Waimbaji wa
bendi ya Msondo ngoma wakitoa burudani wakati walipokuwa wakitumbuiza katika
ukumbi wa Max Bar Ilala Bungoni kutoka kushoto ni Muhidini Gulumo,Hassani Moshi
na Shabani Dede.
|
NGULI wa
muziki wa dansi nchini na kiongozi wa Msondo Ngoma Music Band, Muhidin Gurumo
‘Kamanda’ (73), ametangaza rasmi kustaafu baada ya kuitumikia fani hiyo kwa
miaka 53.
Kamanda
Gurumo aliyabainisha hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam jana, na
kwamba anaondoka katika fani akiwa hana kitu.
“ Leo
nimekuja kuwaaga rasmi wanamuziki na wapenda muziki na waliokuwa mashabiki
wangu kwa ujumla, sitaki tena muziki, ila ikumbukwe kwamba, muziki ni asili
yangu, ila sasa nimeamua kustaafu kwa moyo mmoja, hivyo naahidi kuwa
nitawasaidia wanamuziki wanaobaki kwa uhuru na moyo mmoja,” alisema Gurumo.
Gurumo
alisema anastaafu akiwa hana kitu cha maana katika tasnia ya muziki wa dansi, licha
ya kuutumikia na kufanya kazi kwa moyo wake wote kwa miaka 53.
“Nilianza
kuimba nikiwa kijana wa umri wa miaka 20 mwaka 1960 na tangu hapo sikuwahi
kubadili kazi, lakini sasa nastaafu ilhali nikiwa sina hata baiskeli,” alisema
Gurumo.
Wosia wake
kwa wanamuziki wanaobaki, anawaasa wapige muziki wa nyumbani, hasa waliokuwa
wakipiga bendi ya Msondo.
“Wapige
muziki ambao tulikuwa tunapiga sisi zamani, tofauti na hivi sasa, ambapo
wanamuziki na vijana wengi wanakimbilia katika muziki wa Bongo Fleva, ambao ni
muziki unaokwenda na wakati, lakini ni wa kupita,” alisema.
Aliongeza
kuwa kustaafu kwake hakuzuii kutoa ushauri au kufundisha wanamuziki na wapiga
ala, kwani ana kipaji cha kumfundisha mpigaji wa chombo chochote kwa kutumia
mdomo wake.
Kadhalika, Gurumo
anasema katika nyimbo alizowahi kuimba, wimbo anaoupenda ni ‘Usimchezee Chatu’,
ambao aliuimba kipande kidogo mbele ya waandishi wa habari na katika wanamuziki
wa Bongo Fleva, anampenda, Nasib Abdul ‘Diamond’.
Wakati huo
huo, Mratibu mkongwe nchini wa matamasha mbalimbali na mwanzilishi wa ‘viota’
na kumbi nyingi za burudani jijini Dar es Salaam, Juma Mbizo, anatajwa na
Gurumo kuwa ndiye atakuwa mratibu katika tamasha maalumu litakaloandaliwa la
kumuaga.
Katika
kamati hiyo pia wamo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The African Stars
Entertainment (Aset), Asha Baraka, mdau wa burudani, Said Mdoe, Richardson
Sakalla na Mkurugenzi wa bendi ya The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’, Waziri Ally.
“Hii kamati
imeundwa ili iweze kumsaidia katika kumuandalia tamasha maalumu, hivyo ipo siku
tutaweka wazi tumeandaa kumfanyia nini mkongwe huyu wa dansi, kadhalika siku
hiyo ya tamasha lake, ndipo atakapoimba kwa mara ya mwisho na kuanzia leo
hatapanda katika jukwaa lolote kuimba,” alisema Mbizo.
Mbizo
aliongeza kuwa, Gurumo amepata ridhaa kutoka kwa wanamuziki wenzake wote kabla
ya kufikia uamuzi huo, na kwa kuwa ameimba kwa miaka mingi, sasa ni wakati wake
wa kupumzika.
No comments:
Post a Comment