![]() |
Kamanda Henry Kilewo... |
Hatimaye
makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaokabiliwa na
shtaka la kummwagia tindikali kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wameachiwa kwa
dhamana na Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga.
Makada hao
ambao wanatetewa na mawakili Prof. Abdallah Safari na Peter Kibatala ni pamoja
na Avodius Justinian (Bukoba), Oscar Kaijage (Shinyanga), Rajabu Daniel
(Dodoma), Seif Magesa (Mwanza) na Henry Kileo (Dar es Salaam).
Muda mfupi
baada ya kuachiwa, vijana hao walifichua jinsi walivyopata mateso makali kutoka
kwa maofisa wa jeshi la polisi wakilazimishwa kuwataja viongozi wa juu wa
CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, John Mnyika
na Tundu Lissu kuwa wanahusika na ugaidi.
Bila
kumung’unya maneno waliwataja vigogo kadhaa wa serikali, CCM na mbunge mmoja wa
CHADEMA kuwa ndiyo waratibu wa mikakati hiyo ya kuwabambika CHADEMA kesi za
ugaidi.
Vijana hao
waliowasili mjini Igunga 12:45 jioni juzi na kupandishwa kizimbani katika
mahakama hiyo saa 1:20 usiku na kusomewa shtaka lao la kufanya kitendo
kilicholenga madhara mwilini.
Mapema
hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi,
Mrakibu Msaidizi, Cosmas Mboya, makada hao walidaiwa kutenda kosa la kummwagia
tindikali kada wa CCM, Mussa Tesha, usiku wa Septemba 9, 2011, katika msitu wa
Hanihani, Igunga.
Mbela ya
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ajali Milanzi, ilidaiwa na mwendesha mashtaka
kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walimmwagia kada huyo tindikali sehemu za uso,
puani, mdomoni na kwenye bega la kulia.
Mwendesha
mashtaka alidai kuwa shauri hilo limekwenda wilayani Igunga baada ya Mahakama
Kuu, Kanda ya Tabora, kuwafutia shtaka la ugaidi na kuamuru kwamba warejeshwe
Igunga na kushtakiwa kwa kosa la kumwagia tindikali kisha wapatiwe dhamana.
“Masharti
ya dhamana yaliyowekwa na mahakama ni kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja
atakayesaini dhamana kwa ahadi ya sh milioni 10 za maandishi kila mmoja.
Washtakiwa
wote walikana shtaka hilo na kutimiza masharti ya dhamana kisha hakimu
akaiahirisha kesi Septemba 10 mwaka huu itakapotajwa tena.
Katika hatua
nyingine, vifijo, nderemo, vilio vya furaha na shangwe vilitawala mahakamani
hapo baada ya makada hao kuachiwa kwa dhamana.
![]() |
Makada
CHADEMA wakiingia ,
mahakamani
mjini Tabora.
|
Wafuasi wa
CHADEMA walifanya maandamano yaliyoongozwa na msururu wa magari, pikipiki na
baiskeli wakitembea umbali wa takriban kilomita tano kutoka mjini Igunga kwa
lengo la kuwapokea makada hao.
Akizungumza
kwa kifupi, wakili wao Peter Kibatala, aliendelea kuishukuru Mahakama Kuu Kanda
ya Tabora kwa kuonyesha ujasiri wake na kutimiza majukumu yake ya kutoa haki.
“Namshukuru
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Simon Likelerwa, kwa weledi wake
wa kutoa uamuzi ulio sahihi kisheria na ulioshiba.
“Pia
naipongeza mahakama ya Igunga kwa kuwapatia dhamana washtakiwa kwa masharti
yanayoendana na uzito wa jambo lenyewe kwani dhamana ni haki ya msingi kwa
mshtakiwa yeyote,” alisema.
Mwenyekiti
wa CHADEMA Mkoa wa Tabora, Kansa Mbaruku, alisema kuwa pamoja na kuridhishwa na
hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, pia hiyo ni ishara kuwa
haki imezingatiwa kisheria.
Awali
makada hao walifutiwa mashtaka na mahakama ya wilaya ya Igunga kisha kukamatwa
tena na kupelekwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kusomewa shtaka la ugaidi
ambalo hata hivyo lilifutwa na mahakama hiyo.
Mikakati
ya hujuma
Wakisimulia
kile kilichowapata tangu kukamatwa kwao hadi kufikishwa mahakamani, makada hao
walisema kuwa walipata mateso makubwa huku wakilaghaiwa kupewa vyeo serikalini
na fedha ili mradi wawahusishe viongozi wa CHADEMA na ugaidi.
Evodius
Justinian (Bukoba)
Alisema
kuwa alikamatwa Bukoba: “Nikakaa rumande siku tatu kabla ya kusafisirishwa hadi
Mwanza. Nikiwa huko niliteswa sana ili nikubali kuwa ninajua ule mkanda wa
Wilfred Lwakatare uliokuwa kwenye mitandao.
