MAONI :- Bajeti ya Upinzani ina maono, Serikali iyafanyie kazi. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, June 17, 2015

MAONI :- Bajeti ya Upinzani ina maono, Serikali iyafanyie kazi.


Waziri Kivuli wa Fedha , James Mbatia  wa  Kambi Rasmi ya Upinzani  Bungeni akiwasilisha   bajeti ya  mwaka 2015/16 juzi June 15,2015 bungeni. 

 Tumeisoma kwa umakini mkubwa Bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka 2015/16 iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia.

Bajeti hiyo kwa kiasi kikubwa imeanika kasoro nyingi zilizomo katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2015/16 kiasi cha kuibua maswali mengi kama kweli uandaaji wa bajeti za Serikali katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukizingatia weledi na vigezo vinavyotumika katika mataifa mengi duniani, ikiwa ni pamoja na kutumia takwimu zinazozingatia uhalisia.

Bajeti hiyo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekwenda mbele zaidi kwa kuangalia Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha uliopita na kuzichambua katika muktadha wa takwimu zilizomo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha. 

Yeyote aliyesoma bajeti hizo mbili atakuwa amegundua kasoro nyingi, mojawapo ikiwa ni matumizi ya takwimu katika bajeti ya mwaka ujao zisizozingatia uhalisia na mwelekeo wa uchumi wa nchi yetu na dunia kwa jumla, ikiwa ni pamoja na suala la kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu dhidi ya Dola ya Marekani.

Matokeo yake ni bajeti ya kufikirika na isiyo na uhalisia, kwa maana ya kutozingatia ukweli kwamba Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao ni pungufu kwa asilimia 9.5 sawa na Sh2.363 trilioni au Dola za Marekani milioni 1.143.89, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha unaoishia mwezi huu. 

Takwimu zilizomo katika Bajeti ya Upinzani zinashabihiana na za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambazo zinabainisha kwamba katika kipindi cha Juni 2014 na Juni 2015 thamani ya shilingi moja inaizidi ya leo kwa shilingi 1.2. Kwa maana hiyo, bajeti ya Sh19.8533 ya Juni mwaka jana ni zaidi ya Sh24 trilioni kwa kiwango cha leo. 

Hivyo siyo sahihi Serikali kusema kwamba bajeti ya mwaka ujao imeongezeka kutoka Sh19.8533 mwaka wa fedha uliopita hadi Sh22.495 kwa mwaka wa fedha ujao kwa kuwa bajeti ya mwaka ujao imeshuka kulinganisha na mwaka uliopita kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Marekani.

Matokeo yake ni nini? Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao itakuwa na nakisi ya asilimia 9.5 sawa na Sh2.363 trilioni. Kiasi hicho cha nakisi kitaongezeka maradufu iwapo makusanyo ya kodi na vyanzo vingine vya mapato, ikiwa ni pamoja na misaada ya wafadhili na mikopo kutoka kwenye mabenki hazitapatikana kama ilivyopangwa na katika muda mwafaka, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kutokea tukiangalia hali ambayo imekuwa ikitokea miaka iliyopita. Kinachotakiwa sasa ni Bunge kukubali upungufu huo uliobainishwa na Kambi ya Upinzani na kuipitia bajeti hiyo upya kupitia Kamati ya Kudumu ya Bajeti.

Vinginevyo tutarajie bajeti ambayo itaendelea kuathiriwa na upungufu mkubwa wa fedha kiasi cha mipango ya maendeleo kutotekelezwa na mingine kusimama na watumishi wa Serikali kuendelea kulipwa mishahara pasipo kufanya kazi. 

Bajeti ya Upinzani imetoa mapendekezo mengi na tunaishauri Serikali isione aibu kuyatekeleza. Moja ya mapendekezo hayo ni upungufu uliomo katika bajeti hiyo, ambao tumeuelezea kwa kirefu hapo juu. Tunadhani mapendekezo hayo yanagusa mambo muhimu na ya msingi. Matumaini yetu ni kwamba Serikali itayapokea na kuyafanyia kazi kwa mustakabali wa nchi yetu.

Source:-Gazeti la Mwananchi June 17,2015....FULL TEXT-HOTUBA NZIMA YA BAJETI YA MWAKA 2015-2016 HII HAPA

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad