Kuwaka moto uwanja wa Kenya :Mamlaka haijatoa Kauli kuhusu hasara ya mali pamoja na chanzo cha moto huo. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, August 07, 2013

Kuwaka moto uwanja wa Kenya :Mamlaka haijatoa Kauli kuhusu hasara ya mali pamoja na chanzo cha moto huo.

Hali ya taharuki imetawala katika kiwanja cha ndege cha Nairobi baada ya moto mkubwa kutokea na kusababisha ndege kadhaa kukwama. Moto huo ulianza tangu alfajiri (Agosti 07,2013) na haijajulikana chanzo chake ni nini.


Mpaka sasa mamlaka haijatoa kauli yoyote kuhusiana na hasara ya mali pamoja na chanzo cha moto huo.


Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imesema moto huo ulikuwa "mkubwa sana" na kwamba chanzo chake bado hakijafahamika ambapo  msemaji wa polisi nchini Kenya, David Kimaiyo, akitaka kuwepo kwa utulivu.

Waziri wa Usafiri na Miundombinu, Michael Kamau, anaongoza upelelezi huo. Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri kadhaa wamekuwapo kwenye uwanja huo wa ndege tangu mapema asubuhi ya leo (Jumatano, 7 Agosti) , mara tu baada ya taarifa za moto kusambaa.
Baadhi ya abiria na watu waliokuwa wakitarajia kusafiri  kwenda nje ya nchi, walikwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya ndege za kutokea Kenya kusimamisha huduma kutokana na moto uliozuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Uwanja huo uliopo Nairobi ambao hutumiwa na ndege nyingi za kimataifa kuunganisha safari zake katika nchi mbalimbali, ulisimamisha kwa dharura safari za ndege zikiwamo za Shirika la Ndege ya Kenya (KQ) kwa siku nzima ya jana.

Taarifa zilisema ndege zote zilizokuwa zitue uwanja wa Jomo Kenyatta kwa siku ya jana hazikuruhusiwa, na zile zilizokuwa tayari angani zilielekezwa kutua kwenye viwanja vya ama Mombasa, Kenya au Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) uliopo mkoani Kilimanjaro, Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, ambapo taarifa zingine zilisema kuwa moto huo ulianza kuwaka saa 11 alfajiri na kusababisha usumbufu kwa abiria na wale waliokuwa na shughuli zao kwenye uwanja huo.

Hata hivyo, vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vilifanikiwa kuuzima. 

Ilielezwa kuwa moto huo ulianzia katika chumba cha Idara ya Uhamiaji kinachotumiwa na wasafiri wanaowasili.

Tukio hilo limemfanya Rais wa Kenya, Bw.Uhuru Kenyatta kufika uwanjani hapo kujionea hali ilivyo akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw.Joseph Ole Lenku na Waziri wa Usafirishaji na Miundombinu,Bw. Michael Kamau.

Kutokana na kufungwa kwa uwanja huo, marubani wamekuwa wakielekezwa kutumia viwanja vingine, ukiwamo Mombasa, Eldoret na Dar es Salaam (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, Uganda.

Maafisa wa serikali wanasema sehemu ya paa la Kitengo Namba 1 cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta lilianguka kutokana na moto huo, na kuwapa tabu sana wafanyakazi wa kikosi cha uokozi kupambana na moto huo ulioanza mapema asubuhi.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Kenya, Titus Naikuni, mewahakikishia wasafiri kwamba ajali hii ya moto haijaondosha usalama wao.


Moto huu umetokea katika siku ambayo Kenya inakumbuka mwaka wa 15 tangu mashambulizi ya mabomu kwenye ubalozi wa Marekani jijini Nairobi.

Mashambulizi kama hayo yalifanyika pia siku na muda huo huo kwenye ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambapo matukio hayo mawili yaligharimu maisha ya watu 220.

Hadi sasa hakujawa na taarifa zozote za kuihusisha ajali hii ya moto na mashambulizi ya kigaidi.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad