CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) kimeingia katika mzozo mpya wa vikao vya chini kupinga
uamuzi wa vikao vya juu, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya chama hicho.
Mzozo
huo umehusisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Constancia Buhiye, na Katibu
wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambaye
kikatiba ndiye msemaji wa chama.
Baada
ya Nape juzi kusitisha uamuzi wa NEC Mkoa wa Kagera kufukuza madiwani wanane,
jana Buhiye aliita waandishi wa habari mjini Bukoba na kuwaeleza kuwa hatambui
kauli ya Nape.
Alisisitiza
kuwa hata kama Nape alitangaza kusitisha uamuzi wa mkoa kuwavua uanachama wa
CCM madiwani hao, na kuwataka waendelee na kazi zao hadi vikao vya juu
vitakapojadili suala lao na kutoa uamuzi, msimamo wa NEC Kagera ni kwamba
waliofukuzwa wamefukuzwa, si madiwani tena.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi, Nape alisema CCM Taifa imeagiza madiwani hao
wanane waendelee na kazi zao za udiwani kama kawaida, huku wakisubiri uamuzi wa
Kamati Kuu ambayo imeamua kuweka ajenda yao kwenye kikao hicho kitakachofanyika
Dodoma Agosti 23.
Nape
alifafanua kuwa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye
vyombo vya dola hasa wabunge na madiwani, uamuzi wa NEC mkoa si wa mwisho,
kwani unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu ndipo utekelezwe.
Hata
hivyo, Buhiye alisema kuwa chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa taratibu,
miiko, kanuni, katiba na miongozo, hivyo uamuzi uliotolewa na NEC mkoa juzi
ulikuwa halali kwa sababu ulitolewa kwenye kikao halali.
Alipoulizwa
kama haoni msimamo wake unapingana na wa chama makao makuu, Buhiye alidai kuwa
hakumsikia Nape akitoa kauli hiyo, na kwamba hawezi kuitoa.
Alisisitiza kuwa
hata kama ni kweli Nape alitoa kauli hiyo, msimamo ni kwamba madiwani
wameshafukuzwa.
Buhiye
alisisitiza kuwa hajapata barua ya Nape kumweleza uamuzi wa taifa na wala
hajamsikia kwa masikio yake kupitia kwenye vyombo vya habari akitengua uamuzi
wao.
“Kwa
mujibu wa ibara ya 14 ya katiba ya chama ni kuwafukuza uanachama wanaokihujumu
kwa namna yoyote na ibara ya 15 kuwavua uongozi ndani ya chama huku,” alisema.
Aliongeza
kuwa mkoa unayo haki ya kusimamisha mwanachama yeyote kwa kufuata muongozo wa
vikao kuanzia ngazi ya chini kwa wale walioteuliwa na NEC.
“Anayozungumza
Nape ni yake na mimi nazungumza kwa niaba ya kikao cha NEC mkoa wa Kagera,”
alitamba na kuongeza kuwa uamuzi wa mkoa hauwezi kutenguliwa na kikao chochote
kwa mujibu wa katiba ya chama hicho isipokuwa kutolewa ushauri na uongozi wa
juu.
Alisema
walitarajiwa kuifikisha taarifa ya uamuzi wao makao makuu ya chama jana
kutokana wao kuchelewa kuituma.
Uamuzi
wa kufukuza madiwani ulifikiwa katika kikao cha NEC mkoa kilichoketi Jumanne
jioni Agosti 14, lakini ulisitishwa siku moja baadaye kwa kigezo kuwa utaratibu
wa kuwafukuza ulikuwa umekiukwa.
Madiwani
hao wanatuhumiwa kukisaliti chama kwa uamuzi wao wa kuungana na wenzao wa
upinzani kusaini hati ya tuhuma za Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani,
wakitaka ang’olewe kutokana na kuiingiza halmashauri kwenye mikataba mitatu ya
kifisadi.
Miradi
hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka
Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu na wananchi
hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma
nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru
na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa
pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) bila kibali
cha Baraza la Madiwani.
Vile
vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh
milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo
pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297
zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya
mradi wa kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Nape atoa Msimamo.
![]() |
Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye. |
Alipotafutwa
kuzungumzia msimamo wa chama mkoa wa Kagera kupinga maamuzi ya taifa, Nape
alisema hili si suala la kubishana kwenye vyombo vya habari sasa.
“Nilichosema
mimi ndio utaratibu wa chama unaopaswa kufuatwa wala si utaratibu wa Nape.
Anayebisha anabishia katiba na kanuni za CCM hambishii Nape, na mimi ndiye
msemaji wa chama,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu uvumi ulionezwa mjini Bukoba kuwa Makamu Mwenyekiti wa sasa, Philip
Mangula, na mstaafu Pius Msekwa hawajapendezwa na uamuzi wake wa kubatilisha
maamuzi ya NEC Kagera, Nape alisema, “Mangula na Msekwa ni wazee, wao ndio
waliotunga kanuni na taratibu ambazo mimi nazitumia kuongoza, hawawezi kuzipinga
kanuni walizozitengeneza wao.”
Kuhusu
msimamo upi sasa unapaswa kufuatwa na madiwani hao, Nape alisema kuwa msemaji
wa chama ni yeye na kwamba maamuzi ya CCM Taifa yanapaswa yaheshimiwe.
Katika
hatua nyingine, madiwani hao nane walisema kuwa pamoja na makao makuu kutengua
maamuzi ya awali, uongozi wa mkoa juzi jioni uliwakabidhi barua za kuwafukuza
uanachama.
Chanzo
chetu kutoka ndani ya CCM zilidai kuwa mwenyekiti Buhiye amekuwa na visasi
dhidi ya uongozi wa chama makao makuu baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya
ujumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ambayo sasa inashikiliwa na Prof. Anna Tibaijuka.
Hivi
karibuni akiwa mjini Bukoba, Rais Jakaya Kikwete alijaribu kuingilia kati
mgogoro huo kwa kuwataka meya Amani na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis
Kagasheki, kumaliza tofauti zao ili miradi hiyo iendelee kutekelezwa.
Hata
hivyo, ushauri wake ulipuuzwa na madiwani hao pamoja na wenzao wa CHADEMA na
CUF wakisema tatizo si ugomvi kati ya wawili hao bali wanapinga ufisadi wa meya
wao kuingia mikataba ya miradi bila kuwashirikisha.
Chanzo:Tanzania
Daima.
No comments:
Post a Comment