Hospitali ya Kigoma,Kagera na Geita rasmi Hospitali za Rufaa za Mkoa. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, July 02, 2018

Hospitali ya Kigoma,Kagera na Geita rasmi Hospitali za Rufaa za Mkoa.

Hospitali ya Maweni mkoani Kigoma, Bukoba mkoani Kagera na ile ya Mkoa wa Geita zimetangazwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto rasmi kuanzia Juali 1 2018 Kuwa Hospitali za Rufaa za Mkoa.

Aidha Wizara hiyo  imepokea Hospitali 28 za Rufaa za Mikoa ambazo zilikuwa chini ya usimamizi wa OR-TAMISEMI .

 Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameyabainisha hayo leo July 02,2018 wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.

Hospitali ambazo tumezipokea zina jumla ya vitanda 7,474 na jumla ya watumishi 8,671 ambao, kati yao Wauguzi ni 3,960, Madaktari 536, Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ni 182, na waliobakia ni watumishi wa kada zingine mbalimbali za Afya” alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kuwa Hospitali ambazo Wizara imezipokea ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru (Arusha), Dodoma General (Dodoma), Kitete (Tabora), Shinyanga, Geita, Singida, Mpanda (Katavi), Mawenzi (Kilimanjaro), Bombo (Tanga), Morogoro, Ligula (Mtwara), Sokoine (Lindi), Maweni (Kigoma), Sekou Toure (Mwanza), Mwananyamala, Amana, Temeke (Dar es Salaam), Songwe, Kibena (Njombe), Iringa, Tumbi (Pwani), Sumbawanga (Rukwa), Bariadi (Simiyu), Musoma (Mara), Songea (Ruvuma), Mbeya, Babati (Manyara) na Bukoba (Kagera).

Waziri Ummy alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara imetenga shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya kipaumbele katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambako tayari huduma zinatolewa ikiwemo Matibabu kwa wagonjwa wa dharura ,Huduma za upasuaji wa dharura hususani wakati wa ujauzito na uzazi pamoja na Huduma za tiba kwa wagonjwa mahututi zikiwemo za watoto wachanga .

Mnamo Novemba 25, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akizindua Hospitali ya Taaluma na Tiba (MAMC) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) aliagiza kuwa Hospitali za Rufaa za Mikoa zihamishiwe kwenye usimamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW) kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad