![]() |
|
|
Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imefadhaishwa
na msiba wa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda Mhashamu Pascal
William Kikoti ambao ulitokea kwa ghafla sana.
Waziri Mkuu
ametoa salaam hizo leo mchana (Jumamosi, Septemba Mosi, 2012) kwenye ibada ya
mazishi ya Askofu iliyofanyika kwenye Kanisa la Mt. Maria Imakulata mjini
Mpanda.
Mhashamu
Askofu Kikoti alifariki dunia Agosti 28, mwaka huu katika Hospitali ya Bugando,
jijini Mwanza amezikwa kwenye kanisa hilo ambalo ndiyo makao makuu ya Jimbo
Katoliki Mpanda.
Waziri Mkuu
alisema: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete na viongozi wote wa Serikali kwa jumla, tumefadhaishwa sana na
msiba huu mkubwa, tena uliotokea kwa ghafla. Lakini kwa kuwa haya ni mapenzi
yake Mungu ambaye ndiye Muumba wetu sote tumelazimika kuipokea taarifa hii kwa
majonzi makubwa.”
Alisema yeye
binafsi alifarijika sana na uongozi wake, maono yake na shauku yake ya kutoa
huduma za kiroho na za kijamii kwa jumla. Alisema mchango wake umegusa jamii
nzima na siyo tu katika kutoa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii
zilizolenga kuleta maendeleo kwa wananchi katika Jimbo la Mpanda na nchini
kote.
“Mhashamu
Askofu Kikoti, ametutoka akiwa na umri mdogo sana wa kichungaji wa miaka 55,
baada ya kulitumikia jimbo hili kwa miaka 11. Kabla ya kifo chake alikuwa na
malengo mengi mazuri yakiwemo ya kufungua Seminari Ndogo ya Jimbo, kujenga
Kituo cha Kichungaji na Kijamii na kupanua Shule ya Sekondari ya Mtakatifu
Maria ya hapa Mpanda. Hivyo basi ni dhahiri kwamba kifo hiki ni pigo kubwa siyo
kwangu, au kwa waumini wa Kanisa Katoliki, au Wanampanda tu, bali wananchi wote
nchini kwa jumla,” alisema.
Mapema
akitoa salaam za Baba Mtakatifu katika ibada hiyo ya mazishi, Balozi wa Baba
Mtakatifu nchini Tanzania, Mhashamu Askofu Francisco Montecillo Padilla alisema
hayati Baba Askofu Kikoti hatasahaulika kwa mema aliyoyatenda Iringa akiwa
Padri na hapa Mpanda akiwa Askofu.
“Nilimfahamu
Askofu Kikoti Februari, mwaka huu mara baada ya kuanza kazi hapa nchini…
alikuwa ni mtu wa maneno machache lakini wa vitendo zaidi. Tunashukuru kwa
kuijenga Dayosisi hii mpaka sasa, kuwajali watu wake na zaidi ya yote
kuwapenda,” alisema.
Aliwasihi
waumini wa Jimbo Katoliki la Mpanda kuendelea kuwa na umoja hasa katika kipindi
hiki cha majonzi.
Ibada hiyo
iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo, ilihudhuriwa na Maaskofu 28 kutoka majimbo mbalimbali ya
Tanzania isipokuwa Askofu Renatus Msonganzila wa Musoma na Askofu Aloycius
Balina wa Shinyanga ambao walitajwa kuwa ni wagonjwa.
Maaskofu wa Mbulu na Moshi waliwakilishwa na
wasaidizi wao.
Wakati
huohuo, katika ibada hiyo ya mazishi, Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki
la Sumbawanga alitangazwa rasmi kuwa ameteuliwa na Baba Mtakatifu Benedict wa
16 kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Mpanda hadi atakapotangazwa
Askofu mwingine.
Uteuzi wake ulianza
(Ijumaa, Agosti 31, 2012).
Askofu Dk
Paschal William Kikoti (55), amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa shinikizo
la damu ambalo lilipanda kufikia 240 hadi 260, hali iliyomsababishia kifo
katika Hospitali ya Bugando, Mwanza.
Historia
yake.
Askofu
Kikoti alizaliwa Machi 3, 1957 huko Ihimbo, Parokia ya Nyabula, Jimbo Katoliki
la Iringa.
Alipata
elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Iringa, kisha elimu ya sekondari katika
Seminari ndogo ya Mafinga na mafunzo ya falsafa katika Seminari ya Peramiho,
Songea pamoja na Seminari Kuu ya Ntungamo, Bukoba.
Kwa upande
wa theolojia, alisoma Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora na mwaka 1988 alipata
daraja la upadri.
Baada ya
upadrisho wake, alifanya kazi jimboni Iringa na kati ya mwaka 1989- 1990
alikwenda masomoni Rome, Italia ambako alisomea Historia ya Mababu wa Kanisa na
Theolojia na kupata Udaktari wa Falsafa (PhD).
Mwaka
1997alirudi nchini na kufundisha katika Seminari ya Peramiho na Novemba 4,
2004, aliteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Mpanda na
alisimikwa rasmi Januari 14, 2001 hadi umati ulipomfika.
Pia, alikuwa
Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi ya TEC tangu mwaka 2009 akisaidiwa na Katibu
Mtendaji, Padri Raphael Madinda.
Napendwa
kutoa pole kwa kanisa katoliki Tanzania ,Mwadhama kadinali, maaskofu na mapadri
pamoja na Wana Katavi kwa kuondokewa na mwenzetu.MUNGU AIPE ROHO YA
MAREHEMU PUMZIKO LA MILELE’’Amen.








No comments:
Post a Comment