|
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Jaji Frederick Werema (Pichani) amejiuzulu nafasi yake hiyo
kuanzia jana, Jumanne Desemba 16,2014, kufuatia sakata la uchotaji wa fedha kutoka akaunti ya
ESCROW ambapo zaidi ya dola milioni 120 zilihamishwa.
Mwanasheria
mkuu, pamoja na baadhi ya wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali
walituhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa
miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta.
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya Kikwete
amekubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.
Katika barua
yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema amesema ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri
wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua
hali ya hewa. Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake
ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.
kamati ya
Bunge ya hesabu za Serikali ilipeleka pendekezo kumtaka Jaji Werema kuwajibika.
Sakata la
Akaunti ya Escrow liliibuliwa bungeni na mmoja wa wabunge wa bunge la Tanzania,
David Kafulila na kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.
Baada ya uchunguzi
kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa mwezi Novemba,2014,
kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu taarifa ya ukaguzi maalum
kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na
umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni mwa
maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu, maafisa
waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini,
mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika katika kashfa hii na hivyo
kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria wahusika na wengine
kuondolewa katika nyadhifa zao za kuteuliwa.
Mwenyekiti
wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Zitto Kabwe
Kamati hiyo
ya Bunge pia ilipendekeza kuwa waziri wa Nishati na Madini, waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwanasheria mkuu, katibu mkuu wa wizara ya
Nishati na Madini na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe kwa
kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Pia maazimio
ya Kamati ya kudumu ya bunge ilipendekeza kuwa, kwa miaka mingi mikataba mibovu
ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na makampuni binafsi imeisababishia Tanesco
hasara ya mabilioni ya fedha na kutishia uhai wake wa kifedha, serikali
iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye kamati zake kwa lengo la
kutekeleza vema wajibu wake wa kuimamia na kuishauri serikali.
Akaunti ya
Escrow ilianzishwa katika Benki Kuu ya Tanzania ili kuhifadhi fedha, baada ya
kuibuka kwa mvutano kati ya Shirika la Umeme la Tanzania, Tanesco na kampuni ya
kufua umeme ya IPTL kuhusu ongezeko la mtaji wa uwekezaji, huku TANESCO
ikilalamika kuwa gharama za kununua umeme kutoka kampuni ya IPTL zilikuwa za
juu mno.
Fedha hizo zingeendelea kutunzwa katika Akaunti hayo hadi wakati
ambapo suluhisho la mvutano wa wabia hao wawili lingepatikana.
Habari Na:-BBC Swahili.
|
No comments:
Post a Comment