juu na lazima vitawekwa katika kila kona ya
uwanja.
Vibendera hivi vinaweza kuwekwa pia katika mstari wa katikati kiasi
umbali wa mita moja kutoka usawa wa matari wa pembeni.
KIROBO-DUARA
CHA KONA
Kutakuwa na virobo-duara vya nusu-kipenyo cha mita 1 (yadi 1) katika kila
kibendera cha kona, ndani ya eneo la uwanja.
MAGOLI
katikati ya kila mstari wa goli litasimikwa goli. Lango hili litakuwa na
milingoti miwili iliyosimikwa umbali sawa kutoka kila upande wa kibendera cha
kona.
Milingoti hii itaunganishwa na mtambaa-panya sehemu ya juu. Nguzo na
mtambaa panya vinaweza kuwa katika mfumo wa miti, chuma au aina nyingine ya
matirio iliyothibitishwa.
Vinaweza pia kuwa na maumbo ya mraba, mstatili,
mduara au umbile la yai na hayatakuwa hatarishi kwa wachezaji. Umbali kati ya
milingoti ni mita 7.32 (yadi 8) na umbali kutoka mtambaa-panya kuja chini
katika mstari wa goli itakuwa ni mita 2.44 (futi 8).
Milingoti na
mtambaa-panya vitakuwa na upana unaolingana usiozidi sentimeta 12 (inchi 5).
Mstari wa goli nao pia utakuwa na upana sawa na milingoti pamoja na
mtambaa-panya wa goli.
Nyavu zinaweza kufungwa katika magoli na sakafu iliyo
nyumba ya goli alimradi tu zitapashwa kufungwa vyema kiasi cha kutokuleta
bughudha kwa mlinda mlango.
Nguzo za goli (yaani milingoti miwili na mtambaa-panya) lazima zitakuwa na
rangi nyeupe.
USALAMA
Malango lazima yasimikwe imara ardhini. Magoli ya kuhamisha yanaweza kutumika
tu ikiwa kama yatakuwa yanakidhi sharti hili.
MUONGOZO WA
KAMATI MAALUMU YA FIFA
MUONGOZO 1:
Ikiwa kama kutakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya kusimama makocha wa timu
zinazopambana, lazima eneo hilo litakidhi matakwa yaliyothibitishwa na Bodi ya
Vyama vya Soka Kimataifa kama tutakavyoona hapo baadae katika kipengele cha
Eneo la Ufundi.
MUONGOZO 2:
Pale itakapotakiwa kutumika teknolojia maalumu ya goli (goal-line technology),
marekebisho ya muundo wa goli yanaweza kufanyika . marekebisho haya lazima
yatakidhi matakwa ya program maalumu ya FiFa.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 2: MPIRA.
==============
Ukiisoma Sheria Namba 1 inayoelezea kuhusu Dimba la
Soka. Sheria namba 2. Sheria hii inazungumzia kwa muhtasari
kuhusu mpira. Wengine wanaita boli. Wengine gozi la ng’ombe. Mimi hupenda kuita
jabulani nikitiwa hamasa na mpira wa Nike uliotumika katika Fainali za Kombe la
Dunia mwaka 2010, huko Bondeni kwa Madiba. Kama na wewe una jina unalopendelea
utatuambia unaitwa je?
UMBILE NA
VIPIMO
Mpira wa soka utakuwa na sifa zifuatazo:
§ Umbo la tufe
§ Utatengenezwa kwa matirio ya ngozi
au matirio nyingine itakayokuwa inafaa
§ Mduara usiozidi sentimeta 70 (inchi
20) na usiopungua sentimeta 68 (inchi 27)
§ Usiozidi gramu 450 na usiopungua
gramu 410
§ Mgandamizo (presha) kati ya
600-1100g/cm2 kutoka usawa wa bahari.
KUBADILISHA
MPIRA MBOVU
Ikiwa kama mpira utapasuka ama utapata kasoro wakati wa mchezo yafuatayo
yatafanyika:
§ Mchezo utasimama
§ Mchezo utaanza tena kwa mwamuzi
kudondosha mpira eneo ambapo mpira wa awali ulipata kasoro, isipokuwa tu kama
mchezo ulisimamishwa ndani ya eneo la goli ambapo katika hali kama hiyo mwamuzi
ataudondosha mpira mpya eneo la goli sambamba na mstari wa goli katika pahala
karibu na ulipokuwa mpira ulioharibika kabla ya mchezo kusimama.
Ikiwa kama mpira utapasuka ama utapata kasoro wakati wa kupiga mkwaju wa penati
au penati ikiwa imeshapigwa tayari, na haukumgusa mchezaji yeyote ama milingoti
ya goli ama mtambaa-panya wa goli, penati itarudiwa.
Ikiwa kama
mpira utapasuka ama utapata kasoro sekunde chache kabla ya mchezo kuanza, au
wakati wa golikiki, au wakati wa konakiki au wakati wa frikiki au wakati penati
au wakati wa kurusha, zoezi litarudiwa.
Ieleweke
katika kanuni hii kwamba mpira hautabadilishwa isipokuwa kwa idhini ya mwamuzi.
