VIDEO :Francis ‘SMG’ Cheka alivyotawazwa kuwa bingwa mpya wa dunia wa WBF, katika uzito wa Super Middle baada ya kumshinda Mmarekani, Phil Williams kwa Pointi. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, August 31, 2013

VIDEO :Francis ‘SMG’ Cheka alivyotawazwa kuwa bingwa mpya wa dunia wa WBF, katika uzito wa Super Middle baada ya kumshinda Mmarekani, Phil Williams kwa Pointi.

Mgeni Rasmi katika Mpambano wa Kimataifa wa kuwania Mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa WBU,kati ya Mabondia Francis Cheka wa Tanzania na Phil Williams wa Marekani,Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo, Mh. Dkt. Fenella Mukangala (mwenye koti jeupe) akimvisha Mkanda wa Ubingwa huo, Bondia Francis Cheka baada ya kumshinda kwa Point Mpinzani wake, katika Mchezo uliomalizika usiku huu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee,Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Bingwa wa Zamani wa Masumbwi, Fransous Bhotha.


Bondia Francis Cheka wa Tanzania (kushoto) akimrushia makonde makali mpinzani wake, Phil Williams kutoka nchini Marekani wakati wa mpambano wao wa Kimataifa kuwania Mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa WBU,uliofanyika usiku huu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee,Jijini Dar es Salaam.Bondia Francis Cheka ameibuka kidedea baada ya kumchapa mpinzani wake huyo kwa Point.

Wanahabari wakipata taswira za mpambano huo ambapo hadi mwisho wa mchezo uliokuwa wa raundi 12,Francis Cheka aliweza kuibuka Kidedea kwa kumchapa mpinzani wake huyo kwa point na kufanikiwa kumnyang’anya mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa WBU.
 




BONDIA Mtanzania, Francis ‘SMG’ Cheka Jana (Agosti 30,2013) usiku wa kuamkia leo ametawazwa kuwa bingwa mpya wa dunia wa WBF, katika uzito wa Super Middle baada ya kumshinda Mmarekani, Phil Williams kwa pointi katika pambano la Raundi 12, lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Jaji wa kwanza Eddie Marshall kutoka Afrika Kusini alitoa pointi 116 kwa 115, jaji wa pili Fidel Hayness alitoa pointi 119 kwa 118 na jaji wa tatu, John Chagu alitoa pointi 117 kwa 116 (wote wa Tanzania), wakimpa ushindi Cheka.

Kwa ushindi huo, Cheka amefuata nyayo za bondia mwingine Mtanzania, Rodgers ‘Tiger’ Mtagwa ambaye aliwapiga Wamarekani kadhaa kwao, ambako anaishi tangu 1998.

Miongoni mwa mabondia Wamarekani ambao Mtagwa, mtoto wa Keko Mwanga, Temeke, Dar es Salaam amewahi kuwapiga ni Garvin Crout kwa Knockout (KO) Raundi ya kwanza pambano la Raundi nane, kwenye ukumbi wa Blue Horizon, Philadelphia, Pennsylvania, Marekani pambano lililochezeshwa na refa James Condon Septemba 12, mwaka 2000 na mwingine Donovan Carey kwa KO pia Raundi ya Pili Juni 15, 2001 ukumbi huo huo.

Katika pambano hilo lililochezeshwa na refa kutoka Afrika Kusini, Drake Ribbinck, mabondia hao walianza kwa kusomana Raundi ya kwanza wakitupiana makonde ya tahadhari na katika Raundi ya pili, kila mmoja alitaka.

Cheka aling’ara katika Raundi ya Tatu na ya nne na Mmarekani akaibuka Raundi ya Tano na kuanza kuonyesha upinzani. Raundi ya Sita Mmarekani aliongeza kasi ya urushaji makonde na Raundi ya saba na ya nane walipigana sawa, ingawa Williams alianguka kwa kuteleza na kuinuka kuendelea na pambano.

Raundi ya 10 mabondia hao waliendelea kutupiana makonde kwa zamu, lakini Raundi ya 11 na 12 pamoja na Williams kusimama imara kutafuta ushindi wa Knockout (KO), lakini SMG alikuwa makini katika kukwepa na kurusha ngumi za kudonoa kichwani kwa mpinzani wake.

Na kwa sababu hiyo haikushangaza baada ya pambano, bondia mwenye maskani yake Morogoro kutangazwa bingwa mpya wa WBF.

Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara aliyekuwa mgeni rasmi alijaribu kwa tabu tabu kumvisha taji Cheka kutokana ulingo kuvamiwa na mashabiki waliopagawa na ushindi wa bondia huyo.

Katika mapambano ya utangulizi, Thomas Mashali alimshinda kwa pointi Mada Maugo, wakati Alphonce Mchumia Tumbo alimshinda kwa Technincal Knockout (TKO), baada ya wasaidizi wake kurusha taulo Raundi ya tano katika pambano la Raundi sita.

Hata hivyo, dosari  iliyojitokeza katika usiku huo ni mabondia kugoma kupanda ulingoni hadi kwanza walipwe fedha zao na ilianzia kwa Mchumia Tumbo, ikafuatia kwa Maugo na Mashali na baadaye Cheka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad