![]() |
Dk. Emmanuel Nchimbi. |
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari
wakati alipokuwa akitoa taarifa ya Uchunguzi wa Matukio yaliyolalamikiwa dhidi
ya askari Polisi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma.
Baadhi ya
matukio hayo ni pamoja na tukio la gari la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)
kutumika katika uhalifu (ubebaji bangi) katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,
Polisi Mkoa wa Morogoro kutumia fuvu la kichwa cha binadamu kumbambikizia
mfanyabiashara kwa lengo la kupata fedha na Mauaji ya mfanyabiashara wa Wilaya
ya Kasulu yaliyofanywa na Askari wawili wa Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo
ameitoa katika Ukumbi wa Mikutano wa wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo(Agosti
22,2013).
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka Maafisa wanne wa
Jeshi la Polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja ambaye atafunguliwa mashtaka
ya kijeshi kutokana na kukiuka maadili na taratibu za jeshi hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri Nchimbi amesema hatua
hiyo ni katika kuendeleza vita ya kuhakikisha kuwa jeshi la polisi linakuwa na
nidhamu, linatekeleza wajibu wake wa kutenda haki na kuwalinda raia na mali
zao.
Alisema
amewachukulia hatua Maafisa hao baada ya kuridhia maoni ya kamati aliyoiunda
kufanya uchunguzi wa matukio yaliyolalamikiwa dhidi ya askari polisi katika
mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma kati ya Desemba 2012 na Mei,
2013.
Waziri
Nchimbi aliwataja waliovuliwa madaraka kuwa ni Mkuu wa kikosi cha kutuliza
ghasia mkoani Arusha Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro, Mkuu wa Upelelezi wilaya
ya Mvomero mkoani Morogoro Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi
cha Dumila Inspekta Juma Mpamba na mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kasulu ASP
Daniel Bendarugaho na kumsimamisha kazi Inspekta Isaack Manoni.
Alifafanua
kuwa Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro alivuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia
kikamilifu askari na maafisa walio chini yake ambao walikamatwa wakisafirisha
bangi yenye uzito wa kilogramu 540 kwa kutumia gari la polisi.
Alisema
askari hao wawili waliokamatwa wakisafirisha bangi, walikuwa wakifanya kazi
kwenye kituo cha Ngarananyuki na baada ya kukiri kosa walifukuzwa kazi mwezi
Mei mwaka huu.
Alisema kwa
upande wa Inspekta Jamal Ramadhan amevuliwa madaraka yake kwa kutochukua hatua
stahiki baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara wa Mvomero Samson Mwita
kubambikiwa fuvu la kichwa cha binadamu na askari polisi watatu wakishirikiana
na matapeli wawili.
“Katika
tukio hilo Inspekta Isaack Manoni amesimamishwa kazi na atashtakiwa kijeshi
kutokana na tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa, Cpl. Edward aliyekuwa dereva wa
gari la Polisi lililokamatwa na bangi kitendo ambacho kimelifedhehesha jeshi la
polisi” alisema Waziri Nchimbi.
Alibainisha
kuwa Inspekta Juma Mpamba amevuliwa madaraka hayo kwa kuonesha udhaifu katika
utendaji wake wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari walio chini yake
kitendo kilichosababisha askari kujipangia kazi nje ya utaratibu na
kumbambikiza mfanyabiasha huyo kesi kwa lengo la kujinufaisha kinyume na
maadili ya kazi. Aliongeza kuwa askari waliohusika na tukio hilo wamefukuzwa
kazi na kushtakiwa.
Waziri
Nchimbi alisema ASP Daniel Bendarugaho amevuliwa madaraka kwa kutokuwa makini
katika kufanya na kusimamia upelelezi wa kesi ya mauaji ya marehemu Gasper
Mussa Sigwavumba aliyeuawa baada ya kupigwa na askari polisi wawili Desemba
mwaka jana.
Alisema
upelelezi mbovu uliofanywa chini ya usimamizi wa Mkuu huyo wa upelelezi
ulisababisha kesi hiyo kuondolewa mahakamani. Aliongeza kuwa upelelezi wa kesi
hiyo utaanza upya ili haki itendeke.
No comments:
Post a Comment