Ningependa kuwatakia Waislamu wote ulimwenguni Sikukuu njema ya Eid! Eid Mubarak! - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, August 09, 2013

Ningependa kuwatakia Waislamu wote ulimwenguni Sikukuu njema ya Eid! Eid Mubarak!

Ni msimu wa sikukuu ambao kimsingi unahitimisha rasmi kuondoka kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ni wakati wa kuzichunga nafsi na kurejea kule zilikokuwa kabla ya mfungo.

Kuondoka kwa Ramadhan maana yake ni wafungaji walewale kujiandaa na mfungo mwingine wa siku sita (sitashaawal) na kuanza kwa mwaka mpya wa Kiislamu.

Tukiwa ndani ya mfungo na hata kabla mfungo haujawadia kulikuwa na maandalizi ya aina yake. Maandalizi yalijumuisha kutafuta mavazi ya heshima na staha na yale ya ajabu ajabu kufichwa kabisa na kuruhusu mfungo utawale.


Hadithi zinatukumbusha kwamba kabla mfungo haujaanza sheitwani huwa anaingia kifungoni ili kuwaepusha wafungaji na mambo yake machafu.

Ndiyo maana ndani ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kunashuhudiwa utulivu wa hali ya juu.

Mfungo ndio huo unaondoka na heshima, ustaarabu, utaratibu, upole na unyenyekevu wake.

Ibilisi anaachwa huru na kurudi ulingoni kuwapotosha wafungaji waliojinyima kwa siku hizo walizoruzukiwa na Mwenyezi Mungu.

Haitapendeza, si ustaarabu wala uungwana kwa mfungaji mara mwezi mtukufu unapoondoka na yeye mara moja anarudi kwenye uchafu ambao alikuwa ameusitisha wakati wa mfungo.

Hii inanikumbusha hadithi moja inayosema ni sawa na mtu aliyetoka kuoga na anapomaliza anaingia tena kwenye matope na kuchafuka upya.

Ndiyo maana Mtume (S.A.W) alisema ana hasara yule ambaye mwezi mtukufu umemdiriki na ukaondoka akiwa hajasamehewa madhambi yake kwani kuuona au kuupata tena ni majaaliwa yake Allah (S.W).

Kuwadia kwa Eid hakumaanishi marejeo ya machafu tuliyokuwa tumeyaacha na tukiomba usiku na mchana kusamehewa madhambi yake.

Itakuwa hasara kwetu kama ilivyotajwa na Mtume (S.A.W). Tunapaswa kuzichunga nafsi na uchafu hasa siku ya Eid Mosi na vile vile tujipange kwa Sitashaawal.

Mfungo wa siku sita nao tunapaswa kuudiriki kwani nao una fadhila kubwa ndani yake.

Na tukimaliza mfungo sita ndiyo mwanzo wa kujiandaa na hasa wale wenye uwezo kwenda kufanya ibada ya kuhiji miji mitukufu ya Makkah na Madina.

Tusherehekee Sikukuu ya Eid kama ilivyoelekezwa na Allah (S.W) na mjumbe wake Mtume Muhammad (S.A.W).

Tumuombe Allah atughufirie madhambi yetu na atuepushe na sheitwani muovu.

Ni sikukuu ya kula na kunywa vilivyo halali pekee, atakaye kula na kunywa vya haramu hakuichunga nafsi yake.

Napenda  Kuwatakia Wadau wote wa Mwana wa Makonda.Blog  Eid-el-Fitr njema na  Kwa wale walioweza Kitimiza Nguzo Hii Muhimu ya Kufunga Katika Mwezi Huu wa Ramadhani basi Naomba Mwenyezi Mungu azikubali Funga zenu na Dua zote, Mwenyezi Mungu awazidishie Mema ya Duniani na Funga zenu ziwe za Kheri,
Tushereheke Siku kuu hii kwa Amani na Upendo, Na Kufanya yale yote yanayo Mpendeza Mwenyezi Mungu.


Wabillahi Tawfiq


0789 925 630/0756 830 214/0654 399 127.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad