Sheikh Issa Ponda Issa. |
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI 12 AUGUSTI 2013.
YAH:
KUJERUHIWA KWA SHEIKH ISSA PONDA ISSA.
KWA mara
nyingine tena, sisi mashirika ya utetezi wa haki za binadamu, THRD-Coalition,
LHRC, SIKIKA, TGNP, CPW na TAMWA tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe
wetu huu kwa wananchi wa Tanzania.
Ujumbe wenyewe unahusu kujeruhiwa kwa Sheikh
Issa Ponda Issa na hali inayoendelea kukua ya uvunjaji wa haki za binadamu
nchini.
Jana, tarehe
11 August 2013 tulipokea kwa masikitiko makubwa taarifa rasmi ya Jeshi la
Polisi nchini kuhusu tukio la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya za Kiislam
Tanzania – Sheikh Issa Ponda Issa lililotokea mkoani Morogoro tarehe 10 August
2013.
Awali ya
yote, tuseme wazi, kuwa hatufungamani na taasisi yoyote ya dini wala chama
chochote cha siasa. Wajibu wetu mkuu ni kuhakikisha kuwa haki za binadamu
zinaheshimiwa na kulindwa kikamilifu bila upendeleo au ubaguzi kwa misingi
yoyote ile.
Tunasikitishwa
sana na hali ya uvunjaji wa haki za binadamu inayotokana na tabia iliyokithiri
ya vyombo vya dola kutumia nguvu inayokiuka haki za msingi za wananchi.
Tunapenda kuwafahamisha kuwa, tunalaani matumizi ya nguvu yanayofanywa na
vyombo hivyo. Pia, tunahuzunishwa na uhalifu, vurugu na tabia ya wananchi
kujichukulia sheria mikononi na hatukubaliani na vitendo vyovyote vile vya
kuvunja amani. Maathalan vitendo vinavyoongezeka vya wananchi kutumia tindikali
kama silaha dhidi ya wenzao.
Tunafahamu
kuwa, wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao na kuwa wanayo haki
ya kuwakamata washukiwa wa uahlifu kwa mujibu wa sheria. Pamoja na yote
tunalaani kitendo alichofanyiwa Kiongozi wa Jumuiya za Kiislam Tanzania, Sheikh
Issa Ponda Issa. Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, tumeelezwa kuwa
Sheikh Ponda alijeruhiwa wakati 'polisi walipopiga risasi hewani ili
kuwatawanya wale waliokuwa wafuasi wake.'
Na pia kwa mujibu wa vyombo vya
habari vilivyodai kumhoji ndugu Isihaka Rashid, tumeelezwa kuwa Sheikh Ponda
alipigwa risasi begani na Polisi.
Kutokana na
hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:-
1. Kutokana
na uzoefu tulio nao wa matukio yanayofanana ya hayo, hatuna imani kabisa na
kamati/tume iliyoteuliwa na Jeshi la Polisi ili kuchunguza tukio hilo. Hofu
yetu inatokana na ukweli kwa Jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa kumjeruhi Sheikh
Ponda, na kutokana na misingi ya haki za asili – haikubaliki mhusika kuwa
hakimu kwenye shauri linalomhusu.
2. Tunalaani
kabisa utaratibu ambao Jeshi la Polisi liliutumia ili kumkamata Sheikh Ponda.
Utaratibu huu wa kumkamata mtuhumiwa mbele ya halaiki ya wafuasi wake ulikuwa
ni hatarishi kwa maisha ya askari wenyewe pamoja na maisha ya raia na pia
ilikuwa inaibua hamasa na hamaki ya umma.
3. Tunatoa
wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo Kikatiba ina jukumu la
kufuatilia na kuchukua hatu kwa masuala kama haya , ifanye hima kufuatilai na
kuchukua hatua zote stahiki za kisheria. Aidha ikiwa Tume itahitaji msaada wetu
wa rasilimali watu na fedha, tuko tayari kuisaidia ili ifanye kazi hii kwa
haraka kama inavyostahili.
4. Tunaiomba
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ifuatilie pia matukio mengine ya
matumizi ya nguvu yanayofanywa na vyombo vya dola katika sehemu mbalimbali kama
vile Mtwara, Arusha, Zanzibar, Kigoma na sehemu nyinginezo nchini.
5.
Tunawaomba wananchi wawe watulivu na wazingatie sheria za nchi katika kudai
haki zao.
6.
Tunavitaka vyombo vya dola vianza kujifunza kutenda haki kwa kuzingatia misingi
ya haki za binadamu na utawala bora.
7. Tunampa
pole katibu wa Jumuiya za Kisilam Tanzania Sheikh, Issa Ponda Issa pamoja na
wote walioathirika katika kadhia hiyo.
Imeandaliwa
na Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania na kusoma kwenu kwenu na;-
Onesmo
Olenguruwa,
Mratibu wa
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania.
No comments:
Post a Comment