Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO) limekana kuwepo mgawo wa umeme kwa sasa huku likikiri kuwa hali ya upatikanaji wa nishati hiyo iko katika dharura na haijarejea katika hali ya kawaida kama inavyotakiwa.
Ufafanuzi
huu unakuja baada ya gazeti hili kuripoti hali tete ya kifedha inayolikabili
shirika hili na hivyo kutishia taifa kuingia gizani wakati wowote.
Hata hivyo
TANESCO na serikali kupitia kwa Wizara ya Nishati na Madini wamekuwa kimya kwa
muda pasipo kuzungumzia mgawo wa umeme ambao umekuwepo kwa wiki takriban mbili
katika maeneo mengi nchini.
Akizungumza
jana makao makuu ya shirika hilo Ubungo, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi
Mkuu, Felchesmi Mramba, alisema kuwa hakuna mgawo wa umeme kwa sasa na kwamba
ikitokea serikali ingetangaza.
Pamoja na
kukanusha kuwepo kwa mgawo, Mramba alisema ukweli ni kwamba bado nchi iko
katika hali ya dharura na hali ya umeme haijarejea katika hali yake ya kawaida
kiasi cha kuondoka katika hali ya dharura.
“Ushahidi wa
kwamba bado tuko katika hali ya dharura ni kwamba bado mitambo ya dharura
tuliyokodi kupambana na hali ya umeme inaendelea kuhitajika lakini pia mabwawa
hayana maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya umeme bila kuhitaji mitambo ya
matufa,” alisema.
Aliongeza
kuwa vilevile miundombinu ya gesi haiwapi gesi ya kutosha kuwasha mitambo yote
ya gesi ya megawati 501.
Mramba
alibainisha kuwa tangu Julai mwaka 2012 hadi Februari 2013, serikali imetumia
jumla ya sh bilioni 231.2 kama ruzuku kwa TANESCO kwa ajili ya kununua mafuta
ya mitambo.
“TANESCO kutoka
kwenye mapato yake imetumia jumla ya sh bilioni 423.3 katika kipindi hicho
kununulia mafuta, hivyo fedha yote iliyotumika kununulia mafuta ndani ya
kipindi hicho ni sh bilioni 654.5,” alisema.
Mramba
aliongeza kuwa mitambo ya dharura inahitaji fedha nyingi kuiendesha
kulinganisha na bei halisi ya kuuza umeme huo. Akitolea mfano alisema kuwa ili
kuzalisha zinahitajika megawati 365 kwa mafuta (Dizeli-lita 1,368,00, HFO-LITA
500,000 na Jet A1-Lita 518,000 kwa siku.
Alisema kuwa
jumla ya sh bilioni 5.4 zinahitajika kila siku au sawa na sh bilioni 162 kwa
mwezi na kwamba mapato yanayotokana na kuuza asilimia 100 ya umeme wote
unaozalishwa ni sh bilioni kwa siku sawa na takriban sh bilioni 70.2 kwa mwezi
baada ya kuondoa kodi na tozo mbalimbali.
“Hata kama
TANESCO ingeamua isilipe mishahara wala isifanye matengenezo ya mitambo,
isinunue vifaa vya kuunganishia wateja, au isiingie gharama nyingine zozote,
bado ingepata hasara ya karibu sh bilioni 90 kila mwezi,” alisema.
Mramba
aliongeza kuwa kwa sababu kuna matumizi mengine muhimu ya kiuendeshaji, TANESCO
inajikuta ikipata hasara kubwa zaidi kwa mwezi.
Kuhusu deni
la Songas, mkurugenzi huyo alikiri kuwa ni kweli kampuni hiyo inaidai TANESCO
na akasisitiza kuwa mkataba kati ya Songas na TANESCO unaruhusu hali hiyo.
Hata hivyo,
kauli hiyo inatofautiana na kauli ya Naibu Waziri wa Nishari na Madini, George
Simbachawene, aliyesema jana asubuhi kuwa wanaoshinikiza kuwa kuna deni kati ya
Songas na TANESCO ni madalali tu.
Chanzo:Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment