Kamanda Gurumo astaafu muziki baada ya kuitumikia fani hiyo kwa miaka 53. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, August 23, 2013

Kamanda Gurumo astaafu muziki baada ya kuitumikia fani hiyo kwa miaka 53.

Mwimbaji Mkongwe wa Bendi ya Msondo Ngoma Muhidini Gulumo kushoto akiimba sambamba na Hassani Moshi 'Tx Jr' wakati wa bendi hiyo ilipotumbuiza katika ukumbi wa Max Bar Ilala Bungoni, Gulumo ni mwanamziki Mkongwe pekee aliyedumu katika Jukwaa kwa mda mrefu nchini .

Waimbaji wa bendi ya Msondo ngoma wakitoa burudani wakati walipokuwa wakitumbuiza katika ukumbi wa Max Bar Ilala Bungoni kutoka kushoto ni Muhidini Gulumo,Hassani Moshi na Shabani Dede.

NGULI wa muziki wa dansi nchini na kiongozi wa Msondo Ngoma Music Band, Muhidin Gurumo ‘Kamanda’ (73), ametangaza rasmi kustaafu baada ya kuitumikia fani hiyo kwa miaka 53.

Kamanda Gurumo aliyabainisha hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam jana, na kwamba anaondoka katika fani akiwa hana kitu.

Leo nimekuja kuwaaga rasmi wanamuziki na wapenda muziki na waliokuwa mashabiki wangu kwa ujumla, sitaki tena muziki, ila ikumbukwe kwamba, muziki ni asili yangu, ila sasa nimeamua kustaafu kwa moyo mmoja, hivyo naahidi kuwa nitawasaidia wanamuziki wanaobaki kwa uhuru na moyo mmoja,” alisema Gurumo.

Gurumo alisema anastaafu akiwa hana kitu cha maana katika tasnia ya muziki wa dansi, licha ya kuutumikia na kufanya kazi kwa moyo wake wote kwa miaka 53.

Nilianza kuimba nikiwa kijana wa umri wa miaka 20 mwaka 1960 na tangu hapo sikuwahi kubadili kazi, lakini sasa nastaafu ilhali nikiwa sina hata baiskeli,” alisema Gurumo.

Wosia wake kwa wanamuziki wanaobaki, anawaasa wapige muziki wa nyumbani, hasa waliokuwa wakipiga bendi ya Msondo.

Wapige muziki ambao tulikuwa tunapiga sisi zamani, tofauti na hivi sasa, ambapo wanamuziki na vijana wengi wanakimbilia katika muziki wa Bongo Fleva, ambao ni muziki unaokwenda na wakati, lakini ni wa kupita,” alisema.

Aliongeza kuwa kustaafu kwake hakuzuii kutoa ushauri au kufundisha wanamuziki na wapiga ala, kwani ana kipaji cha kumfundisha mpigaji wa chombo chochote kwa kutumia mdomo wake.

Kadhalika, Gurumo anasema katika nyimbo alizowahi kuimba, wimbo anaoupenda ni ‘Usimchezee Chatu’, ambao aliuimba kipande kidogo mbele ya waandishi wa habari na katika wanamuziki wa Bongo Fleva, anampenda, Nasib Abdul ‘Diamond’.

Wakati huo huo, Mratibu mkongwe nchini wa matamasha mbalimbali na mwanzilishi wa ‘viota’ na kumbi nyingi za burudani jijini Dar es Salaam, Juma Mbizo, anatajwa na Gurumo kuwa ndiye atakuwa mratibu katika tamasha maalumu litakaloandaliwa la kumuaga.

Katika kamati hiyo pia wamo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (Aset), Asha Baraka, mdau wa burudani, Said Mdoe, Richardson Sakalla na Mkurugenzi wa bendi ya The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’, Waziri Ally.

Hii kamati imeundwa ili iweze kumsaidia katika kumuandalia tamasha maalumu, hivyo ipo siku tutaweka wazi tumeandaa kumfanyia nini mkongwe huyu wa dansi, kadhalika siku hiyo ya tamasha lake, ndipo atakapoimba kwa mara ya mwisho na kuanzia leo hatapanda katika jukwaa lolote kuimba,” alisema Mbizo.


Mbizo aliongeza kuwa, Gurumo amepata ridhaa kutoka kwa wanamuziki wenzake wote kabla ya kufikia uamuzi huo, na kwa kuwa ameimba kwa miaka mingi, sasa ni wakati wake wa kupumzika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad