|
May 28 2016 Serikali
iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalum ya
Ualimu wa Sayansi na Hisabati Chuo Kikuu Dodoma.
Wanafunzi
waliosimamishwa masomo walikuwa wamegawanyika katika makundi makuu mawili.
Kundi la kwanza lilikuwa ni wanafunzi 6,595 waliodahiliwa katika Stashahada
Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari na kundi la pili lilikuwa na wanafunzi
1,210 waliodahiliwa katika mafunzo ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi.
Taarifa iliyotolewa leo
na waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako
amesema kwamba baada ya hatua ya kuwaondoa wanafunzi chuoni kuchukuliwa,
Serikali ilifanya Uchambuzi wa wanafunzi
hao kwa lengo la kujiridhisha na sifa zao.
Baada ya uchambuzi huo leo July 19 2016 Serikali imetangaza maamuzi
haya…….
Kundi la Stashahada
Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari
Serikali imesema kwa
kuwa uchambuzi umebainisha kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja la I na la II
ambao pia wamefaulu masomo mawili ya Sayansi kwa kiwango cha C-A ni 382 (mwaka
wa I -134 na mwaka wa II – 248), wanafunzi hao ndiyo pekee watakaorudishwa katika
Chuo Kikuu cha Dodoma ili wakamalizie mafunzo yao katika Chuo hicho.
Wanafunzi 4,586 wa
mwaka wa I wa Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari
waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika Vyuo vya Ualimu vya Morogoro,
Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo yao.
Wanafunzi 1,337 wa
Mwaka II watahamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Korogwe na Kasulu kumalizia
masomo yao.
Wanafunzi 290 waliokuwa
wamedahiliwa kusoma Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya
Sekondari Masomo ya Sayansi na Hisabati ambao hawana sifa stahiki wanashauriwa
kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizo nazo kwenye chuo chochote
wanachotaka wao.
Kundi la Programu ya
Ualimu wa Elimu ya Msingi.
Serikali imesema
wanafunzi katika kundi hili hawakuwa sehemu ya program maalum ya kupunguza
uhaba wa walimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati.
Walikuwa wanaandaliwa
kufundisha shule za msingi wakati lengo la Programu Maalum ilikuwa ni
kukabiliana na tatizo za uhaba wa walimu wa Sekondari.
Maudhui ya program
waliyokuwa wanasoma hayakuwa sawasawa na yale ya Programu ya Ualimu wa
Sekondari wa Sayansi na Hisabati.
Wanafunzi 29 wa mwaka
wa II wenye Cheti cha Daraja IIIA waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Ualimu wa
Shule za Msingi watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo
yao kwa gharama zao wenyewe.
Wanafunzi 1,181
waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Kawaida ya Ualimu wa Elimu ya Msingi waombe
mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali popote watakapotaka wao.
Aidha Serikali imesema
itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM na wanafunzi
watakaohamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Serikali watapewa mkopo wa kiasi
cha Sh. 600,000/= kwa mwaka ambayo ni ada ya Mafunzo ya Ualimu itakayolipwa
moja kwa moja Chuoni.
|
No comments:
Post a Comment