Katika suala
la zima la kuwa na afya bora, hiyari iko mikononi mwa mtu mwenyewe. Unaweza
kuamua kuishi na afya bora na unaweza pia kuamua kuishi na afya mbaya, uamuzi
ni wako.
Kama ilivyo kwa jambo lolote, nia, uelewa na kujituma ndiyo huwa siri
ya mafanikio, hivyo hata katika suala la afya ni hivyo hivyo.
Mtu kuwa na
afya njema siyo jambo linaloweza kuja lenyewe bila wewe mwenyewe kufanya
jitihada za kupata maarifa ya kutambua mahitaji ya mwili wako, halikadhalika,
kuwa na afya mbaya hakuji kwenyewe, bali huwa ni matokeo ya kutokuzingatia au
kutokujua mahitaji ya mwili wako jana, hasa katika suala zima la chakula na
mtindo wa maisha unayoishi.
Katika
makala ya leo, tutakupa baadhi ya dondoo muhimu zitakazokusaidia kukupa mwanga
wa njia bora ya kuishi maisha yenye afya njema kwa kujua hulka ya mwili wako na
kufanya kile mwili unataka;
MWILI IMARA.
Mwili
umetengenezwa ili kufanyakazi na kujishughulisha nyakati za mchana na kupumzika
usiku giza linapoingia, ndivyo mwili ulivyoumbwa na ulivyozoea.
Ingawa kuna
mwanga wa bandia unaoweza kubadilisha usiku ukaonekana kama mchana, lakini
viungo ndani ya mwili vinafuata asili yake na huwezi kuvidanya.
Hivyo huna
haja ya kushindana na mwili wako, kama una uhuru wa kupanga muda wako, ni vyema
kufanyakazi zako mchana na kisha ukalala mapema na kuamka mapema.
Hii itaupa
mwili nafasi ya kutosha ya kupumzika wakati nishati yake inapokuwa katika
kiwango chake cha chini. Utashangaa kiwango cha kazi au michezo utakayoweza
kuifanya kwa kuamka asubuhi mapema.
Hapa
inasisitizwa kwamba kulala na kuamka mapema ndiyo mwili unavyotaka na ndivyo
ambavyo utakavyoweza kufanya kazi au shughuli yako yoyote kwa ufanisi zaidi na
bila kuuchokesha mwili.
TIBA MBADALA.
Vyakula kama
vile matunda, mboga na baadhi ya vyakula vingine vilivyopo jikoni kwako, vina
uwezo mkubwa wa kutumika kama tiba mbadala.
Ni vizuri kujua uwezo wa kila
tunda, mboga au mmea wowote katika kutibu magonjwa madogo madogo kama kichwa,
tumbo, mafua, n.k, badala ya kukimbilia matumizi ya dawa kali kali (Anti
Biotic).
Kwa matatizo
ya mafua na kusikia baridi mwilini, vitunguu swaumu ni dawa nzuri sana.
Tengeneza supu ya kuku yenye mchangayiko wa vitunguu swaumu visivyopungua punje
sita na yai bila kiini chake, kisha kunywa - mafua na baridi vitatoweka.
Kwa matatizo
ya kuchafuka kwa tumbo au kujaa gesi, chukua kijiko kimoja na nusu cha
mdalasini, weka kwenye kikombe kimoja cha maji yenye uvuguvugu, changanya kisha
acha kwa muda wa dakika kumi na tano.
Baada ya muda huo, kunywa mchangayanyiko
huo, mchafuko wa tumbo utaondoka mara moja.
DONDO ZA
AFYA BORA.
Unene ni
tatizo kubwa miongoni mwa vijana na watu wazima. Watu wengi wanakula kupita
mahitaji yao halisi. Utafiti unaonesha kuwepo uhusiano mkubwa wa ulaji kupita
kiasi na hatari ya kuatwa na magonjwa.
Ulaji wa
chakula kiasi na chenye manufaa kiafya, kutakuhakikishia wewe na familia yako
afya imara kwa miaka mingi ijayo.
Ni bora kula kila siku mlo wenye faida kwa
mwili wako badala ya kufanya hivyo pale unapoambiwa na daktari tu.
Ulaji wa
mboga pekee (vegetarianism) unaendelea kupata umaarufu duniani kwa sababu
unamuwezesha mtu kupata faida zote sawa na mtu anayekula nyama, lakini bila
kuwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wowote.
Jizuie kula
kupita kiasi na hakikisha unakunywa maji mengi kila siku. Wakati mwingine watu
hutafsiri kiu kama njaa na kuishia kufakamia chakula wakati kilichokuwa
kikihitajika mwilini kilikuwa maji tu.
Hivyo tunashauriwa kutii miili yetu kwa
kuhakikisha tunakunywa maji ya kutosha, hata kama hatusikii kiu, kwa sababu
pale tunaposikia kiu, tayari mwili unakuwa umepungukiwa maji.
No comments:
Post a Comment