Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye akionesha kitabu
cha maadili yanayotakiwa kufuatwa na wana CCM alipokuwa akizungumza katika
mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo februari 18,2014, kuhusu onyo walilopewa
makada wa CCM wanaodaiwa kutangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda kuwadia.
Makada hao waliohojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya chama hicho ni; Mawaziri
wakuu wastaafu, Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa
Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Januari Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, Wiliiam
Ngeleja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen
Wassira. Makada hao watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 12.
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI.
Kati ya tarehe 13/02/2014 na tarehe 18/02/2014 kumekuwa na mfululizo wa
vikao kadhaa vya Chama kitaifa vilivyoshughulikia suala la maadili ndani ya
Chama.
Vikao hivyo ni pamoja na Kamati Ndogo ya Udhibiti tarehe 13-14/02/2014, Tume ya
Udhibiti na Nidhamu 18/02/2014 na Kamati Kuu tarehe 18/02/2013.
Waliohojiwa katika mfululizo wa vikao hivi ni wafuatao:-
1. Ndg. Frederick Sumaye
2. Ndugu Edward Lowasa
3. Ndugu Bernard Membe
4. Ndugu Stephen Wassira
5. Ndugu January Makamba
6. Ndugu William Ngeleja
Baada ya kuwahoji ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na
hivyo kupendekeza adhabu.
Mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya
Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa
wahusika.
Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo:-
1. Walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla
ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari
2010, Ibara 6(7)(i).
2. Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na
baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Kosa hili
nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari
2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.
Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa
adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na
iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi.
Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za
CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:-
“Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa
kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za
kujirekebisha.”
Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua
kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika
kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za Chama.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka
kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais yanayovunja na kukiuka
maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI,
18/02/2014.
|
No comments:
Post a Comment