MBUNGE wa
Karagwe, Gozbert Blandes (CCM), ameshindwa kufanya mkutano wa hadhara katika
mji wa Kayanga, wilayani humo baada ya kukosa wananchi wa kuwahutubia.
Blandes
alipanga kufanya mkutano wa hadhara mjini Kayanga Jumamosi ya Agosti 3, mwaka
huu, lakini alilazimika kuuahirisha baada ya mahudhurio ya wananchi kuwa
hafifu.
Dalili za
mkutano huo kutofanikiwa zilianza kuonekana siku moja kabla wakati mtu
aliyekuwa akitangaza taarifa za kuwepo kwa mkutano huo kusema: “Wale waliokuwa
wakisema Blandes hawezi kufanya mkutano Kayanga waje wajionee.”
Kauli hiyo
iliashiria kuwepo shaka kwa waandaaji wenyewe kuhusu kufanikiwa kwa mkutano
huo.
Akitoa
taarifa za kuahirishwa kwa mkutano huo, Katibu wa CCM wilayani humo, Anatory
Nshange, alidai kuwa Blandes asingefanya mkutano kutokana na kuwepo kwa
shughuli ya bomoa bomoa ya nyumba mbili za wananchi katika eneo la Mgakorongo
mjini hapa.
Hata hivyo,
katibu huyo hakueleza uhusiano wa mkutano wa mbunge na bomoa bomoa, hasa
ikizingatiwa kuwa nyumba zilizobomolewa ni za wanachama wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadena).
“Ndugu
wananchi wa Kayanga, leo tulipanga kufanya mkutano wa mbunge wetu hapa mjini
Kayanga, lakini tumeamua kuuahirisha kwa sababu kumejitokeza bomoa bomoa kule
Mgakorongo.
“Tunawaomba
radhi sana kwa usumbufu wowote, lakini tunawaahidi tutaandaa mkutano mwingine
na tutawataarifu,” alisema Nshange.
Uchunguzi wa
Tanzania Daima umebaini kuwa kuahirishwa kwa mkutano huo kunatokana na
kukosekana watu hali iliyosababishwa na mgogoro wa kisiasa ulioibuka baada ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kufuatia utata wa matokeo yaliyompa ushindi
Blandes.
Wananchi
wengi wa jimbo la Karagwe wanaamini kuwa Blandes hakushinda uchaguzi huo na
kwamba alipora ushindi wa aliyekuwa mgombea wa CHADEMA kwa kusaidiwa na Jeshi
la Polisi wilayani humo.
“Huyu si
mbunge wetu; mbunge wetu ni wa CHADEMA. Blandes alipata ubunge kwa kutumia
mitutu ya bunduki za polisi na mabomu ya machozi.
“Hatuwezi
kwenda kumsikiliza mtu aliyeingia madarakani kwa njia za mabavu kwani kukubali
kumsikiliza ni sawa na kukubaliana na kuhalalisha uporaji wa kura aliofanya
mwaka 2010,” alisema mwananchi mmoja.
“Hatuwezi
kwenda kumsikiliza mtu ambaye aliwaagiza polisi kutufyatulia risasi za moto na
kutupiga mabomu mwaka 2010. “Kwa nini tukamsikilize mtu aliyekusudia kutuua?
Akawahutubie hao polisi wake,” alieleza mwananchi mwingine ambaye pia hakutaka
kuandikwa jina gazetini.
Alipotafutwa
mbunge huyo kuzungumzia sababu za kuahirishwa kwa mkutano wake, alikanusha
kupanga kufanya mkutano huo kama ilivyotangazwa na viongozi wake wa chama.
“Siyo kweli!
Sijapanga wala kuandaa mkutano Kayanga, kama hao viongozi wa CCM wamesema kuwa
nimepanga kuhutubia hapo hawakuwa wakweli.
“Labda wao
walipanga na walitaka kupata watu kupitia kwangu. Naomba uniamini mimi maana
ubunge wangu hauna ubia na mtu yeyote,” alisem Blandes na kudai kwa sasa yuko
nchini Uganda.
Habari Na
George Maziku,Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment