Maandamano ya amani yaliyokuwa yameandaliwa na chama
cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) yamegeuka shubiri kwa wakazi wa jiji la
Mwanza baada ya kuibuka mapambano makali baina ya waandamanaji hao na jeshi la
polisi mkoani Mwanza na kusababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa
chama hicho.
Maandamano hayo ya amani ya jana(Agosti 19,2013) ambayo
yalianzia katika eneo la Buzuruga nje kidogo ya jiji la Mwanza yalikuw
ayakiongozwa na wabunge Highness Kiwia wa Ilemela pamoja na Ezekiel
Wenje kuelekea katika viwanja vya Furahisha, yalilenga kumshinikiza Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza Bw.Ernest Ndikilo kutoa barua zinazodaiwa kuandikwa na ofisi ya
Waziri Mkuu Tamisemi kuwarejesha madiwani watatu waliotimuliwa katika Manispaa
ya Ilemela kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo.
Polisi wenye silaha pamoja na askari kanzu walianza
kutanda katika eneo hilo la Furahisha wakiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa
makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza RCO Konyo ambaye alikuwa akitumia gari lenye
namba za usajili DK 068EXV aina ya Toyota Land Cruiser.
Maandamano hayo ambayo awali yalionekana kana kwamba
yangelimalizika salama yaliwasili katika viwanja vya Furahisha majira ya saa
5.38 huku yakiongozwa na gari la polisi lenye namba za usajili za nchi ya Uganda 779
UAG likiwa nimesheheni polisi wenye silaha nzito ikiwa ni pamoja na mabomu ya
machozi na bunduki pamoja na askari kadhaa ambao walikuwa katikati ya
maandamano hayo.
Baada ya maandamano hayo kuwasili katika viwanja vya
Furahisha kwa amani,waandamani hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali
yaliyosomeka kuwa ‘Matata hatutaki uendelee kuwa Meya wa Ilemela rudia kazi
yako ya awali, na jingine Jaji Sumari tumechoka kuahirisha mara kwa mara kesi
dhidi ya Matata na jingine lililosomeka kuwa RD Ndikilo tunahitaji
barua za kurejeshwa kwa madiwani wetu.
Hata hivyo tofauti na ilivyokuwa imetangazwa kuwa
maandamano hayo ya amani yangelipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw.Ernest
Ndikilo,hakukuwa na kiongozi yoyote wa Serikali ambaye alikuwepo uwanjani hapo
kupokea maandamano hayo.
Kufuatia kutoonekana kwa kiongozi yoyote wa
Serikali,viongozi wa chadema pamoja na wabunge wao walikutana kwa faragha kwa
dakika kadhaa kwa ajili ya kujua hatima ya maandamano hayo ambapo Mbunge wa
Nyamagana Bw.Ezekiel Wenje alipanda jukwaani saa 6.45 na kuwaeleza maelfu ya
waandamanaji kuwa wameamua kumtuma Mbunge wa Ilemela Bw.Highnes Kiwia kwenda
ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuchukua majibu kwa ajili ya kuwaletea
wananchi walioandamana juu ya hatima ya madiwani hao.
Hata hivyo saa moja baadae Mbunge huyo alisimama
jukwani na wakuwaeleza waandamani hao kuwa simu ya Mbunge Kiwia ilikuwa
haipatikani hivyo kuwataka kuandamana kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza kujua
kulikoni na hapo ndipo hali ya hewa ilipochafuka.
Jeshi la polisi baada ya kuona wandamanaji hao
wameanza kuelekea katika ofisi za Mkuu wa mkoa liliwataka kutawanyika ambapo
waandamanaji hao walikaidi ndipo jeshi la polisi lilipoamua kutumia mabomu ya
machozi kuwatawanya wafuasi hao.
Vurugu hizo ambazo zilianza majira ya saa 7.30
zilisababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara kutokana na waandamanji hao
kuweka vizuizi vya mawe na kuchoma matairi,ambapo pia maduka na ofisi
mbalimbali zililazimika kufungwa kwa muda kupisha vurugu hizo.
Baadhi ya wananchi ambao walikuwa wakitumia usafiri
wa umma walionekana wakishuka kupitia katika madirisha ya magari hayo na
kukimbia kwa hofu ya kujeruhiwa na mabomu pamoja na mawe ambayo yalikuwa
yakirushwa na waandamanji hao kwa jeshi la polisi.
MKUU WA MKOA WA MWANZA ALONGA.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza akizungumza na Mbunge Kiwia
pamoja na viongozi wa chadema ofisini kwake alisema kuwa ameshangazwa na uvumi
huo kuwa ofisi yake imekalia barua ya kurejeshwa kwa madiwani Abubakar
Kapera(Nyamanoro),Dan Kahungu(Kirumba) pamoja na Marietha Chenyenge(Ilemela).
RC Ndikilo alisema kuwa Serikali imekuwa ikifanya
kazi zake kwa maandishi na sio kwa kufuata maneno ya mtaani na kueleza kuwa
hana barua yoyote toka ofisi ya Waziri Mkuu inayomualifu kuhusu kuwarejesha
madiwani hao baada ya kukata rufaa.
“Hata Mbunge kuna siku ulinipigia simu ukiniuliza
juu ya kuwepo kwa barua hizo name nilikujibu kuwa kwa kuwa uko hapo Bungeni
Dodoma ambapo pia kuna ofisi ya Waziri Mkuu nilikujibu kuwa ni muhimu ukawaona
viongozi wakuu wa Tamisemi ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu,pia nilikushauri kuwa
wakupe japo nakala ya barua hiyo”,alisema RC Ndikilo.
“Lakini cha kushangaza nimekuwa nikisikia maneno ya
ajabu kuwa nimeficha barua za madiwani hao,ikumbukwe kuwa madiwnai hao
hawakukata rufaa kwangu bali walikata rufaa ngazi ya juu kabisa,ili kukata
mzizi wa fitina naomba kati ya tarehe 26 hadi 27 wewe Mbunge pamoja na mimi
twende TAMISEMI kukutana na viongozi ili kukata mzizi wa fitina na tuje
tuwaeleze wananchi ukweli uliopo”,alisema RC Ndikilo.
Kuhusu suala la Meya Henry Matata kutoondolewa
madarakani RC Ndikilo alisema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kw
akuheshimu mamlaka ya mahakama na kuwataka chadema kuvuta subira hadi pale
mahakama itakapotoa maamuzi yake.
KAULI YA MBUNGE KIWIA.
Akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza,Kiwia alisema kuwa waliamua kuitisha maandamano hayo kutokana na
kuelezwa na Waziri Hawa Ghasia kuwa tayari barua hizo zimeishatumwa mkoani
Mwanza.
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa hawa madiwani
waliosimamishw ani wawakilishi wa wananchi,wamekaa nje kwa miezi saba sasa na
uchaguzi wa Meya haukuwa halali ndio maana tuliamua kuitisha maandamano kwa
ajili ya kuhakikisha madiwani hawa wanarejeshwa.
RPC MANGU.
Akizungumza kwa simu juu ya kutokea kwa vurugu
zilizosababisha kupigw akwa mabomu ya machozi,Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza
Ernest Mangu alisema kuwa polisi walifanikiwa kudhibiti vurugu hizo na hadi
sasa hawezi kusema ni wananchi wangapi ambao walikamatwa kuhusu vurugu hizo.
WANANCHI WAWALAUMU VIONGOZI NA WANASIASA NA KUWAPONGEZA POLISI.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mtanzania juu ya
vurugu zilizotokea waliwaonyoshea kidole wanasiasa pamoja na viongozi wa mkoa
wa Mwanza kutokana na kushindwa kusema ukweli juu ya tukio hilo.
Baadhi walisikika wakisema kuwa kama barua zipo
kweli madiwani hao wanapaswa kupewa na kama azipo basi walioeneza maneno hayo
wachukuliwe hatua kali kutokana na uchochezi.
Wananchi hao pia walilipongeza jeshi la polisi
kutokana na kutumia busara badala ya nguvu kuhakikisha maandamano hayo yanakuwa
ya amani.
No comments:
Post a Comment