Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi
kuendesha operesheni kabambe, itakayofanyika kwa kushtukiza wakati wowote
kuanzia sasa, kuwaondoa kwa nguvu nchini Raia wa Kigeni wanaoishi nchini kinyume cha Sheria na waliokaidi agizo
la Rais Jakaya Kikwete, lililowataka
kurejea makwao kwa hiari yao ndani ya wiki mbili, kuanzia Julai 29, mwaka huu.
Wahamiaji
hao , ambao wamekuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria za nchi na taratibu za
Idara ya Uhamiaji, wanatoka katika nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Agizo
hilo lilitolewa na Rais Kikwete Julai 29, mwaka huu, alipofanya ziara katika
Mkoa wa Kagera, ambako aliwapa wiki mbili wahamiaji haramu wawe wamerudi makwao
kwa hiari yao, vinginevyo wangekamatwa katika operesheni maalumu ya kijeshi
baada ya muda huo kuisha.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwaambia waandishi wa
habari, jijini Dar es Salaam jana(Agosti 20,2013) kuwa operesheni hiyo
aliyoiita ya “ghafla”, itafanyika baada ya Rais Kikwete kumpa kibali cha
kuiendesha.
Alisema
maeneo yatakayohusika zaidi na operesheni hiyo ni ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na
kwamba, hawatakuwa na ‘msalie mtume’ kwa mgeni yeyote atakayebainika kuishi
nchini isivyo halali.
Aliwataka
viongozi wa serikali za vijiji vilivyoko katika mikoa ya kanda hiyo kufahamu
kwamba, ni kosa kisheria kushirikiana na wahamiaji haramu.
Kutokana
na hilo, alionya kuwa watakaobainika wakiwaficha Raia hao wasiokuwa na Kibali halali cha kuishi nchini, watakamatwa
na kufikishwa mahakamani.
Awali,
Waziri Nchimbi alisema baada ya agizo hilo la Rais Kikwete, mwitikio umekuwa
mzuri na kwamba, hadi kufikia usiku wa Agosti 18, mwaka huu, Raia hao wasiokuwa na kibali halali cha kuishi nchini
10,672 walikuwa wameondoka nchini na mali zao.
Alisema
kati ya wahamiaji hao , katika Mkoa wa Kagera, Wanyarwanda walikuwa
6,088, Warundi 4,000 na Waganda 269.
Kwa
mujibu wa Waziri Nchimbi, katika Mkoa wa Kigoma, walioondoka ni 150, kati yao
Warundi ni 142 na DRC ni wanane.
Alisema
katika Mkoa wa Geita wahamiaji walioondoka ni 165; kati yao Wanyarwanda
ni 126 na Warundi 39.
Hata
hivyo, alisema kazi ya wahamiaji hao kuondoka nchini, bado inaendelea na
kuwataka wananchi hususan wa Mkoa wa Kagera kuwaacha waondoke bila kunyanyaswa,
ikiwamo kupora mali zao.
Hata
hivyo, alisema kati ya wahamiaji haramu walioondoka, 14 wamerudi tena nchini na
kukiita kitendo hicho kuwa ni cha “kichokozi.”
Alisema
Rais Kikwete alitoa agizo lile baada ya wizara kufanya utafiti na kumpa taarifa
na kwamba, wahamiaji haramu wanaosumbua ni wale wanaomiliki vyeti bandia vya
kuzaliwa.
No comments:
Post a Comment