![]() |
John Tendwa. |
Rais Jakaya
Kikwete amemteua Jaji Francis Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa kujaza
nafasi iliyoachwa na John Tendwa ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.
Taarifa
iliyotolewa Dar es Salaam jana(Agosti 05,2013) na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Sefue ilisema kuwa uteuzi huo ulianza Agosti 2, 2013.
Kabla ya
uteuzi huo, Jaji Mutungi ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali katika idara ya
Mahakama, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.
Historia ya
Jaji Mutungi katika utumishi wake mahakamani ilianza mwaka 1989 alipoanza kazi
akiwa hakimu, baadaye akateuliwa kuwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam.
Baadaye
aliteuliwa na kushika nafasi za Msajili Mahakama ya Ardhi; Hakimu Mfawidhi
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma,
Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Msajili Mahakama ya Rufani na hatimaye
Jaji katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Kuhusu
Tendwa, ameachia nafasi hiyo akiwa katika msuguano wa kisiasa na baadhi ya
vyama vya siasa, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho
hivi karibuni kilitangaza kutokumtambua wala kushirikiana naye.
Katika
utumishi wake huo wa miaka 12 tangu alipoachiwa nafasi hiyo na Jaji George
Liundi, Tendwa amekuwa akishutumiwa mara kwa mara kwa upendeleo dhidi ya vyama
vya upinzani, madai ambayo amekuwa akiyapuuza. Alipotafutwa tena jana
kuzungumzia madai hayo hakupatikana kwa kuwa alikuwa nje ya nchi.
Mbali na
Chadema, Tendwa ambaye amewahi kukwaruzana na vyama cha CUF na TLP, mara
nyingine amekuwa akitoa tishio la kuvifuta vyama hivyo kwa kile alichodai kuwa
vinachochea vurugu.
Hali hiyo
ilimjengea uhasama baina ya ofisi yake na vyama vya upinzani na kuna wakati
aliwahi kutajwa adui namba moja wa vyama vya upinzani na demokrasia.
Source :Mwananchi.
No comments:
Post a Comment