LEO JAN 27,2016 BUNGENI DODOMA:-Serikali Yatoa Ufafanuzi Juu Ya Kutorusha Matangazo Ya Bunge. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, January 27, 2016

LEO JAN 27,2016 BUNGENI DODOMA:-Serikali Yatoa Ufafanuzi Juu Ya Kutorusha Matangazo Ya Bunge.


Hali ya Sintofahamu imetawala Bungeni jioni hii ya leo January 27, 2016 kufuatia wabunge wa Upinzani kupinga TBC kusitisha kurusha live matangazo ya moja kwa moja kuanzia jana, January 26, 2016 kwa kigezo cha kubana matumizi.

Kutokana na vurugu hizo, Polisi wamelazimika kuingia Bungeni na kuwatoa nje wabunge wa Upinzani kufuatia kugoma kutokana na maagizo ya Mwenyekiti wa Kikao cha Bunge, Andrew Chenge.

 Chanzo cha vurugu hizo  ni  Wabunge wa Upinzani kupinga kuendelea kwa mjadala wa Bunge wakitaka kauli ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuhusu TBC kusitisha kurusha matangazo ya moja kwa moja toka Bungeni  ijadiliwe kwanza.

Sakata hilo liliibuka tangu asubuhi ambapo Mwenyeki wa Bunge, Andrew Chenge aliahirisha Kikao cha Bunge mara mbili huku akiitaka kamati ya uongozi kukutana  ili kutoa majibu.

Maamuzi ya kamati ya uongozi.
 
Baada ya Bunge kurejea jioni hii mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge ameliambia,Bunge kuwa maamuzi ya kamati ya uongozi baada ya kuketi mchana wa leo ni kama ifuatavyo.


(a) Mwenyekiti wa Bunge alikuwa sahihi kutaka hoja iliyokuwa mbele ya Bunge kuhusu hotuba ya Rais iendelee.



(b) Hakuna haki yoyote ya Bunge iliyovunjwa kwa Bunge kuendelea na kazi yake baada ya hoja ya Waziri



(c) Hoja ya Bunge iliyo mbele ya Bunge ni hotuba ya Rais na kamati ya uongozi imeagiza shughuli ziendelee kama kawaida.



(d) Endapo kuna Mbunge yoyote ambaye hataridhika atumie kanuni ya 5 (4) kuomba kibali kwa katibu wa bunge ili apate nafasi maalumu.

Aidha kwa mujibu wa ratiba ya kikao cha Bunge ni kwamba Bunge litajadili hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 Novemba 20, 2015 kwa muda wa siku 3. Baada ya kauli hii, vurugu ziliibuka Bungeni


Wabunge  wa  Upinzani walianza kupiga mayowe, ikiwemo kuimba nyimbo mbalimbali suala lililomlazimu Mwenyekiti kuwaondoa Wabunge wa Ukawa wote watoke nje ili wabunge wengine waendelee na kikao cha kujadili hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Wabunge wa CCM wako Bungeni wanaendelea na kikao cha Bunge.

Waziri wa Habari,Utamaduni, Wasanii,na Michezo  Nape Nnauye akitoa  kauli Bungeni mjini Dodoma Januari 27, 2016. 

Hapo majira ya Asubuhi,Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliahirisha bunge mara mbili kutokana na mvutano ulioibuka baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuomba bunge liahirishe kujadili hotuba ya rais na badala yake wajadili kuzuiwa kwa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) kurusha matangazo ya moja kwa moja.

Kabla ya kuahirishwa kwa bunge, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliwasilisha taarifa ya serikali kulieleza bunge kwamba, serikali imesitisha huduma ya matangazo ya moja kwa moja kupitia TBC.

Kutokana na taarifa hiyo, Zitto alisimama na kuliomba bunge kusitisha shughuli za kuendelea kujadili hotuba ya rais ambayo ilianza kujadiliwa jana ili kutoa fursa kujadiliwa hatua ya serikali kuzuia haki ya wananchi kupata matangazao ya moja kwa moja kupitia televisheni hiyo.

Hata hivyo, Chenge alianza kuonesha nia ya kutaka kuzima hoja ya Zitto lakini wabunge wa upinzani kwa umoja wao waliungana na Zitto katika kushikilia msimamo wa kujadiliwa suala la TBC kabla ya kuendelea na mjadala wa hotuba ya rais.

Yalisikika maneno kama ‘usituburuze, mtemi, hapa hakuna kuburuzana’ huku wabunge wengine wakipiga kelele kuashiria kuunga mkono hoja ya Zitto.

Kutokana na mvutano huo, Chenge alilazimika kuagiza kamati ya uongozi kukutana ili kujadili taarifa hiyo na baadaye kuwasilisha kulichojadiliwa na kamati hiyo.

“Naipa kamati saa moja,” alisema Chenge jambo ambalo lilipokelewa kwa mikono miwili na upinzani. Baada ya kauli hiyo mwenyekiti huyo aliahirisha bunge kwa saa moja.

Hata hivyo, baada ya bunge hilo kurejea tena baada ya kupita saa moja , Chenge aliahirisha tena bunge kwa kuwa, kamati ilikuwa haijamaliza kujadili.

Wakati akizungumza bungeni wakati wa kuwasilisha kauli ya serikali Nape alisema, “naomba kutoa kauli ya serikali kuhusu TBC kutangaza moja kwa moja vikao vya majadiliano ya bunge.”

TBC ilianza kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005. Kabla ya kuanza kurusha moja kwa moja, TBC wakati huo televisheni ya taifa ilikuwa inarekodi matukio yote ya bunge na kurusha usiku katika vipindi maalumu vilivyojulikana kama bungeni leo kwa maana ya yaliyojiri ndani ya bunge kwa siku husika.

Hata hivyo Nape alisema “baada ya kuanza kwa utaratibu wa kuanza kurusha matangazo moja kwa moja mwaka 2005, gharama za kufanya kazi hio zimekua zikipanda kwa kasi hadi kufikia Sh. 4.2 bilioni kwa mwaka kwa maana ya mikutano minne ya bunge.

“Shirika limekuwa likigharamia kwa sehemu kubwa matangazo hayo kwa kutumia mapato yake yanayotokana na matangazo madogo madogo ya biashara, ifahamike kuwa asilimia 75 ni vipindi vingi vinavyolenga kutoa elimu kwa umma na asilimia 25 ni burudani.”

Nape amesema, kutokana na hali hii, TBC imeona ni busara kubadilisha mfumo wa utangazaji wa shughuli za bunge ili kukabiliana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Amesema TBC imeona ni busara kuanzia mkutano huu wa bunge iwe inarusha baadhi ya matangazo ya bunge moja kwa moja yaani ‘live’ ikiwa ni njia ya kubana matumizi.

Amefafanua kuwa, “chini ya utaratibu huu, TBC itahakikisha kuwa, baadhi ya matukio ya matukio ya bunge yatarushwa moja kwa moja na mengine kurekodiwa na kuandaliwa kipindi maalum kitakachoitwa leo katika bunge.

“Kipindi hiki kitakua na mambo yote muhimu yaliyojiri ndani ya bunge kwa siku husika. Kipindi hichi kitakuwa kinarushwa kuanzia saa nne usiku hadi saa tano usiku.”

HAPA CHINI TAZAMA VIDEO KWA KUBOFYA PLAY.

Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za  Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga  na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630 .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad