Taifa Stars yawaramba Wakenya, Harambee Stars bao 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, November 14, 2012

Taifa Stars yawaramba Wakenya, Harambee Stars bao 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imewatandika wenzao wa  Kenya, Harambee Stars bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza jioni hii katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa ulio katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).




Hadi mapumziko, Taifa Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0  lililofungwa  na  beki Aggrey Morris katika dakika ya nne, baada ya kupanda kusaidia mashambulizi.


Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa anayetambuliwa na FIFA, Oden Mbaga, Harambee Stars, walio chini ya Kocha kutoka Ufaransa, Henri Michel  walitawala dakika 10 za mwanzo,kwa kumchezesha Staa wao anaecheza Klabu ya Ufaransa ya Auxerre, Dennis Oliech na Taifa Stars, chini ya Kocha kutoka Denmark, Kim Poulsen, walimchezesha Staa wa TP Mazembe ya Congo DR, Mbwana Samatta.



Baada ya mchezo huo, kocha wa Harambee, Mfaransa Michel alionyesha kukerwa na matokeo hayo na kusema timu yake haikucheza vizuri, wakati Polusen, amefurahia ushindi huo akisema timu yake haijacheza kwa miezi miwili na baada ya siku mbili za mazoezi wameifunga Kenya.



Katika hatua Nyingine  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko kwa kiingilio cha juu cha mechi ya raundi ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville itakayochezwa Jumapili (Novemba 18 mwaka huu).


Awali kiingilio cha juu katika mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni kilikuwa sh. 5,000. Lakini kwa lengo la kuwafanya wadau wa kiingilio hicho kuchangia gharama za mechi hiyo sasa kutakuwa na viingilio vitatu tofauti katika viti vya VIP.


Kwa VIP A ambayo ina viti 748 kiingilio kitakuwa sh. 10,000, VIP B inayochukua watazamaji 4,160 kiingilio ni sh. 5,000 wakati VIP C yenye viti 4,060 kiingilio ni sh. 2,000. Kwa sehemu nyingine (viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu) ambavyo jumla yake ni 48,590 kiingilio kitabaki kuwa sh. 1,000.


Timu ya Congo Brazzaville kwa taarifa tulizopata awali kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Congo (FCF) ilikuwa iwasili jana (Novemba 13 mwaka huu) usiku. Lakini timu hiyo haikutokea na sasa tunatarajia itawasili leo (Novemba 14 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines. Congo itafikia Sapphire Court Hotel.


Wakati huo huo, Kamati ya Serengeti Boys itakutana na waandishi wa habari kesho (Novemba 15 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika kuanzia saa 5 asubuhi hoteli ya JB Belmont, ukumbi wa Ngorongoro.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad