TEC yaagiza Misa, Mafungo kuomba Mvua. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, January 14, 2017

TEC yaagiza Misa, Mafungo kuomba Mvua.

Maaskofu na Mapadre wote nchini Tanzania wameombwa kuandaa Misa, Mikesha, Mafungo, Hija na Maombi mbalimbali kwa ajili ya kuombea mvua kutokana na ukame uliopo.

Hayo yalibainishwa jana,January 13, 2017 katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Askofu wa Jimbo la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa.

Alisema kuwa hiki ni kipindi cha kilimo na mvua katika maeneo mengi nchini lakini hali sio ile iliyozoeleka kwani mvua hazifiki kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Kutokana na hali hii yapo maeneo Tanzania ambayo tayari yamekumbwa na uhaba mkubwa wa chakula. Ninaomba uwepo wa kasi ya sala kila mahali kuombea hali hii,” alisema Askofu Ngalalekumtwa. Alisema pia kuwa kuadhimishwa kwa misa, hija, maombi na mikesha kutasaidia kwa kuwa kila aombaye hupokea.

Alifafanua kuwa kila mmoja anapaswa kuomba baraka za Mwenyezi Mungu kuhusu kazi za mikono yake hususan kilimo ili akapate mazao ya nchi na kumtumikia Mungu kwa mioyo ya utulivu na shukrani.

Hata hivyo, akinukuu maandiko Matakatifu ya Biblia, Askofu Ngalalekumtwa alisema kuwa Mungu aliyewatunza wana wa Israeli walipokuwa safarini wakielekea nchi ya Ahadi kwa kipindi cha miaka 40, awaangalie kwa wema, upole na upendo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad