Mwanamuziki
nguli wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Maalim Gurumo aliyefahamika pia kama
kamanda na mashabiki wa muziki wa dansi, aliyeaga dunia Jumapili iliyopita
katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar, alikutana na mateso ya kwa saa 72 za
mwisho wake baada ya kulazwa akiwa taabani kwa siku tatu.
Mtoto wa
marehemu anayejulikana kwa jina la Abdalah aliliambia Uwazi kuwa siku
mauti yalipomfika baba yake katika wodi namba sita Jengo la Mwaisela,
alimtembelea na kumkuta akiwa katika hali nzuri na alipopewa chakula alikula,
akashiba lakini cha ajabu alisema hatakula tena.
Kijana huyo
alisema muda mfupi baadaye, hali ya baba yake ilibadilika, akaanza kupumua kwa
shida ndipo alipozidiwa na baadaye kukata roho.
Mzee Gurumo
alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu kwa muda mrefu na aliwahi kulazwa
katika hospitali hiyo ya Muhimbili.
Baadhi ya
watu waliomtembelea mzee Gurumo kwa nyakati tofauti akiwa hospitalini hapo ni
pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
ambaye alimuombea afya njema na akaruhusiwa kurudi nyumbani.
Kifo chake
kimeacha simanzi si tu kwa familia yake, bali kwa wadau wa muziki wa dansi
kwani alikuwa mwalimu na kiongozi wa wanamuziki wengi ambao sasa wanatamba.
Baada ya kustaafu muziki, Mzee aliwahi kupewa zawadi ya gari na msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ aina ya Toyota Funcargo.
Baada ya kustaafu muziki, Mzee aliwahi kupewa zawadi ya gari na msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ aina ya Toyota Funcargo.
Akizungumzia
msiba huo, Kiongozi wa Bendi ya Extra Bongo, Ally Choki alisema wamempoteza
mwalimu wa muziki asiyekuwa na choyo ya kuelimisha.
“Ni kama
tumepoteza tochi tukiwa kwenye msitu mnene usiku wa manane,” alisema.
Naye msemaji
wa Bendi ya Mlimani Park Ochestra (Sikinde Ngoma ya Ukae), Jimmy Chika
alipozungumza na Uwazi alisema mzee Gurumo aliwahi kuja kuwatembelea na kuimba
mwezi mmoja uliopita katika Ukumbi wa DDC, Kariakoo jijini Dar.
“Alikuja
kama mara tatu hivi ukumbini, naona alikuwa kama anatuaga kwa sababu alikuwa
mwanzilishi wa bendi na mbunifu wa mtindo wa Sikinde, aliubuni Septemba, 1978,”
alisema Chika.
Mzee Kassim Mapili, mwanamuziki wa mkongwe, kwa upande wake
alisema kifo cha Gurumo ni pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibika na akafafanua
kuwa ni mtu ambaye hakuwa mbinafsi.
Baadhi ya
wanamuziki ambao amefanya nao kazi kwa karibu ambao sasa watakuwa wanamlilia
mwalimu wao ni pamoja na Hassan Rehani Bitchuka, Said Mabela, Roman Mng’ande
‘Romario’ na wengine wengi.
Gurumo pia
ameacha simanzi katika miji mbalimbali nchini kwa kuwa amewahi kutembelea
kimuziki na alifanikiwa kujizolea mashabiki lukuki.
Hadi
Uwazi linakwenda mitamboni msiba ulikuwa nyumbani kwake Mabibo, Dar huku
taratibu za mazishi zikifanyika.
Marehemu
Gurumo aliyezaliwa mwaka 1940 ameacha mjane mmoja na watoto sita, watatu wa
kiume ambao ni Abdallah, Omar na Mwalimu na wa kike pia wakiwa watatu ambao ni
Mariam, ambaye ndiye mtoto mkubwa wa marehemu, Mwazani na Kibibi aliye wa
mwisho kuzaliwa.
Mungu
ailaze roho ya marehemu maali pema peponi. Amina.
Credit:- Gazeti la Uwazi/ GPL
Credit:- Gazeti la Uwazi/ GPL
No comments:
Post a Comment