|
Mkuu wa Idara ya Habari
na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na
masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3.
Jerry amefungiwa leo
baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es
Salaam.
Na amefungiwa baada ya
kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF
mbele ya Kamati ya Ogunde.
Makosa yaliyomtia
hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015
alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini
amekaidi kulipa hadi leo.
Kwa kosa hilo
akahukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja- wakati shitaka
lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea
mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
Katika shitaka hilo,
Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga SC kuwafanyia vurugu mashabiki wa
Simba SC kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka
huu,2016 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Alihamasisha mashabiki
wa Yanga kufanya vurugu katika mechi dhidi ya Maembe kwa kusema mashabiki wa
Simba hawana haki ya kuingia uwanjani, kwa sababu Uwanja umekodiwa na Yanga. Na
hili Kamati ilijiridhisha baada ya kusikiliza sauti zake alipokuwa akihojiwa na
vituo vya Redio,”kimesema chanzo kutoka kwenye Kamati hiyo.
Kwa kosa hilo Jerry
Muro amefungiwa mwaka mmoja pia na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 ingawa adhabu
zote zinakwenda sambamba – maana yake atakuwa pembeni na masuala ya soka kwa
mwaka mmoja tu.
Hata hivyo, Jerry Muro
alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho
hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni.
“Kamati ilisikiliza kwa
makini taarifa zake alipokuwa anazungumza na vituo vya Redio na kugundua
alikuwa sahihi, hivyo hapa hana hatia,”kimesema chanzo.
Hata hivyo, Jerry Muro
amehukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao na inadaiwa hakutoa taarifa
ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
Badala yake, imeelezwa
Katibu wa Yanga SC, Baraka Deusdedit alifika mapema Jana Julai 07,2016, kabla ya kikao kwa ajili ya
kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro amekwenda kwao Kilimanjaro kusafisha
makaburi ya wazee wake.
Lakini Kamati ikaamua
kuendelea na kikao kwa mujibu wa kanuni na hatimaye kuchukua hatua ilizochukua.
Hata hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF.
|
No comments:
Post a Comment