Wanajeshi
saba wa Tanzania, ambao ni miongoni mwa kikosi cha Umoja wa Mataifa, cha
kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wanadaiwa kuwa wameuawa.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kwamba wanajeshi hao wa Tanzania,
wamekufa kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi wanaopigana na
Serikali.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, miili yao wanajeshi hao bado ipo nchini Sudan ikisubiri
taratibu za kusafirishwa kuletwa nchini.
Hii
ni mara ya kwanza kuripotiwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Tanzania
wanaolinda amani katika nchi mbalimbali kufa kwa wakati mmoja.
Agosti
mwaka jana wanajeshi watatu wa Tanzania huko Darfur waliripotiwa kuuawa kwenye
tukio kama hilo.
Msemaji
wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , Kanali Kapambala Mgawe
alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu vifo vya wanajeshi wa Tanzania huko Darfur,
alisema kuwa naye amesikia, lakini hana taarifa rasmi kwa mujibu wa taratibu za
kiofisi.
Hii
ni mara ya pili kwa wanajeshi wa Tanzania kuuawa katika Jimbo la Darfur, ambapo
Agosti mwaka jana, Kanali Mgawe alinukuliwa na vyombo vya habari akithibitisha
kutokea kwa vifo vya askari watatu ambao gari lao lilizolewa na maji walipokuwa
wakivuka mto uliokuwa umefurika maji.
Kanali
Mgawe aliwataja askari hao kuwa ni Sajini Julius Chacha, Sajini Anthony Daniel
na Koplo Yusuph Said na kwamba askari wengine walinusurika baada ya kuogolea.
Tanzania
ina askari 850 kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani jimbo la
Darfur, ambao ni sehemu ya askari 1,081 wa kulinda amani katika jimbo la
Darfur.
Wanajeshi
hao wa Tanzania wametawanywa kwenye miji ya Khor Abeche na Muhajeria kusini mwa
Darfur.
Aprili
mwaka huu Tanzania ilipeleka wanajeshi wa kulinda amani katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupambana na kikundi cha waasi wa nchi hiyo M23
kinachopigana kuiangusha serikali ya DRC.
Majeshi
ya Tanzania yalipelekwa kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa. Tanzania
inaungana na nchi za Afrika Kusini na Malawi kukamilisha kikosi cha wanajeshi
3,000. Tanzania imepeleka wanajeshi 850.
Chanzo:
Gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment