Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunga “Zoezi la
Onesha Uwezo Medani” lililoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi
Kavu ambalo ni sehemu ya Jeshi la wananchi Tanzania katika eneo la Lang’arurusu
nje kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.
Akizungumza
na Askari na Maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo,
Rais Magufuli amesema katika awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria
kulitumia Jeshi la wananchi Tanzania katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha
viwanda na kampuni za ujenzi ili kuharakisha maendeleo.
Ametoa mfano
wa kiwanda cha Nyumbu ambacho kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na
kueleza kuwa wakati umefika wa kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili
kiweze kufanya uzalishaji mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali
ilivyo hivi sasa.
“Zipo nchi
nyingi ambazo majeshi yao yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya
kupigiwa mfano, wakati umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi
na viatu, hatuna sababu ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza
sisi wenyewe” Alisisitiza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli amelipongeza Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa “Zoezi
Onesha Uwezo Medani” ambalo limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao
katika jukumu lake la kiulinzi.
Ameahidi
kuwa ataendeleza juhudi zilizofanywa na viongozi wenzake waliotangulia za
kuliimarisha kwa vitendea kazi na maslai ya wanajeshi ili liweze kutekeleza
wajibu wake bila vikwazo.
Pamoja na
kuwapongeza Askari na maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika
zoezi hilo, Rais Magufuli ameagiza Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga
Taifa (JKT) walioshiriki zoezi hilo kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.
Akitoa
maelezo ya awali kabla ya hotuba ya Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na
kusimamia juhudi za kuliboresha jeshi hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa
wanajeshi ili kuwajengea uwezo na morali ya kutekeleza majukumu yao ya kuilinda
nchi, pamoja na kutoa msaada stahiki kwa nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani
popote duniani.
Kwa upande
wake Mkuu wa majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange
amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na
litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na
uzalendo mkubwa.
Kabla ya
kuwahutubia maafisa wa jeshi la wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria
ufungaji wa “Zoezi Onesha Uwezo Medani”, Rais Magufuli ameoneshwa zana
mbalimbali za kivita ikiwa ni pamoja na kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa
mafupi, masafa ya kati na masafa marefu.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
22 Januari,
2016.
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange wakati
waufungaji wa zoezi la Onesha Uwezo Medani lililofanyika Monduli nje kidogo ya
Jiji la Arusha.
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akijadiliana jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis
Mwamunyange wakati akielekea kupewa maelezo ya zoezi zima la Onesha Uwezo
Medan.
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi katika tukio hilo la Ufungaji.
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akielekea
kwenye uwanja wa maonesho akiwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini
General Davis Mwamunyange.
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
katika picha ya pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi mara baada ya
kufunga zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha.
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipewa
maelezo ya zana mojawapo ya Kivita katika Zoezi la Onesha Uwezo Medani Mkoani
Arusha… Picha na IKULU.
Source:-Mpekuzi.
|
No comments:
Post a Comment