Kuna wakati
ambapo, wanawake wanajikuta wakikabiliwa na swali la, Je, mwanaume huyu
ananipenda kweli?
Hii hutokea pale anapokutana na mwanaume ambaye, huenda
amevutiwa naye. Pengine mwanaume naye anaweza kuonesha kuvutiwa na mwanamke
huyo.
Kwa hiyo,
mwanamke hujiuliza kama akubali ombi la mwanaume huyo na kukubali kuzungumza
naye au kuanzisha naye uhusiano, kama mwanaume atakuwa amezungumza naye kuhusu
jambo hilo.
Ni kweli kwamba, kuna ugumu kwa mwanamke kujua hasa ni kwa namna
gani anaweza kujua kwamba, huyo mwanaume amempenda kweli au hapana.
Kuna vitu
vingi ambavyo vinaweza kuwa ni dalili ya kumpenda mwanamke, lakini wakati huo
huo vinaweza visiwe.
1. Hebu
tuchukulie kwamba, mwanaume ameonesha kuwa na tabia tunazoziita nzuri. Labda
amekumbuka kirahisi jina la mwanamke, ameonesha kuwa msikilizaji mzuri,
ameonesha kuwa anajali kuhusu kinachosemwa na mwanamke, na amekuwa anamuuliza
maswali kwa dhati na utulivu.
Hapa mwanamke anaweza kuamini kwamba, huyu
mwanaume anampenda. Lakini ukweli huenda ukawa ni kinyume chake.
Inawezekana
huyo mwanaume ni muungwana tu, na anaonesha tabia hizo kutokana na uungwana
wake na siyo kutokana na kumpenda kimapenzi mwanamke.
2. Kuna watu
ambao wana upendo, wamekomaa kihisia na wanajua kuhusiana vizuri na watu.
Hii
haina maana kwamba, kumwonesha mtu tabia hizo, kuna maana ya kumpenda au
kumpenda sana mwanamke.
Dalili hizi ni nzuri na inawezekana zikawa zinaonesha
mwanaume kumpenda mwanamke, lakini mwanamke asilichukulie jambo hilo kwa namna
hiyo.
3. Mwanaume
anaweza kuonesha kuwa na udadisi kuhusu mwanamke kwa maana kwamba, kutaka kujua
mambo yake, kumfuatilia au kuulizauliza kuhusu habari za mwanamke.
Hii haina
maana kwamba mwanaume amempenda kimapenzi. Inawezekana mwanaume akawa amevutiwa
kimapenzi na mwanamke ndiyo maana akaonesha tabia hizo, lakini siyo lazima iwe
hivyo.
Kumbuka kwamba, mwanaume anaweza kuvutiwa na mazungumzo ya mwanamke,
akavutiwa hata na namna alivyo usoni, hivyo akapenda kuzungumza naye lakini
siyo kwa sababu anampenda.
4. Kuna
wanaume ambao wana wake au wapenzi, lakini wanajisikia vizuri kusikiliza
wanawake wengine au kujua tu habari za wanawake wengine, bila kuwa na haja ya
kuanzisha uhusiano nao.
Mwanaume anapompa mwanamke ‘ofa’ hasa ya chakula cha
mchana au usiku, ni dalili ya wazi ya kuvutiwa naye. Hapa kuna uhakika mkubwa
zaidi, labda tu kama mazungumzo yanayotajwa kufanywa wakati huo wa chakula
yanafahamika, na ni ya shughuli maalum.
Kwa hiyo ‘ofa’ ya chakula ni dalili
nzuri na yenye uhakika. Lakini kuna jambo ambalo ni muhimu kwa mwanamke
kulifahamu katika hali kama hii.
Kuna wakati mwanaume kumpa ‘ofa’ mwanamke kwa
chakula cha mchana au jioni, kunaweza kusiwe na maana ya moja kwa moja kwamba,
uhusiano utaundwa. Inawezekana katika kutoka outing huko, mwanaume akaghairi.
Kwa wengine huchukua muda hadi kuamua kuhusu kuunda uhusiano au hapana.
5. Hata
mwanaume kuamua kumpeleka mwanamke kwa familia yao na kumtambulisha kama rafiki
yake, ni hatua yenye kuonesha kwamba, mwanaume ameamua kumpenda mwanamke huyo.
Lakini wakati mwingine hii inaweza ikawa ni janja yake kutaka tu kumthibitishia
mwanamke ili amhadae vizuri, na wala hakuna maana ya uhusiano wa kudumu.
6.
Kuzungumza kwa pamoja kuhusu masuala ya baadaye ya kiuhusiano, kama vile, idadi
ya watoto na mambo mengine ambayo mara nyingi huzungumzwa na watu ambao tayari
wako kwenye uhusiano ni dalili ya mwanaume kuvutiwa mwanamke.
Lakini tatizo la
jambo hili ni kwamba, kuzungumza masuala ya baadaye inaweza kuwa ni njia ya
mwanaume kutaka kujisikia au kujua jinsi inavyokuwa katika mambo hayo.
Inaweza
kuwa pia ni njia yake ya kutaka kupima wanawake wanavyosema kuhusu masuala
hayo. Lakini inaweza ikawa mwanaume huyo anatafuta kujua misimamo ya mwanamke
huyo ili hatimaye afanye uamuzi. Kwa hiyo, bado haioneshi kuwa amevutiwa na
kuamua tayari.
Mara nyingi
wanawake hudanganywa na dalili fulani zinazooneshwa na wanaume wakati
wanapoanza kuzoeana nao. Dalili hizi huwafanya kuamini kwamba, wanaume hao
wamewapenda tayari, wakati siyo kweli.
Kwa kuangalia baadhi ya dalili hizo kama
nilivyozitaja, mwanamke anaweza kuwa makini wakati anapoanzisha uhusiano, ili
asikurupuke na kujikuta amedanganyika. Ni kweli, kuna wakati ni dalili zinasema
kweli, lakini kuna wakai zinadanganya kuhusu kupenda au kupendwa.
No comments:
Post a Comment