![]() |
Taifa Stars. |
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa
kuiwezesha timu ya taifa, Taifa Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba
Watanzania kuiombea timu ili ifanye vizuri katika mechi yake ya kesho (Juni 8
mwaka huu) dhidi ya Morocco mjini Marrakech.
Stars,
ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake la mashindano ya awali ya
Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast kwa tofauti ya pointi moja, inacheza
na Morocco katika mechi ya nne itakayofanyika Marrakech baada ya kuibuka na
ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam mwezi
Machi.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo(Jini 07,2013), Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema
kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa
Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini
Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.
“Katika kipindi chote hiki hatujawahi kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF.
“Lakini katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri; kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata kuzilipia ada ya kucheza mechi (appearance fee).
“Posho za wachezaji zimepanda kwa karibu mara mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”
“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee timu na tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia kwa kuwa vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.
Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.
Katika mkutano huo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda Morocco kuishangilia timu.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine zilitarajiwa kusafirishwa jana(Juni 06,2013).
Aidha Taifa
Stars inatupa karata yake ya pili ugenini kwenye mechi za mchujo za Kombe la
Dunia kwa kesho (Juni 8 mwaka huu) kuikabili Morocco (Lions of the Atlas)
kwenye Uwanja wa Grand Stade hapa Marrakech, Morocco.
Stars
iliifunga Morocco mabao 3-1 zilipokutana Machi 24 Mwaka huu jijini Dar es
Salaa. Lakini zilipokutana hapa Marrakech mara ya mwisho mwaka 2011, Morocco
iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Taifa Stars Ilipoteza
mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Ivory Coast mwaka jana, na kushinda mbili
mfululizo nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco.
Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 3 usiku
kwa saa za Morocco ni ya pili kwa Stars katika uwanja huo ambapo mwaka juzi
ilifungwa mabao 3-1.
No comments:
Post a Comment