|
Idadi ya watu waliokufa
katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya Kampuni ya CITY BOYS imeongezeka na
kufikia 32 baada majeruhi aliyekuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu (ICU) kufariki dunia.
Ajali hiyo iliyohusisha
mabasi hayo wakati moja likitokea Dar es Salaam kuelekea Kahama mkoani
Shinyangana lingine likitokea Kahama kuelekea Dar es Salaam, ilitokea saa tisa
Jumatatu,Julai 04,2016 katika eneo la Maweni, Kata ya Kintiku Wilaya ya Manyoni mkoani
Singida.
Akizungumza jana,Julai 06,2016, Kaimu
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ibehzi Ernest alisema kazi ya kutambua
miili ya marehemu hao bado inaendelea.
Alisema hadi jana miili
ya watu 25 waliokufa kwenye ajali hiyo ilikuwa imetambuliwa na ndugu zao.
Dk
Ernest ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Ajali, Upasuaji na Mifupa alisema kati
ya maiti 25 zilizotambuliwa 12 zimechukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
“Wengine wametibiwa na
kuruhusiwa tumebaki na majeruhi watano ambao hali zao zinaendelea vizuri,”
alisema.
Kwa siku nzima ya juzi
na jana watu walikuwa wakipishana kuwatambua ndugu zao katika chumba cha maiti
cha Hospitali ya Rufaa ya Dodoma. Kutokana na miili kuharibika, ndugu hao
walikuwa wakirudi mara mbili kuangalia.
|
No comments:
Post a Comment