KWA KIFUPI.
- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa za mateso ya mtoto huyo zilifikishwa Kituo cha Polisi wilayani Kilosa za saa za mchana jana, baada ya uongozi wa kijiji na kata kutoa taarifa na tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Wakati jamii
ikiwa bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na kusababisha
kifo chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika Kijiji cha Matongola,
Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa,Mkoani Morogoro baada ya kubainika mtoto wa miaka sita akiwa
amefichwa uvunguni mwa kitanda na kufanyiwa vitendo vya kikatili na Mama yake
mzazi.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema
kuwa taarifa za mateso ya mtoto huyo zilifikishwa Kituo cha Polisi wilayani
Kilosa ,saa za mchana juzi (Julai 11,2014), baada ya uongozi wa kijiji na kata kutoa
taarifa na tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Mama
aliyefanya ukatili huo anafahamika kwa jina la Sala Mazengo ambaye alimficha
ndani mtoto wake aliyefahamika kwa jina la Devota Malole na kumfanyia vitendo
vya kikatili ikiwa pamoja na kutompa chakula, wala kumfanyia usafi.
Baada ya
kufichuliwa kutoka alipofichwa, mtoto huyo alionekana kuwa dhaifu kiafya
kutokana na kukosa lishe pamoja na mazingira aliyokuwa akiishi kutoridhisha,
jambo ambalo ni kosa kisheria, pia ukiukwaji wa haki za watoto.
Inadaiwa kuwa
tangu mwka 2009, Sala amekuwa akimficha mtoto wake huyo ambaye sasa amelazwa
katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu.
Hata hivyo,
mwanamke huyo alipoulizwa alidai kuwa afya ya mtoto wake ilikuwa mbaya tangu
alipozaliwa kutokana na magonjwa ya mara kwa mara, pia hali ngumu ya maisha
ilichangia kudhoofisha afya ya mtoto huyo.
Alidai kuwa
ana watoto sita, pia alikiri kumlaza chini mtoto huyo kutokana na kuwa na
kitanda kimoja, ambacho hakiwatoshi watoto hao.
Aliongeza
kuwa hata chakula amekuwa akikipata kwa shida kutokana na kushindwa kufanya
kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda
Paulo alisema kuwa mwili wa mtoto huyo umedhoofu kutokana na kufichwa
ndani kwa muda mrefu na bado mwanamke huyo hajaeleza sababu za kufanya vitendo
vya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
“Siwezi
kutoa taarifa ya kidaktari, lakini kutokana na afya ya mtoto yule na mazingira
tuliyomkuta ni dhahiri alikuwa akipata mateso na kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi tunaufanya na kwamba taratibu za kumfikisha
mtuhumiwa huyo Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa zinaendelea,” alisema Kamanda
Paulo.
Alisema kuwa
mpaka sasa bado haijafahamika kama mtoto Davota ni mlemavu au la na kwamba
taarifa za afya ya mtoto huyo zitatolewa baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi
wa kina.






No comments:
Post a Comment