“Nilikataa,
niliteswa sana nikahojiwa kama nilimmwagia Musa Tesha tindikali nilikataa.
Nilisafirishwa kwa ndege kuja Dar es Salaam ambako nilipokelewa na polisi.
“Nikiwa
uwanja wa ndege niliomba ruhusa kwenda chooni, askari walinifuata huko
wakanitesa sana. Nilifanyiwa mahojiano na Advocate Nyombi na afande Pasua.
Walinilazimisha nikubali kuwa viongozi wetu huwa wanafanya vitendo vya
kigaidi,” alisema.
Alisema
kuwa akiwa makao makuu ya jeshi la polisi, aliteswa sana kwa maelekezo ya
Afande Pasua na Nyombi katika ghorofa ya nane, jengo la makao makuu ya polisi.
“Niliambiwa
nieleze siri za Dk. Slaa, Mbowe, Mnyika na Lissu na niseme kuwa walihusika na
vitendo vya utekaji na utesaji, nilipokataa nilipigwa shoti za umeme ili
nikubali kusema.
“Walikuwa
wametafuta hata waandishi wa habari wakisubiri nikubali ili wanirekodi. Nilitoa
maelezo kwa kulazimishwa huku nikiteswa. Nilipata nafuu baada ya wakili wangu,
Nyaronyo Kicheere, kuja ndipo nikaeleza nilivyofanyiwa ukatili,” alisema.
Alisema
kuwa alisafirishwa toka Dar es Salaam hadi Igunga na kwamba kila walipopita
alitambulishwa kwa makamanda wa polisi kuwa ni mtu hatari sana.
Seif
Magesa (Mwanza)
Alisema
kuwa alikamatwa Mwanza na mabaunsa wa Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry
Matata, aliyefukuzwa CHADEMA, wakiambatana na Adam Chagulani ambaye pia
alifukuzwa pamoja na baadhi ya maafisa wa Usalama wa Taifa.
“Nilipelekwa
ofisi za Usalama wa Taifa. Nilihojiwa nikiulizwa mimi ni nani katika CHADEMA na
kwa nini huwa nawasiliana na Mbowe, Dk. Slaa, Lissu au Mnyika,” alisema.
Alisema
kuwa aliuzwa kama viongozi hao wanahusika na utekaji wa watu mbalimbali
unaotokea nchini na alipokataa aliteswa sana kuanzia saa 3 hadi 7 usiku.
“Nilipigwa
shoti za umeme kwa maelekezo ya afande Pasua. Yeye alikuwa anakuja kuniaga kuwa
anaenda kunywa pombe, vijana watafanya kazi yao. Waliniambia kuwa Lwakatare
alikuwa amenitaja kuwa mimi nafanya vitendo vya kigaidi. Nilikataa kata kata,”
alisema.
Aliongeza
kuwa Aprili 23, mwaka huu, waliwaleta mama yake mzazi, mama mkwe na mkewe huku
wakimdhalilisha mbele yao lakini alikataa kubadili maelezo yake.
“Siku moja
nikiwa nahojiwa simu ya afande aliyekuwa ananihoji ilikuwa karibu; kiongozi
mmoja wa CCM (anamtaja) alipiga simu akisema kama nimekataa kusema lolote
nipelekwe Igunga ambako nilipelekwa nikasomewa shtaka la kummwagia tindikali Musa
Tesha,” alisema.
Oscar
Kaijage (Shinyanga)
“Mimi
nilikamatwa, nikaambiwa niwasaidie askari kufahamu wizi wa milioni 100 uliokuwa
umefanyika kwa njia ya mtandao kwa kuwa mimi ni wakala wa Airtel.
“Lakini
nilipokubali kwenda na askari kituoni nikawekwa chini ya ulinzi. Ghafla
nikapelekwa kwa mkuu wa upelelezi akanielekeza kuwa nikapekuliwe nyumbani
kwangu kama kuna silaha ya aina yoyote au chupa zenye majimaji. Nilipekuliwa
hawakupata kitu. Ilikuwa yapata saa 5 mchana,” alisema.
Aliongeza
kuwa ilipofika saa 12 jioni, alipelekwa tena kwenye ofisi ya mkuu wa upelelezi,
akakutana na askari alioambiwa wanatoka Dar es Salaam.
“Hapo
nikamkuta afande ninayemfahamu, anaitwa Pasua kwa kuwa aliwahi kufanya kazi
Shinyanga na Simiyu. Walinihoji kwa nini nina namba za viongozi wa CHADEMA.
Nikawaabia, ‘mbona hamuulizi za wale wa CCM?’,” alisema.
Alisema
kuwa alijibiwa kuwa wanajua hana kosa ila wanataka ushirikiano aseme kuwa
Mbowe, Slaa, Mnyika na Lissu wanahusika na utekaji unaotokea nchini.
“Nilikataa.
Afande Pasua nikamwambia anajua kazi yangu na mimi namjua yeye ndipo wakasema
sasa kwa kuwa sitoi ushirikiano nitaunganishwa kwenye kesi ya kummwagia Musa
Tesha tindikali huko Igunga,” alisema.
Aliongeza
kuwa alipelekwa Igunga na wakati wanahojiwa na askari wa kutoka makao makuu,
walikuwa wanafanya siri hata OCD wa pale alikuwa haruhusiwi kusikia.
Rajabu
Kihawa (Dodoma)
Alidai
kuwa alichukuliwa Dodoma baada ya kupigiwa simu na msichana mmoja aliyedai kuwa
na maagizo kutoka kwa kaka yake anayesoma naye Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Nilikataa
lakini alikuwa anapiga simu kila mara, nikaona ngoja nikamsikilize. Nilipofika
kabla sijaongea naye nilikamatwa na maafisa sita wa polisi waliojitambulisha,
wakaninyang’anya simu zote na kunipeleka polisi.
“Walinihoji
kama najua mkanda wa Lwakatare, nikasema sijui. wakanihoji kama viongozi wa
CHADEMA wanahusika na utekaji unaoendelea nchini, nako nikasema sijui,”
alisema.
Alisema
kuwa baada ya hapo alipelekwa na kufungiwa Chamwino siku mbili bila kupewa
chakula kisha askari wakaja wakamuuliza kama amebadili msimamo.
Alitolewa
akapelekwa hoteli ya Nam, ambapo aliwakuta vijana waliofukuzwa kwenye uongozi
wa Bavicha (anawataja) meya mmoja wa Mwanza na diwani aliyefukuzwa CHADEMA na
kijana mwingine wa chama hicho mkoa wa Pwani aliyevuliwa uongozi wa Bavicha.
“Niliombwa
nikubali kupewa sh milioni 30 ili nikubali kurekodiwa nikisema kuwa Mbowe, Dk
Slaa, Lissu na Mnyika wanahusika na vitendo vya kigaidi na utekaji.
“Nilikataa.
Baadaye niliingizwa katika chumba kimoja cha hoteli hiyo nikakuta mbunge mmoja
wa CHADEMA kutoka Kanda ya Ziwa (anamtaja) akaniambia, ‘angalia huku’
akinionyesha simu yake kuwa alikuwa akiwasiliana na Rais,” alisema.
Kihawa
aliongeza kuwa aliahidiwa kupewa cheo kizuri serikalini na fedha ili mradi
akubali kuwa viongozi hao wa CHADEMA wanafanya vitendo vya kigaidi.
“Nilimuuliza
kwa nini alikuwa ananishauri hivi wakati yeye ni mbunge wa chama chetu. Akasema
mimi nilishinda ubunge sio kwa sababu nipo CHADEMA, bali ni muhimu hata
akiondoka CHADEMA.
“Nilikataa
kukubali ushauri wao ndio niliambiwa napelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi
ya Musa Tesha,” alisema.
Henry
Kileo (Dar)
Alisema
kuwa alipigiwa simu na maafisa wa polisi makao makuu Juni 17, mwaka huu,
wakimwarifu kuwa wanataka kufanya mahojiano naye lakini hawakusema ni kuhusu
nini.
“Juni 21,
mwaka huu, wakili wangu Peter Kibatala na John Mnyika (mbunge wa Ubungo)
tulienda polisi makao makuu, nilihojiwa mambo mbalimbali likiwemo tukio la kummwagiwa
tindikali Musa Tesha.
“Nilicheka
sana kwa kuwa kabla ya kuitwa nilipata taarifa za kikao kilichofanyika Dodoma
ili kuniunganisha na kesi ya ugaidi. Mahojiano yalifanyika wakati tayari kuna
kesi iliyokuwa inaendelea huko Igunga,” alisema.
Kileo
alisema kuwa baada ya mahojiano hayo na kuandikisha maelezo saa 11.30 jioni,
polisi walimnyima dhamana na kumpeleka rumande ya kituo kikuu cha polisi
alikolala.
“Jumamosi
ya Juni 22, familia yangu ilikuja kunitembelea ikakatazwa lakini baadaye wakili
wangu aliwasiliana na makao makuu ya polisi ndipo wakaruhusiwa kuniona.
“Juni 22,
mwaka huu, nilisafirishwa kwa ndege nikapelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi
ya kummwagia tindikali Musa Tesha baada ya kukataa kujibu maswali ya
kuwahusisha viongozi wa CHADEMA na vitendo vya utekaji vinavyotokea nchini,”
alisema.
Source:Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment