Taswira ya Mkutano wa 6 wa Ujirani Mwema baina ya Nchi ya Tanzania na Burundi uliofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera huku wito ukitolewa kwa Wataalamu wa kimataifa kutatua migogoro ya Kimipaka. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, September 02, 2013

Taswira ya Mkutano wa 6 wa Ujirani Mwema baina ya Nchi ya Tanzania na Burundi uliofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera huku wito ukitolewa kwa Wataalamu wa kimataifa kutatua migogoro ya Kimipaka.

Ni Taswira katika Viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera  ambapo (Septemba 02,2013)kulikuwa na tukio moja kubwa na la Kihistoria la Viongozi  wandamizi na Wataalam wa Kada mbalimbali  kutoka nchini Burundi na Tanzania  ambao wamekutana kwenye mkutano wa Sita wa Ujirani Mwema kujadili changamoto za kimipaka baina ya nchi hizo kupitia wananchi wanaoingiliana kimataifa  katika shughuli za uzalishaji mali.-(Picha na Shaaban Ndyamukama-Ngara).

Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Ngara mkoani Kagera nchini Tanzania ( OCD)  Bw.Abel Mtagwa katikati akiteta jambo na Afisa Uhamiaji wa Burundi kushoto pamoja na Mkuu wa  Ofisi ya Takukuru  wilaya ya Ngara Bw.Kiondo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Masawe kushoto akiwa na Wakuu wa Mikoa kutoka Nchini  Burundi nyuma yao ni Mkuu wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera nchini Tanzania Bw.Kostantine Kanyasu.



Mwenye miwani ni Mkuu wa Mkoa wa Chankuza Bw.Nilagira Berikimas wakibadilishana mawazo ambapo wamesema Tanzania haina mahusiano mabaya na Nchi ya Burundi na changanoto mbalimbali za kimahusiano ukiwemo ulinzi na usalama zitamalizwa kwa njia  za vikao  ili kulinda amani kwa watu wa mataifa hayo.

Mwenye kibagarashia Kichwani ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera nchini Tanzania Bw.Soud  Mkubila akiteta jambo na Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanal Fabian Masawe  na Mkuu wa Mkoa wa Chankuzo  nchini Burundi  Bw.Nilagira Berikimas.


Wajumbe wa kamati ya ardhi kutoka Tanzania na Burundi wakibadilishana mawazo njeya kikao chao wilayani Ngara mkoani Kagera.

Baadhi ya Waandishi wa habari wakiwa na wataalam kutoka Wizara ya ardhi na Mipaka ya nje  katika mkutano wa Sita wa Ujirani Mwema uliofanyika (Septemba 02,2013)katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya  ya Ngara mkoani Kagera.

Wakuu wa Mikoa mitano nchini Burundi na mwenzao  wa Mkoa wa Kagera Kanal Fabian Masawe pamoja na mkuu wa wilaya ya Ngara Bw.Kostantine Kanyasu wakiimba wimbo wa hamasa wa Maendeleo na Amani  mkoani Kagera katika mkutano wa Sita wa Ujirani Mwema uliofanyika (Septemba 02,2013)katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya  ya Ngara mkoani Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw.Fabian Masawe akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari Bw.Shaaban Ndyamukama.
Wataalamu wa masuala ya mipaka ya kimataifa kutoka Burundi wakiwa nje ya Ukumbi wa Halmashauri ya  Ngara baada ya kikao na wenzao wa Tanzania.
 

Viongozi  wandamizi kutoka nchini Burundi na Tanzania  wamekutana katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwenye mkutano wa sita wa ujirani mwema kujadili changamoto za kimipaka baina ya nchi hizo kwa wananchi wanaoingiliana kimataifa  katika shughuli za uzalishaji mali.

Mkuu wa mkoa wa kagera kanali mstaafu Fabiani Masawe akifungua mkutano huo  leo(September 02,2013)  amewataka wataalamu wa mipaka ya kimataifa kutoka mataifa hayo kufanya kila linalowezekana kuinyoosha mipaka ya nchi hizo jirani na kuondoa migogoro kwa wananchi walioko katika nchi hizo. 

Kanali Masawe amesema kuwa migogoro ya kuhamisha alama za kimataifa zinazotenganisha taifa moja na jingine imeanza kuibuka mwaka 1983 na mataifa hayo kuwa na mikutano ya mazungumzo  bila kupata suluhisho kwa wananchi wake .

Amesema wakulima na mataifa ya Tanzania na Burundi walioko mipakani wanalazimika kuanzisha uhasama na kuvunja mahusiano yao kwa kugombania mahali pa kulima na kulishia mifugo na migogoro hiyo kuwa mikubwa kasha kuingizwa kwenye vikao vya kimataifa .

 Mipaka hii imekuwa ya kurithi kutoka kwa wakoloni ambayo iliwekwa bila kushirikisha watu wa maeneo husika na waaasisi wa mataifa haya wameongoza bila migogoro lakini ilikuwa ni kutokana na uchache wa watu  kwenye mataifa yao”.Alisema Masawe.

Aidha alidai kuwa wataalamu wa nchi hizo hawana budi kukubaliana na kuweka alama ambazo kwa namna moja au nyingine imeondolewa na mabadiliko ya hali ya hewa kama mito na vijito ama kwa kukauka au kufurika na kuhama njia za awali.

Alisema kuna haja ya kutekeleza maazimio ya pamoja kwa vitendo katika nchi jirani  ili kuweka alama ambazo hazitafutika au kuondolewa na watu wenye nia ya kuingilia taifa jingine ambazo ni za kisasa katika mfumo wa digitali na si kuendelea na mfumo wa analojia ambao umepitwa na enzi. 

Katika hatua nyingine Kanali Masawe alisema kuwa mikutano ya kubaini mipaka kupitia Umoja wa Afrika ilikuwa itekelezeke hadi 2012kisha kushindwa  na sasa muda umeongezwa hadi 2017  hivyo mataifa hayo yatumie muda huo kupanga bajeti ya kuwezesha maazimio ya AU yaweze kufanikiwa. 

Awali katika kikao hicho  mkuu wa wilaya ya Ngara Costantine Kanyasu alisema kuwa migogoro ya kimipaka kati ya Tanzania na Burundi japo sio kubwa lakini wakazi wa kijiji cha Kasange Mugoma na Mukikomero wanaingiliana kwa shughuli za kilimo na kanza kuhitilafiana wakati wa mavuno.

Bw.Kanyasu alidai kuwa vigingi vya kimipaka vilivyopo maeneo hayo baadhi yake vimeng’olewa na wahalifu wanaodhani katika kusimikwa kwake kuna madini yalichimbiwa ardhini ma kuvifukua na kupasua kuona kilichomo ndani ya vigingi hivyo.

Alifafanua kuwa pamoja na wananchi wa wilaya hiyo na mikoa ya Muyinga pamoja na  Chankuzo nchini Burundi kuwa na mahusiano mema kuna haja ya alama za kimataifa kati ya taifa na jingine kutambulika kwa wananchi hao na kuishi kwa usalama na amani.

Hata hivyo Wakuu wa mikoa ya Muyinga ,Chankuzo Ruyigi na  Makamba  wamedai Tanzania haina mahusiano mabaya na Nchi ya Burundi na changanoto mbalimbali za kimahusiano ukiwemo ulinzi na usalama zitamalizwa kwa njia  za vikao  ili kulinda amani kwa watu wa mataifa hayo.

Kiongozi wa wakuu hao Nilagira Berikimas alisema mikutano na vikao vya mara kwa mara kwa kushirikisha wataalamu wa fani mbalimbali zikiwemo kamati za ulinzi na usalama za nchi hizo hakutakuwa tena na mtafaruku wa kimazingira kuhusu mahusiano yao.

Sote tuko ndani ya Afrika  na Jumuia ya afrika ya Mashariki hivyo la msingi nikuitana kuja Tanzania au Burundi na kufanya mazungumzo na maazimio ya pamoja kuyatekeleza kuanzia ngazi za vitongoji  .Alisema Berikimas.

Aliongeza kuwa siku za hivi karibuni miezi miwili iliyopita kulikuwa na vikao vya pamoja baina ya viongozi wa wilaya ya Ngara na mikoa ya Muyinga na Chankuzo kujadili mahusiano  katika usalama na  jinsi ya kukuza biashara kwa wananchi kuuziana na kubadilishana bidhaa.  

Wajumbe kutoka Tanzania  katika mkutano huo walikuwa ni  wataalamu wa mipaka ya kimataifa  kutoka wizara ya ardhi, wizara ya Nishati na Madini, wizara ya maji na mazingira,  ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya Rais pamoja na ofisi ya  waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.  

Picha/ Habari Na: Shaaban Ndyamukama 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad