|
Leo, March 27, 2018, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) Mussa Assad amekabidhi Ripoti ya Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa Rais John Magufuli.
Kutokana na
ripoti hiyo Rais Magufuli
amemuagiza Waziri wa TAMISEMI Selemani
Jafo kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wawili wa Halmashauri za Kigoma Ujiji na Pangani kutokana na kuwa na hati chafu za hesabu hizo katika
matokeo ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka
2016/2017, ambapo muda mfupi uliopita Waziri Jafo ametangaza rasmi
kuwasimamisha kazi watendaji hao.
Ripoti hiyo
iliyowasilishwa leo Machi 27, 2018 inaonyesha halmashauri 166 kupata hati
safi, 16 hati zenye shaka na halmashauri tatu kupata hati chafu.
Halmashauri
zilizopata hati chafu ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri
ya Kigoma na Pangani.
Waziri Jafo amesema baada ya kuwasimamisha, amemwagiza katibu mkuu
wa wizara hiyo kuunda timu ya watalaamu kuchunguza hati hizo na kutoa matokeo
ndani ya wiki tatu.
Amesema Wakurugenzi waliohusika katika hati chafu ni Daud Mlahagwa
(Pangani), aliyekuwa Mkurugenzi wa Kigoma Ujiji, Judethadeus Mboya ambaye
amestaafu kwa sasa.
“Amestaafu lakini ameacha mambo yakiwa hayako sawa, wakati akiwa ‘account
officer’ mambo yalikwenda kombo na halmashauri hiyo ilipata hati chafu kwa
miaka mitatu mfululizo,” amesema.
Mwingine ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma, Hanji Godigodi.
“Wakurugenzi
hawa waliosababisha hati chafu nawasimamisha kazi kuanzia leo Machi 27, 2018
hadi hapo uchunguzi wa utendaji wao utakapokamilika, hawa wawili nawasimamisha
kazi, kutokana na hili namwagiza katibu Mkuu wa Tamisemi kuunda timu ya
watalaamu kwenda kuchunguza utendaji kazi wa wakurugenzi hao na kunipatia
taarifa ndani ya wiki tatu,”amesema.
Amesema
taarifa itakayopatikana itabainisha kiwango cha uchafu huo na Serikali
itachukua hatua nyingine za kisheria kadri uchunguzi utakavyoelekeza.
Pia,
amewataka wakurugenzi katika halmashauri zilizofanya vizuri katika ukaguzi huo,
waendelee kutekeleza na majukumu yao na kutoa majibu ya hoja zote
zilizobainishwa na ripoti ya CAG.
Amesema
Serikali imeanza kufanya vizuri katika ukaguzi huo baada ya kufikia asilimia 90
na matumaini yaliyopo ni kuondokana na taarifa ya hati chafu ili kuhakikisha
fedha za Serikali zinatumika kwa maendeleo ya wananchi.
|
No comments:
Post a Comment