NYONGEZA
Mipira itakayokubalika katika michezo mbali mbali inayotabuliwa na FIFA
itatakiwa kuwa na alama zifuatazo:
§ FIFA Quality Pro
§ FIFA Quality
§ IMS – International Match Standard
Alama hizi zitaashiria kwamba mpira husika unakidhi viwango vya ubora
vilivyobainishwa na FIFA na kwamba mashirika au makampuni yatakayofanya kazi ya
kupima ubora wa mipira lazima yatapata kibali cha FIFA.
Vyama wanachama wa FIFA
wataruhusiwa kutumia mipira yenye alama hizo tatu zilizobainishwa hapo juu.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 3: IDADI YA WACHEZAJI
==============
Mchezo wa soka utachezwa baina ya timu mbili, kila moja ikiwa na wachezaji
wasiozidi 11, miongoni mwao mmoja atakuwa mlindamlango. Mchezo unaweza
usichezwe ikiwa moja kati ya timu zinazopambana itakuwa na wachezaji chini ya
7.
Mabadiliko:-
kwa michezo maalum inayotambuliwa au kutii miongozo ya FIFA, idadi ya wachezaji
kwa ajili ya kufanya mabadiliko itakuwa isiyozidi wa 3.
Hata hivyo kanuni za
mashindano husika zinaweza kubainisha idadi ya wachezaji wa mabadiliko kuanzia
wa 3 lakini wasiozidi 12.
Lakini, kwa mechi za timu ya taifa idadi ya juu
kabisa ya wachezaji wa mabadiliko itakayokubalika itakuwa ni 6.
Kwa michezo
mingine isiyosimamiwa wala kufuata kanuni za FIFA, idadi kubwa ya mabadiliko
inaweza kufanyika kwa kuzingatia yafuatayo:
§ Timu zinazoshiriki zitakubaliana
idadi ya wachezaji wa mabadiliko
§ Mwamuzi apewe taarifa kabla ya
mchezo
Ikiwa kama mwamuzi hakutaarifiwa, au kama hakuna makubaliano yaliyofikiwa baina
ya timu kabla ya mchezo, basi idadi ya mabadiliko yanayokubalika haitazidi
wachezaji 6.
Kurejerea
mabadiliko:- mchezaji aliyekwisha kufanyiwa mabadiliko na kutoka kwa kadiri ya
kanuni za FIFA hatoruhusiwa tena kuingia uwanjani kucheza katika mchezo uleule.
Mabadiliko ya namna hii yatakubalika katika michezo ya ndondo tu kwa kadiri ya
makubaliano ya waandaaji wa hizo ndondo.
Utaratibu wa
Kufanya mabadiliko
Katika kila mchezo, majina ya wachezaji watakaofanyiwa mabadiliko yatakabidhiwa
kwa mwamuzi kabla ya mchezo kuanza. Mchezaji yeyote ambaye jina lake halitakuwa
miongoni mwa majina aliyokabidhiwa mwamuzi hatopaswa kucheza katika mchezo
husika.
Taratibu za
kufuata wakati wa kufanya mabadiliko:
§ Mwamuzi lazima ataarifiwe kabla ya
kufanya mabadiliko
§ Mchezaji anayetarajiwa kuingia
hatoruhusiwa kuingia dimbani mpaka yule anayetoka awe ametoka kwelikweli
uwanjani na kwamba mwamuzi atamuashiria yule anayeingia kwamba ‘sasa unaweza
kuingia bwana mkubwa’
§ Mchezaji anayeingia atapitia mstari
wa katikati ya dimba na kwamba atafanya hivyo wakati ambapo mchezo utakuwa
umesimama.
§ Mabadiliko yatakamilika pale
mchezaji anayeingia atakuwa ameingia dimbani
§ Mchezaji aliyetoka hatoruhusiwa tena
kucheza katika mchezo husika isipokuwa tu kama kanuni za ndondo zitatumika.
§ Mwamuzi atakuwa mwenye mamlaka ya
mwisho kama mchezaji aingie au asiingie.
Kubadili
mlindamlango:- mchezaji yeyote anaweza kubadilishana nafasi na mlindamlango
ikiwa tu mwamuzi atataarifiwa kabla mabadiliko kufanyika na kwamba mabadiliko
hayo yafanyike wakati mchezo umesimama.
UKIUKWAJI WA
SHERIA HII NA ADHABU ZAKE
Ikiwa kama mchezaji wa mabadiliko ataingia dimbani bila ruksa ya mwamuzi
yafuatayo yatatokea:
§ Mwamuzi atasimamisha mchezo (japo si
muda uleule ambao mchezaji atakuwa ameingi ama mchezaji huyo hataingilia
mchezo)
§ Mwamuzi atamuonesha kadi ya njano
kwa kufanya kitendo kisicho cha uanamichezo na kwamba atamuamuru atoke nje
§ Ikiwa kama mwamuzi atakuwa
alisimamisha mchezo, itabidi auanzishe kwa kupigwa mpira wa adhabu usio wa moja
kwa moja dhidi ya timu ya mchezaji aliyeingia uwanjani kienyeji.
Ikiwa kama yatafanyika mabadiliko kwa kutumia mchezaji ambaye hakutajwa katika
orodha ya wachezaji wa mabadiliko aliyokabidhiwa mwamuzi na kwamba mwamuzi
hakujulishwa juu ya mabadiliko hayo:
§ Mwamuzi atamruhusu yule mchezaji
aingie
§ Mchezaji aliyeingia hatapewa adhabu
yoyote
§ Idadi ya wachezaji wanaopashwa
kufanya mabadiliko katika orodha aliyopewa mwamuzi haitapunguzwa
§ Mwamuzi atatoa ripoti ya tukio hili
kwa mamlaka husika.
Ikiwa kama
mlinda mlango na mchezaji watabadilishana nafasi bila ufahamu wa mwamuzi,
mwamuzi ataruhusu mchezo uendelee mpaka pale mpira utakapotoka nje na ni hapo
mwamuzi atawalima kadi za njano wachezaji waliohusika.
Ikiwa kama
kutafanyika ukiukwaji mwingine wa kanunu hii tofauti na zilizotajwa, mchezaji
atakayehusika ataoneshwa kadi ya njano na mchezo utarejelewa tena kwa mpira wa
adhabu isiyo wa moja kwa moja dhidi ya timu ya mchezaji aliyevunja kanuni.
Kadi
nyekundu.
Mchezaji atakayeoneshwa kadi nyekundu kabla ya mchezo kuanza anaweza
kubadilishwa na mmoja wa wachezaji walio katika orodha ya mwamuzi ya wachezaji
wa mabadiliko.
Mchezaji wa mabadiliko aliyeoneshwa kadi nyekundu kabla au baada ya kuanza kwa
mechi hatoruhusiwa kufanyiwa mabadiliko tena.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 4: VIFAA VYA WACHEZAJI
==============
Usalama :- mchezaji hatakiwi kuvaa kifaa au kitu chochote hatarishi kwake au
kwa mchezaji mwenzake. Hii ni pamoja na vito vya thamani kama pete, mikufu n.k.
Vifaa muhimu
:- vifaa muhimu kwa ajili ya mchezaji vitakuwa ni pamoja na vifuatavyo:
§ Jezi yenye mikono – kama mchezaji
atakuwa amevaa nguo nyingine ndani, rangi ya mikono ya hiyo nguo ya ndani
itapaswa kuwa sawasawa na rangi ya mikono ya jezi.
§ Bukta – kama mchezaji atakuwa amevaa
nguo ya ndani kama vile taiti au , rangi ya hiyo taiti lazima iwe sawa na rangi
kuu ya bukta. Mfano kama rangi ya bukta ni nyekundu yenye michirizi mieupe,
basi rangi ya taiti itatakiwa kuwa na rangi nyekundu.
§ Soksi
§ Vikinga-ugoko (shinguargds)
§ Viatu – njumu
Maelezo
kuhusu vikinga-ugoko:
§ Lazima vifunikwe gubigubi na soksi
§ Vitatengenezwa ka mipira, plastiki,
au matirio yoyote inayofaa ya kufanana na hayo
§ Vitatakiwa kuwa kinga kwa miguu ya
mchezaji kwa kiwango fulani.
Rangi
§ timu zinazopambana zitavaa rangi
tofauti tofauti na rangi za timu zote mbili zitakuwa tofauti na rangi za
wamuzi.
§ Kila mlindamlango atavaa rangi
tofauti na wachezaji wenzake pamoja na waamuzi.
UKIUKWAJI WA
SHARIA HII NA ADHABU ZAKE
ikiwa kama sharia hii itakiukwa, mchezo hautasimama, ila mwamuzi atamuru
mchezaji aliyefanya makosa kutoka nje ya uwanja kusahihisha makosa yake ya
kiuvaaji.
Mchezaji atatoka nje ya uwanja pale mpira utakapokuwa umesimama kwa
sababu ya kutoka nje au sababu nyingine.
Mchezaji
yoyote atakayepaswa kutoka nje ya uwanja kwenda kurekebisha uvaaji wake
hatorudi ndani ya uwanja isipokuwa kwa kuruhusiwa na mwamuzi. Mwamuzi
atajiridhisha kwanza ikiwa kama mchezaji amerekebisha uvaaji wake kabla ya
kumruhusu kurejea uwanjani.
Mwamuzi
atamruhusu mchezaji kuingia pale tu mpira utakapokuwa umetoka nje ya uwanja.
Mchezaji
aliyeamuriwa kutoka kwenda kurekebisha uvaaji wake akirejea bila ruksa ya
mwamuzi atalimwa kadi ya njano.
Kurejelewa
kwa mchezo:- ikiwa kama mwamuzi atasimamisha mchezo kwa ajili ya kutoa adhabu
ya kadi ya njano, mchezo utarejelewa kwa kupigwa kwa mpira wa adhabu ndogo
dhidi ya timu ya mchezaji aliyepigwa kadi ya njano.
MSIMAMO WA
FIFA JUU YA SHERIA HII:
Kuhusu vifaa muhimu vya michezo:
Vifaa muhimu vya michezo havitakuwa na maneno au misemo au vijembe vya kisiasa,
au kiimani, au hata misemo binafsi, au picha zenye ujumbe fulani usioendana na
maudhui ya mchezo wa mpira wa miguu. Adhabu itatolewa dhidi ya timu ya mchezaji
atakaekiuka sheria hii.
Mavazi ya
ndani:
Wachezaji hawataruhusiwa kuonesha maandishi yaliyo katika nguo za ndani yenye
maudhui ya itikadi za kisiasa au imani za kidini isipokuwa kwa nembo ya
makampuni yaliyotengeneza hilo wazi. Mchezaji au timu ya mchezaji itakayokiuka
sheria hii itakumbana na rungu la FIFA.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria Namba 5: MWAMUZI
==============
Mamlaka ya
Mwamuzi
Kila mchezo utaendeshwa na mwamuzi ambaye atakuwa na mamlaka kamili ya
kuhakikisha sheria za soka zinafuatwa katika mchezo atakaokuwa amepangiwa
kuchezesha.
Nguvu na
Majukumu
Mwamuzi atahakikisha:
§ Sheria za soka zinafuatwa
§ Ataongoza mchezo kwa msaada wa
waamuzi wasaidizi na itakapobidi atasaidiwa pia na kamisaa
§ Atahakikisha kuwa mpira utakaotumika
unakidhi viwango vilivyobainishwa katika Sheria Namba 2
§ Atahakikisha kuwa vifaa vya
wachezaji vinakidhi Sheria Namba 4
§ Atadhibiti muda na kuweka kumbukumbu
ya matukio katika mchezo
§ Atasimamisha, kusubirisha au
kuahirisha mchezo kwa utashi wake ikiwa kama kuna sheria itakiukwa.
§ Atasimamisha, kusubirisha, au
kuahirisha mchezo ikiwa kutatokea sintofahamu ya aina yoyote kutoka nje ya
uwanja
§ Atasimamisha mchezo ikiwa kwa maoni
yake atajiridhisha kuwa kuna mchezaji ameumia sana na atahakikisha mchezaji
yule anaondolewa uwanjani. Mchezaji aliyeumia atarejea tu uwanjani baada ya
mchezo kuwa umeanza tena.
§ Ataruhusu mchezo uendelee mpaka pale
mpira utakapotoka nje ikiwa kwa maoni yake atajiridhisha kuwa kuna mchezaji
ameumia na kwamba mchezaji huyo hakuumia sana.
§ Atahakikisha kuwa mchezaji
anayetokwa na damu ametoka nje ya uwanja na kwamba mchezaji huyo atarudi tu
uwanjani ikiwa damu zitakuwa zimekoma kumtoka na kwamba hawezi kurudi kienyeji
mpaka pale mwamuzi atakapomuonesha ishara ya kumruhusu kurudi.
§ Ataruhusu mchezo uendelee ikiwa kama
timu iliyofanyiwa madhambi watanufaika na kuendelea kwa mchezo na kama
hawatanufaika mwamuzi atarejerea madhambi ya awali na kuruhusu kupigwa kwa
mpira wa adhabu.
§ Atamuadhibu mchezaji atakayefanya
madhambi mfululizo katika muda uleule mfupi
§ Atamchukulia hatua za kinidhamu
chezaji atakaefanya makosa ya kustahili kadi ya njano au kadi nyekundu lakini
atafanya hivyo tu mpaka pale mpira utakapokuwa umetoka nje.
§ Atachukua hatua dhidi ya maofisa wa
timu watakaoonesha utovu wa nidhamu na kwa utashi wake anaweza kuwaamuru kutoka
uwanjani.
§ Atachukua hatua kutokana na ushauri
wa mwamuzi msaidizi kwa matukio ambayo kwa bahati mbaya hakuona
§ Atahakikisha kuwa mtu asiyehusika
haruhusiwi kuingia uwanjani
§ Ataashiria kuanza kwa mchezo baada
ya kuwa umesimama
§ Atawakabidhi mamlaka ripoti ya
mchezo ambayo itaambatana na taarifa juu ya hatua za kinidhamu alizochukua
dhidi ya wachezaji au viongozi wa timu na matukio mengine ambayo yatatokea
kabla, wakati na baada ya mchezo.
Maamuzi ya
Mwamuzi
§ Maamuzi ya mwamuzi yatakuwa ya
mwisho. Hii ni pamoja na ikiwa kama goli limefungwa ama halikufungwa na matokeo
ya jumla ya mchezo.
§ Mwamuzi atabadili maamuzi ikiwa tu
kwa akili zake atagundua kuwa amekosea au kama atashauriwa na mwamuzi msaidizi
au kamisaa – lakini kwa sharti kwamba asijekuwa ameshaanzisha mchezo au
amemaliza mchezo.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria Namba
6: WAAMUZI WASAIDIZI
==============
Majukumu:- watateuliwa waamuzi wasaidizi wawili ambao majukumu yao yatakuwa
kama ifuatavyo:
§ Wataashiria mpira wote umetoka nje
ya uwanja
§ Wataashiria ni timu gani inapaswa
kupiga kona, goal kick, au kurusha mpira
§ Wataashiria ikiwa kama mchezaji
ameotea
§ Wataashiria kufanyika kwa
mabadiliko
§ Wataashiria juu ya matukio yoyote
ambayo mwamuzi wa kati atakuwa hakuona.
§ Wataashiria juu ya madhambi
yanayoweza kufanyika na wao kuona vema zaidi kuliko mwamuzi wa kati. Hii ni
pamoja na madhambi yanayofanyika katika eneo la penati.
§ Wataashiria ikiwa wakati wa upigaji
wa mkwaju wa penati, mlinda-mlango alihama kutoka mstari wa goli kabla ya
penati kupigwa na pia wataashiria kama mpira umevuka mstari au laa.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 7: MUDA WA MCHEZO
==============
Vipindi:- Mpambano wa soka utakuwa na vipindi viwili vya dakika 45 kila kimoja,
isipokuwa kama itakubaliwa vinginevyo kati ya mwamuzi wa kati na timu
zinazopambana.
Makubaliano yoyote ya kubadili muda wa vipindi vya mchezo mfano
kupunguza muda na kuwa dakika 40 kutokana na kutokuwa na mwanga wa kutosha
uwanjani lazima yafanyike kabla ya kuanza kwa mchezo na yakidhi kanuni za
mashindano husika.
Mapumziko:-
wachezaji wanastahili kupata mapumziko ambayo hayatazidi dakika 15.
Hata hivyo
kanuni za mashindano zitatakiwa kubainisha muda halisi wa mapumziko na
mabadiliko yoyote juu ya urefu wa muda wa kupumzika lazima yapate idhini ya
mwamuzi wa kati.
Muda wa
nyongeza:- kutakuwa na muda wa dakika za nyongeza kwa vipindi vyote viwili
utakaotokana na kupotea kwa muda kutokana na yafuatayo:
§ Kufanyika kwa mabadiliko
§ Kuhudumia mchezaji aliyeumia
§ Kumuondoa uwanjani mchezaji
aliyeumia
§ Upotezaji wa muda makusudi
§ Sababu nyingine yoyote
Ieleweke katika sharia hii kwamba dakika za nyongeza zitatolewa kwa hiari ya
mwamuzi wa kati.
Kupigwa kwa
penati:- ikiwa kama kutatakiwa kupigwa kwa mkwaju wa penati, muda wa kipindi
husika utaongezwa mpaka pale mkwaju huo wa penati utakapopigwa – zege halilali.
Mchezo
uliokatishwa:- huu utarudiwa isipokuwa tu kama kanuni za mashindano husika
zitabainisha vinginevyo.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 8: KUANZA KWA MCHEZO
==============
Mwamuzi
ataanzisha mchezo ikiwa:-
§ Itakuwa mwanzo kabisa wa mpambano
§ Baada ya goli kuwa limefungwa
§ Mwanzoni mwa kipindi cha pili au
dakika za nyongeza (extra time) pale inapobidi
Utaratibu
Kabla ya kuanza kwa mchezo au kuanza kwa kipindi cha dakika za nyongeza
yafuatayo yatafanyika:-
§ mwamuzi atarusha sarafu na timu
inayopatia (kama ni mkia au kichwa) itachagua goli la kushambulia katika dakika
45 za kwanza za mchezo.
§ Timu iliyokosea jibu katika zoezi la
urushaji wa sarafu itaanzisha mchezo
§ Timu iliyopatia jibu katika zoezi ka
kurusha sarafu itaanzisha mchezo wakati wa kuanza kwa kipindi cha pili
§ Wakati wa kipindi cha pili timu
zitabadilishana magoli
Kuanza kwa
mchezo baada ya goli kuwa limefungwa:-
§ Baada ya kufungwa kwa goli, timu
iliyofungwa itaanzisha mchezo
§ Wachezaji wa kila timu watakuwa upande
wao wa uwanja wakitenganishwa na mstari wa kati
§ Wachezaji wa timu pinzani ya ile
inayoanzisha mchezo watakuwa umbali wa mita 9.15 (yadi 10) kutoka ulipo mpira
mpaka pale mchezo utakapokuwa umeanza
§ Mpira lazima uwe katikati ya uwanja
na ukiwa umetulia
§ Mwamuzi atatoa ishara ya kuanza kwa
mchezo
§ Mpira utakuwa tayari kuchezwa ikiwa
utapigwa na kuanza kutembea
§ Mchezaji alieanzisha mchezo hatakiwi
kuugusa tena mpira ule mpaka pale utakapokuwa umeguswa na mchezaji mwingine
Ukiukaji wa
sheria hii
Ikiwa kama mchezaji anayeanzisha mchezo ataugusa tena mpira kabla haujaguswa na
mchezaji mwingine:
§ Mpira wa adhabu ndogo utapigwa dhidi
ya timu ya mchezaji huyo
Ikiwa kama kutatokea ukiukwaji mwingine tofauti:
§ Mwamuzi ataamuru mchezo uanzishwe
tena
Kudundisha
mpira :- ni namna ya mwamuzi kuanzisha mchezo upya na hii itatokea wakati
mchezo ukiwa unaendelea na mwamuzi atalazimika kusimamisha mchezo kwa sababu
yoyote ambayo hata isiyo andikwa kwenye sharia 17 za soka.
Utaratibu wa kudundisha mpira
Mwamuzi ataudundisha mpira pahala ulipokuwa wakati akisimamisha mchezo
isipokuwa tu kama mchezo ulisimama mpira ukiwa eneo la goli ambapo katika hali
kama hii mwamuzi ataudundisha mpira katika mstari uliosambamba na mstari wa
goli pahala ulipokuwa mpira kipindi mwamuzi anasimamisha mchezo. Mpira utakuwa
tayari kuchezwa pale tu utakapogusa chini.
Mwamuzi
atadundisha mpira tena:
§ Kama utaguswa na mchezaji kabla
haujagusa chini
§ Kama mpira utatoka baada ya kugusa
chini
Kama mpira wa kudundisha utatinga nyavuni?
Kama mpira wa kundundisha utapigwa na kuingia nyavuni kwa goli la timu pinzani,
mpira wa goal kiki utapigwa
Kama mpira wa kudundisha utaingia nyavuni na kuzaa goli la kujifunga, timu
pinzani watapewa kona.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 9: MPIRA UMETOKA AU HAUJATOKA?
==============
MPIRA
UMETOKA NJE
Mpira utakuwa umetoka nje ya dimba ikiwa:
§ Mpira wote utakuwa umevuka mstari wa
goli au mstari wa pembeni iwe ni ikiwa upo chini au hewani. ‘wote’ maana yeka
kusiwe na sehemu ya mpira inabaki juu ya mstari.
§ Mwamuzi atakuwa amesimamisha mchezo
(kumbuka wakati wa mapumziko na baada ya mechi mwamuzi hubeba mpira na kuondoka
nao)
MPIRA
HAUJATOKA NJE
Mpira utakuwa ndani ya dimba muda wote ikiwa ni pamoja na:
§ Utakapogonga mlingoti wa goli au
mtambaa-panya au mlingoti wa kibendera cha kona na kurudi dimbani
§ Utakapomgonga mwamuzi wa kati au
msaidizi wake lakini sharti wawe dimbani
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 10: NAMNA YA KUFUNGA GOLI
==============
NI GOLI AU
SIYO GOLI?
Itahesabika kuwa limefungwa goli ikiwa mpira wote utavuka mstari wa goli ulio
kati ya milingoti miwili ya goli na chini ya mtambaa-panya. Hata hivyo timu
inayofunga goli isiwe imekiuka kanuni wakati wa harakati za kufunga hilo goli.
NANI KASHINDA?
Timu itakayofunga magoli mengi kuliko mwenzake wakati wa mchezo itatangazwa
mshindi wa mchezo husika. Ikiwa kama timu zinazopambana zitafunga idadi sawa ya
magoli au ikiwa kama hakutakuwa kumefungwa goli lolote, mchezo utaamuliwa kuwa
sare au suluhu.
KANUNI ZA
MASHINDANO
Ikiwa kama kanuni za mashindano zinataka lazima apatikane mshindi baada ya
mpambano au baada ya mechi za nyumbani na ugenini, utaratibu pekee unaokubalika
kumpata mshindi ni:
§ Goli la ugenini
§ Muda wa nyongeza
§ Mikwaju ya penati
TEKNOLOJIA
YA GOLI
Teknolojia ya goli au kwa kimombo goal-line technology (GLT) inaweza kutumika
kwa kusudi la kuthibitisha ikiwa kama goli limefungwa au laa. Kutumika au
kutokutumika kwa GLT lazima kuwe kumebainishwa katika kanuni za mashindano
husika.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 11: KUOTEA
==============
Angalizo:-
siyo kosa kisheria kwa mchezaji kuotea. Kwa hiyo mchezaji hatapewa kadi ya
njano wala nyekundu eti kisa kaotea. Wala hataonywa kwa maneno na mwamuzi. Yeye
aotee tu anavyotaka hata mara mia atajujuwa mwenyewe.
Hata hivyo
mchezaji atakuwa ameotea ikiwa:
§ Atakuwa karibu na mstari wa goli la
timu pinzani kuliko mpira wenyewe na mlinzi wa mwisho
Mchezaji atahesabika hakuotea ikiwa:
§ Atakuwa upande wa nusu ya uwanja
inayohusu timu yake
§ Atakuwa katika mstari sambamba na
mlinzi wa mwisho wa timu pinzani
§ Atakuwa sambamba na walinzi wawili
wa mwisho wa timu pinzani
Makosa
Mwamuzi atapuliza kipyenga cha kuotea ikiwa mchezaji anayedhani kuwa yupo
katika nafasi ya kuotea ataingilia mchezo.
Mfano mchezaji amezidi/ameotea
halafu mara ghafla anarudi ndani haraka-haraka kutaka kupokea pasi hapo mwamuzi
lazima apulize kipyenga cha kuashiria kuwa mchezaji huyo ameotea.
Hakuna Makosa
§ Ikiwa mchezaji aliye katika nafasi
ya kuotea atapokea mpira wa goal-kick
§ Ikiwa mchezaji aliya katika nafasi
ya kuotea atapokea mpira wa kurusha
§ Ikiwa mchezaji aliye katika nafasi
ya kuotea atapokea mpira wa kona
Ukiukwaji wa
sharia hii na adhabu zake
Pale itakapotokea kuwa mchezaji ameotea, mwamuzi ataamuru upigwe mpira wa
adhabu ndogo dhidi ya timu pinzani.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba 12: MAKOSA MBALI MBALI NA UTOVU WA NIDHAMU
==============
Itakapotokea
mchezaji anafanya makosa au utovu wa nidhamu hatua zifuatazo zitachukuliwa:
Mpira wa
Adhabu wa Moja kwa Moja :- adhabu hii itatolewa dhidi ya timu pinzani ikiwa
kama mchezaji wao atafanya moja kati ya makosa yafuatayo:
§ Atamkanyaga makusudi au atadhamiria
kumkanyaga makusudi mchezaji wa timu pinzani
§ Atamkwatua au kudhamiria kumkwatua
mchezaji wa timu pinzani
§ Atamrukia mchezaji wa timu pinzani
§ Atampamia makusudi mchezaji wa timu
pinzani
§ Atampiga au atadhamiria kumpiga
mchezaji wa timu pinzani (mfano kupiga kiwiko)
§ Atamsukuma mchezaji wa timu pinzani
§ Atakaba vibaya badala ya kucheza
mpira ataukosa na kumuumiza mcheza ji wa timu pinzani (tackling)
Vilevile,
mpira wa adhabu wa moja kwa moja utaamuriwa upigwe ikiwa yafuatayo yatatendeka:
§ Mchezaji atamkamata makusudi mchezaji
wa timu pinzani
§ Mchezaji atamtemea mate mchezaji wa
timu pinzani
§ Ataushika mpira makusudi ndani ya
eneo la penati (isipokuwa kwa mlindamlango tu)
Penati
Mpira wa
penati utapigwa ikiwa lolote kati ya makosa 10 yaliyobainishwa hapo juu
yatafanyika na mchezaji ndani ya eneo la penati la timu yake, bila kujali eneo
kosa limefanyikia, cha muhimu tu iwe ndani ya eneo la penati la maguu 18.
Mpira wa adhabu ndogo
Mpira wa
adhabu ndogo utapigwa dhidi ya timu pinzani ikiwa mlindamlango ndani ya eneo
lake la kujidai atafanya lolote kati ya haya yafuatayo:
§ Atakaa na mpira kwa zaidi ya sekunde
6 bila kuuachia au kuupiga ili mchezo uendelee
§ Ataudaka mpira. Atauachia. Lakini
kabla haujaguswa na mchezaji mwingine ataudaka tena.
§ Atadaka mpira wa kurusha uliorushwa
kwake moja kwa moja na mchezaji wa timu yake
Mwamuzi pia
ataamuru upigwe mpira wa adhabu ndogo ikiwa kwa maoni yake atahisi mchezaji:
§ Amecheza mchezo wa hatari
§ Amemzuia mchezaji wa timu pinzani
kuambaa na mpira
§ Atamzuia mlindamlango asipige au
kuuachia mpira aliodaka
§ Atafanya lolote tofauti na
yaliyotajwa hapo awali ambapo katika hali kama hiyo mwamuzi atasimamisha mchezo
na kutoa kadi ya njano au nyekundu kwa muhusika
Hatua za
kinidhamu
Kadi ya manjano itatumika kuashiria kuwa mchezaji ameonywa
Kadi nyekundu itatumika kuashiria kuwa mchezaji ametolewa nje.
Anayestahili kupewa kadi ya manjano au nyekundu ni mchezaji tu awe uwanjani au
nje ya uwanja
Mwamuzi ana mamlaka ya kutoa adhabu dhidi ya mchezaji kuanzia mchezo unapoanza
mpaka unapokamilika
Mchezaji atakaetenda kosa la kustahili kadi ya manjano au nyekundu iwe yupo
uwanjani au nje, iwe ni dhidi ya mchezaji wa timu pinzani au mchezaji wa timu
yake au mwamuzi au mwamuzi msaidizi ataadhibiwa kutokana na aina ya kosa.
Makosa
yanayostahili kadi ya manjano
§ Tabia zisizo za kiwanamichezo
§ Utovu wa nidhamu kwa maneno au kwa
vitendo
§ Kukiuka sheria mara kwa mara
§ Kuchelewesha kuanzisha mchezo
makusudi
§ Kutokutii kukaa umbali unaokubalika
wakati wa kupigwa kwa kona, mpira wa adhabu au mpira wa kurusha
§ Kuingia uwanjani bila ruksa ya
mwamuzi
§ Kutoka uwanjani makusudi bila ruksa
ya mwamuzi
Mchezaji
aliye katika benchi la ufundi atapewa kadi ya manjano ikiwa:
§ Ataonesha vitendo visivyo vya
kiwanamichezo
§ Ataonesha utovu wa nishamu kwa
maneno au kwa vitendo
§ Atachelewesha kuanzisha mchezo kwa
makusudi
Kadi
nyekundu
Mchezaji ataoneshwa kadi nyekundu na kutolewa nje ya uwanja ikiwa atafanya
makosa yafuatayo:
§ Kucheza faulo ya hatari
§ Kufanya kitendo cha vurugu
§ Kumtemea mate mchezaji wa timu pinzani
au mtu yeyote
§ Kuzuia timu pinzani wasipate goli
kwa kushika mpira makusudi ndani ya eneo la penati (hii lakini haihusiani na
mlindamlango akishika mpira ndani ya eneo lake la kujidai)
§ Kuzuia timu pinzaniw asipate goli la
dhahir shahir kwa kumcheza rafu mchezaji anayeambaa kwenda kufunga
§ Kutumia lugha ya matusi, kashfa au
kuonesha ishara mbaya
§ Kupewa kadi ya pili ya njano katika
mchezo huohuo.
Mchezaji aliyepewa kadi nyekundu hatakiwi kuonekana eneo la karibu na dimba na
wala asikae katika benchi la ufundi la timu yake.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria namba
13: MPIRA WA ADHABU
==============
Aina za mpira wa adhabu. Ziko mbili:
§ Mpira wa adhabu wa moja kwa moja
§ Mpira wa adhabu ndogo
Mpira wa
adhabu wa moja kwa moja:
§ Ukipigwa na kuzama moja kwa moja
golini kwa timu pinzani, goli litahesabika
§ Ukipigwa na kuzama katika goli la
timu inayopiga huo mpira, refa ataamuru kona
Mpira wa
adhabu ndogo:
Ishara:-mwamuzi ataashiria adhabu ya mpira wa adhabu ndogo kwa kunyanyua mkono
wake juu na ataendelea kuuacha mkono wake wima mpaka pale adhabu itakapochezwa
na kwamba baada ya kuwa umepigwa mpira lazima umguse mchezaji mwingine au utoke
nje.
Kufunga goli
kwa mpira wa adhabu ndogo:
Goli la mpira wa adhabu ndogo litahesabika tu ikiwa baada ya mpira kuwa
umepigwa, utamgusa mchezaji mwingine ndiyo uingie golini. Kinyume na hapo:
§ Kama mpira wa adhabu ndogo utapigwa
moja kwa moja na kutinga nyavuni bila kuguswa na mtu yeyote mwamuzi ataamuru
goal kiki.
§ Kama mpira wa adhabu ndogo utapigwa
moja kwa moja na kuzaa goli la kujifunga, mwamuzi ataamuru kona.
Kuhusu Utaratibu:
Kwa adhabu zote mbili mpira utatakiwa kutulia kwanza kabla ya kupigwa na kwamba
mpigaji hatakiwi kuugusa tena mpira ule mpaka uwe umeguswa na mchezaji
mwingine.
Pahala pa kupigia
mpira wa Adhabu:
§ Kwa mpira wa adhabu ndani ya eneo la
penati dhidi ya timu inayoshambulia(hii ni kwa adhabu za aina zote moja kwa
moja na adhabu ndogo):
ü Wachezaji wa timu inayoshambulia
watakaa umbali wa yadi 10 kutoka ulipo mpira
ü Wachezaji wa timu inayoshambulia
watakaa nje ya eneo la penati mpaka pale mpira utakapopigwa
ü Wachezaji wa timu inayoshambulia
wataruhusiwa kuucheza mpira pale utakapokuwa umetoka nje ya eneo la penati.
ü Kama kutafanyika madhambi ndani ya
eneo la goli – maguu 12, mpira utatengwa popote
§ Mpira wa adhabu ndogo dhidi ya timu inayoshambuliwa:
ü Wachezaji wa timu inayoshambuliwa
watakaa umbali wa yadi 10 kutoka ulipotengwa mpira mpaka pale utakapochezwa
isipokuwa tu kama watakuwa wamejipanga kwenye mstari wa goli.
ü Mpira utakuwa tayari kuchezwa pale utakapopigwa na kuanza
kutembea
ü Ikitokea adhabu inaamuliwa ndani ya
eneo la goli, mpira utatengwa juu ya mstari ulio sambamba na mstari wa goli.
Ukiukwaji wa
sheria hii na adhabu zake:
§ Kama wakati wa kupiga mpira wa
adhabu, mchezaji wa timu pinzani atakaa karibu kuliko vile inavyotakiwa
kisheria, muamuzi ataamuru adhabu ipigwe tena.
§ Kama mpira wa adhabu utapigwa na
timu iliyokuwa inashambuliwa kutoka eneo lao la penati ukawa haujatoka nje ya
eneo la penati, muamuzi ataamuru adhabu ipigwe tena.
Mpira wa
adhabu unaopigwa na mchezaji mwingine tofauti na golikipa:
§ Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa
na kisha mchezaji yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa tena kabla haujaguswa na
mchezaji mwingine, mwamuzi ataamuru upigwe mpira wa adhabu ndogo.
§ Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa
na kisha mchezaji yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa kwa mkono kabla haujaguswa
na mchezaji mwingine:
ü muamuzi ataamuru mpira wa adhabu wa
moja kwa moja
ü muamuzi ataamuru penati ikiwa makosa
haya yatafanyika ndani ya eneo na penati
Mpira wa
adhabu unaopigwa na golikipa
§ Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa
na kisha golikipa yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa tena (siyo na mikono)
kabla haujaguswa na mchezaji mwingine muamuzi ataamuru mpira wa adhabu ndogo.
§ Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa
na kisha golikipa yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa tena na mikono kabla
haujaguswa na mchezaji mwingine:
ü Muamuzi ataamuru ipigwe adhabu ya
mpira wa adhabu wa moja kwa moja kama golikipa ameushika mpira nje ya eneo la
penati.
ü Muamuzi ataamuru mpira wa adhabu
ndogo ikiwa golikipa kaushika tena mpira ule ndani ya eneo la penati.
Panapo majaaliwa tutaendelea...
|
No comments:
Post a Comment