![]() |
Wafuasi wa MDC.
|
Chama cha
Movement for Democratic Change (MDC) nchini Zimbabwe kimewasilisha malalamiko
yake mahakamani kupinga ushindi wa Robert Mugabe katika uchaguzi wa rais wa
wiki iliyopita.
MDC
inataka matokeo ya uchaguzi huo yabatilishwe na uchaguzi mpya uitishwe katika
kipindi cha siku 60.
Chama
hicho kimetaja mambo 15 ,mkiwemo madai ya kutoa hongo,kutumia vibaya haki ya
kuwasaidia wapigaji kura na kuvuruga daftari za wapiga kura.
Bw
Mugabe,mwenye umri wa miaka 89, alishinda uchaguzi kwa asilimia 61% ya kura.
Chama
chake cha Zanu-PF kilipata zaidi ya theluthi mbili za viti vya bunge ikishinda
viti 160 ikilinganishwa na viti 49 kwa MDC.
Mawakili
wa MDC,waliowasilisha malalamiko yao katika mahakama ya katiba,wameiambia BBC
kwamba walikuwa na ushahidi thabiti wa kutumika mbinu zisizo za kawaida katika
utaratibu wa upigaji kura.
Walisema
idadi kubwa ya watu hawakuweza kupiga kura na kwamba chakula chakula na vitu
vingine vilitumika kama hongo za kuwashawishi wapigaji kura wampigie kura Bwana
Mugabe.
"Chama
cha Movement of Democratic Change kinataka matokeo ya uchaguzi huu yatenguliwe
kuwa batili kwa mujibu wa ibara ya 93 ya katiba ya Zimbabwe"Amesema
msemaji wa MDC Douglas Mwonzora.
Hatua ya
MDC inakuja baada ya tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kusema takriban wapigaji kura
305,000 walikataliwa kupiga kura siku ya uchaguzi.
Kwa mujibu
wa takwimu zilizotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi nchini Zimbabwe ZEC,
zimeonesha kuwa watu milioni 3.5 walipiga kura kwenye uchaguzi wa tarehe 31 ya
mwezi July mwaka huu na kusaidia kumuongezea muhula wa saba rais Robert Mugabe.
No comments:
Post a Comment