IMEELEZWA
kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, sawa na watu milioni 31.5, wako
hatarini kupata magonjwa ya ngozi, kutokana na kutumia vipodozi visivyo sahihi.
Kutokana na
hali hiyo, imesisitizwa ipo haja ya elimu ya athari ya vipodozi kutolewa
kuanzia shule za msingi, kwani wengi wa wanaoathirika wanakuwa na uelewa mdogo
juu ya matumizi ya vipodozi.
Hayo
yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi kutoka Hospitali ya Rufaa ya
KCMC ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Eliafoi Masenga wakati wa semina ya kupata
taarifa mbalimbali kuhusu vipodozi hatarishi, iliyofanyika Januari 08,2015, Dar
es Salaam.
Alisema
kutokana na uelewa mdogo, Watanzania wengi wanaathirika. Alitoa mfano kuwa yeye
peke yake anatibu magonjwa ya ngozi kwa watu wasiopungua 12,000 kwa mwaka.
Ofisa kutoka
Shirika la Envirocare, Ephrasia Shayo alielezea kushangazwa na kitendo cha
maduka ya vipodozi, kuuza dawa za hospitalini kinyume cha sheria na kuongeza
kuwa nayo yanachangia kuhatarisha afya za wananchi.
Alitaja
baadhi ya dawa za hospitalini, zinazouzwa katika maduka ya vipodozi kuwa ni
pamoja na Lemovate, Clobetasol, Betacort, Diproson na Mediven.
Alisema
sheria inaeleza wazi kuwa anayeuza vipodozi, haruhusiwi kuuza dawa za
hospitalini, ila anayeuza dawa ya hospitali anaruhusiwa kuuza vipodozi visivyo
na sumu, lakini kwa siku hizi watu wamekuwa wakikiuka sheria hiyo.
Aliongeza
kuwa wauza vipodozi wengi, hawana uelewa katika jambo hilo, ndiyo maana vidonge
vya malaria aina ya mseto vimekuwa vikitengenezwa mkorogo, ambao unachanganywa
na sabuni aina ya “Jaribu”, iliyokatazwa.
MADHARA.
Wakati
wataalamu hao wakionya hayo, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)
imeendelea kupiga marufuku vipodozi visivyo na ubora, vikiwemo vyenye viambato
vyenye sumu inayoathiri afya ya binadamu.
Madhara
yatokanayo na matumizi ya vipodozi vyenye viambato vya sumu ni kupata mzio wa
ngozi na athari kwenye ngozi inapopata mwanga wa jua. Athari hizo husababishwa
na kiambato sumu kiitwacho bithional.
Kwa mujibu
wa Ofisa Mwandamizi wa TFDA, James Ndege, madhara ya kiambato sumu
kijulikanacho kama hexachlorophene, ni kupenya hadi kuingia kwenye mishipa ya
fahamu na kusababisha ugonjwa, hasa kichwani.
Pia
husababisha ugonjwa wa ngozi na kuiathiri mtu anapokuwa juani. Kwa watoto
wachanga, hexachlorophene huathiri ubongo. Pia, husababisha ngozi kuwa laini,
kiasi cha kukaribisha ugonjwa wa fangasi au maambukizo ya vimelea vya maradhi.
TFDA inataja
madhara ya zebaki kuwa ni pamoja na kuharibu ngozi, ubongo, figo na viungo
mbalimbali vya mwili. Mjamzito akitumia vipodozi vyenye zebaki humwathiri mtoto
tumboni, ikiwa ni pamoja na kusababisha azaliwe akiwa na mtindio wa ubongo.
Matumizi ya
zebaki husababisha pia ngozi kuwa laini na mabaka meusi na meupe.
Husababisha
pia mzio wa ngozi na muwasho, ugonjwa wa mishipa ya fahamu na madhara ya upofu,
uziwi na upotevu wa fahamu mara kwa mara.
Vinyl
chloride: Hiki ni kiambato chenye sumu kinachosababisha magonjwa ya kansa ya
ini, ubongo, mapafu na mfumo wa damu. Sumu yake pia humsababishia mtumiaji
kuumwa kichwa, kuhisi kizunguzungu na kupoteza fahamu.
Kiambato
sumu aina ya zirconium husababisha kansa ya ngozi na mapafu. Athari kubwa za
kiambato sumu aina ya halogenated salicylanilide katika afya ya binadamu ni
ugonjwa wa ngozi na mzio wa ngozi mara inapopata mwanga wa jua.
Kwa upande
mwingine, kiambato cha hydroquinone husababisha muwasho na mzio wa ngozi,
kansa, kuchubuka kwa ngozi na kusababisha mabaka meusi na meupe.
Kadhalika,
kiambato aina ya steroids cha kundi la homoni, husababisha madhara mbalimbali
yakiwamo ugonjwa wa ngozi, chunusi, kulainisha ngozi kupindukia, kuchelewesha
kidonda kupona na magonjwa ya moyo.
Chloroform
ni kiambato chenye sumu ambacho husababisha kansa ya utumbo mpana na kibofu cha
mkojo. Husababisha pia ugonjwa wa akili na mishipa ya fahamu, ngozi kuungua,
maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu na kuota vipele.
Madhara
kwenye mishipa ya fahamu yanayosababisha mtu kutopumua vizuri husababishwa na
kiambato chenye sumu, kijulikanacho kama chlorofluorocarbon (halogenated
chlorofuoroalkanes).
Kiambato
sumu aina ya ethylene chloride husababisha kansa, madhara kwenye mishipa ya
kati ya fahamu, ini na mishipa ya moyo. Pamoja na madhara ya kiafya yaliyotajwa
hapo juu, pia kuna madhara ya kiuchumi yanayotokana na matumizi ya vipodozi
visivyo bora na salama.
|
No comments:
Post a Comment