![]() |
Nape Nnauye. |
Suala
la kutimuliwa kwa madiwani wanane wa CCM katika Manispaa ya Bukoba limeingia
sura mpya baada ya Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk Anatory Amani na Mbunge wa
Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kushiriki katika siasa mkoani humo hadi
mwaka 2015.
Habari
zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa
baada ya kubainika mgogoro wa viongozi hao, unakiumiza chama katika jimbo hilo.
Taarifa
zilidai chanzo cha ugomvi kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani, ni kwa kila
mmoja kutaka kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Bukoba mjini katika uchaguzi
ujao. Na kwa uamuzi huo, Kagasheki na Dk Amani hawatashiriki uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015.
Hata
hivyo, akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye alisema viongozi hao watakutana na Kamati Kuu leo na baada
ya hapo utatangazwa uamuzi uliofikiwa.
Mbali
na meya na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, wengine
walioitwa katika kikao hicho cha leo ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo,
Costansia Buhinye, katibu wake, Averin Mushi pamoja na mwenyekiti wa chama
Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na katibu wake, Janath Kayanda.
Kutokana
na uamuzi huo, Kamati Kuu ambayo ilimaliza kikao chake saa 8:30 usiku wa
kuamkia jana italazimika kukaa tena leo kuwaelezea uamuzi uliofikia.
Kumekuwapo
na mgogoro mkubwa katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, ukimuhusisha
Kagasheki na baadhi ya madiwani kwa upande mmoja; na Dk Amani na kundi jingine
la madiwani kwa upande mwingine.
Wakati
wa mgogoro huo madiwani wamekuwa wakituhumiana ufisadi, na CCM imekwishawatuma
viongozi wake wa juu kuingilia kati mgogoro huo akiwamo mwenyekiti wake, Rais
Jakaya Kikwete, lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana.
Kufikishwa
kwenye Kamati Kuu kwa suala hilo kumekuja baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa
Kagera kuamua kuwatimua uanachama madiwani hao, hatua ambayo ilikuwa
inahatarisha nafasi zao na hivyo kukiingiza chama hicho kwenye uchaguzi mdogo.
Habari
kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi
hao kuwajibishwa kwa kukiuka kanuni, kwa kuwa upo uamuzi wa chama unaokataza
viongozi waliochaguliwa katika vyombo vya dola kuwajibishwa kwa staili hiyo.
Madiwani
waliovuliwa uanachama na kata zao katika mabano ni pamoja na Richard Gaspar
(Miembeni ), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia
ni Naibu Meya (Buhembe) na Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa
Wilaya (Kashai).
Wengine
ni Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa
(Kitendaguro) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Habari Na:Mwananchi Jumapili.
No comments:
Post a Comment