AZIMIO LA
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA KUHUSU TANGAZO LA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI
YS ZANZIBAR LA KUITISHA UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR.
Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi),
likiwa ndiyo chombo cha juu cha maamuzi katika Chama baada ya Mkutano Mkuu wa
Taifa, limefanya kikao cha dharura leo, tarehe 28 Januari, 2016, katika Ofisi
Kuu ya CUF, mjini Dar es Salaam.
Kikao hicho
kilikuwa na ajenda moja tu, ambayo ni kufanya maamuzi kuhusiana na tangazo la
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar la kuitisha uchaguzi wa marudio.
Baada ya
kujadili kwa kina tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,
Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi, 2016 na
mwenendo mzima wa hali ya kisiasa Zanzibar tokea alipotoa tamko lake batili la
tarehe 28 Oktoba, 2015 kudai kwamba amefuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe
25 Oktoba, 2015 na matokeo yake, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia
maazimio yafuatayo:
1. KWAMBA
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar umeshafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015, ambapo kwa
upande wa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ulikwisha
kamilika na washindi wote kupewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kama
washindi halali.
Kwa upande
wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, matokeo yalikwisha bandikwa nje ya vituo vya
majumuisho vya majimbo yote 54.
Kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni
kuhakiki matokeo hayo kutoka majimboni na kazi hiyo ilikwishakamilika kwa
majimbo 40 na katika hayo, matokeo ya uchaguzi wa Rais kwa majimbo 31
yalikwishatangazwa kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salum Jecha,
kutangaza isivyo halali kwamba ameufuta uchaguzi huo.
2. KWAMBA
Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa
kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani
uchaguzi halali ulishafanyika.
3. KWAMBA
linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini
katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu
kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.
4. KWAMBA
sababu kuu ya Baraza Kuu kufikia maamuzi haya ni kutokana na matamko yote
mawili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha,
kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi
ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.
Hakuna
kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar
kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa
Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio.
5. KWAMBA
linazipongeza na limetiwa moyo sana na taasisi na jumuiya zote za kimataifa na
kikanda zikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa
Ulaya (European Union), Umoja wa Afrika (African Union), Jumuiya ya Maendeleo
ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja
na nchi za Marekani na Uingereza kwa msimamo wao wa kuungana na Wazanzibari na
kutetea haki yao ya kidemokrasia na maamuzi halali waliyoyafanya katika uchaguzi
mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kutaka mchakato wa uchaguzi huo ukamilishwe
na matokeo yake kutangazwa.
6. KWAMBA
linazipongeza na kutiwa moyo pia na taasisi za hapa nchini zikiwemo taasisi na
jumuiya za kidini, taasisi za haki za binadamu, vyombo huru vya habari, vyama
vyengine vya siasa na Wazanzibari na Watanzania wote wanaopenda amani na
demokrasia kwa msimamo wao wa kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya
katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kuendelea kusisitiza haja ya
kuheshimu na kufuata Katiba na Sheria za nchi yetu na pia haja na umuhimu wa
kutunza amani ya nchi yetu kwa kutaka haki itendeke.
Baraza Kuu
linazihakikishia taasisi na jumuiya hizo zote na pia kuwahakikishia Wazanzibari
na Watanzania wote kwamba CUF itaendelea kusimama kidete katika kulinda na
kutetea Katiba na Sheria za nchi yetu na pia kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya
tarehe 25 Oktoba, 2015.
7. KWAMBA
limesikitishwa na kushangazwa na kitendo cha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi, kuandika barua na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kutaka
vyama vya siasa vishiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20
Machi, 2016 bila ya kujali kwamba uchaguzi huo ni haramu na unakiuka matakwa ya
Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.
Baraza Kuu halikutarajia mtu mwenye hadhi ya
Ujaji kufanya kazi ya kutumikia maslahi ya watawala ambao wameamua kuvunja
Katiba na Sheria za nchi yetu na kukanyanga misingi ya haki na demokrasia huku
akishindwa kukemea uhuni mkubwa uliofanywa wa kubaka demokrasia na haki za
watu.
8. KWAMBA
limesikitishwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, kukwepa dhamana na wajibu wake kama Mkuu wa
Nchi na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuiacha njiani kazi aliyoianza ya kutafuta
ufumbuzi wa mkwamo wa uchaguzi Zanzibar.
Baraza Kuu linamtaka Rais Magufuli
kujitathmini na kujiuliza anajiweka vipi na kutoa taswira gani mbele ya macho
ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake
aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya
kazi na vyama vya CUF na CCM ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu.
9. KWAMBA
linalaani matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri
ya Muungano na Vikosi vya SMZ dhidi ya wananchi wasio na hatia na ambao
wamekuwa watulivu licha ya vitendo vingi vya uchokozi wa makusudi na hata
mashambulizi ya hujuma dhidi yao yanayofanywa na makundi ya vijana wa CCM
waliowekwa katika makambi kadhaa kisiwani Unguja.
10. KWAMBA
linaitaka jumuiya ya kimataifa na hasa taasisi zinazosimamia haki za binadamu
na zinazopambana na makosa ya jinai kimataifa ikiwemo Mwendesha Mashtaka wa
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court – ICC)
kufanya uchunguzi wa kauli na matendo ya uhalifu, uvunjwaji mkubwa wa haki za
binadamu na ubaguzi ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wananchi wa Zanzibar na
kuchukua hatua dhidi ya watu walio nyuma ya maamuzi na utekelezaji wa matukio
hayo.
11. KWAMBA
linawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu na kuwa
watulivu licha ya machungu makubwa waliyoyapitia na wanayoendelea kuyapitia
tokea pale maamuzi yao yalipopinduliwa na CCM kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha.
Baraza Kuu
linatoa wito kwa Wazanzibari wote kuungana pamoja chini ya chama chao cha CUF
walichokipa ridhaa halali kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015
kutetea maamuzi yao waliyoyafanya kupitia sanduku la kura kwa njia za amani.
Baraza Kuu
linawasisitiza tena Wazanzibari kwamba waendelee kutunza amani ya nchi yetu na
kutambua kwamba kutunza amani si udhaifu bali ni jambo linaloipa nguvu jumuiya
ya kimataifa kufuatilia haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar.
12. Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa linawatahadharisha CCM na watawala wasiowajali na
kuwaheshimu wananchi kwamba zama za utawala wa mabavu usioheshimu Katiba na
Sheria za nchi hazina nafasi tena katika dunia ya leo. Baraza Kuu lina imani
kwamba HAKI ITASHINDA.
LIMETOLEWA
NA:
BARAZA KUU
LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC
UNITED FRONT
(CUF – Chama
Cha Wananchi)
DAR ES
SALAAM
28 JANUARI,
2016.
|
Thursday, January 28, 2016
BREAKING NEWS:-CUF Kutoshiriki Uchaguzi wa Marudio Zanzibar.
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment