AFYA YETU:-Soma Madhara Wayapatayo Watanzania wanapotumia Vipodozi tishio kwa Afya. - Mwana Wa Makonda
cV7ufzj

Muhtasari

X-BET

MAIN-

Post Top Ad

cV7ufzj

Saturday, January 10, 2015

demo-image

AFYA YETU:-Soma Madhara Wayapatayo Watanzania wanapotumia Vipodozi tishio kwa Afya.

.com/simgad/
vipodozi_300_172

IMEELEZWA kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, sawa na watu milioni 31.5, wako hatarini kupata magonjwa ya ngozi, kutokana na kutumia vipodozi visivyo sahihi.

Kutokana na hali hiyo, imesisitizwa ipo haja ya elimu ya athari ya vipodozi kutolewa kuanzia shule za msingi, kwani wengi wa wanaoathirika wanakuwa na uelewa mdogo juu ya matumizi ya vipodozi.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Eliafoi Masenga wakati wa semina ya kupata taarifa mbalimbali kuhusu vipodozi hatarishi, iliyofanyika Januari 08,2015, Dar es Salaam.

Alisema kutokana na uelewa mdogo, Watanzania wengi wanaathirika. Alitoa mfano kuwa yeye peke yake anatibu magonjwa ya ngozi kwa watu wasiopungua 12,000 kwa mwaka.

Ofisa kutoka Shirika la Envirocare, Ephrasia Shayo alielezea kushangazwa na kitendo cha maduka ya vipodozi, kuuza dawa za hospitalini kinyume cha sheria na kuongeza kuwa nayo yanachangia kuhatarisha afya za wananchi.

Alitaja baadhi ya dawa za hospitalini, zinazouzwa katika maduka ya vipodozi kuwa ni pamoja na Lemovate, Clobetasol, Betacort, Diproson na Mediven.

Alisema sheria inaeleza wazi kuwa anayeuza vipodozi, haruhusiwi kuuza dawa za hospitalini, ila anayeuza dawa ya hospitali anaruhusiwa kuuza vipodozi visivyo na sumu, lakini kwa siku hizi watu wamekuwa wakikiuka sheria hiyo.

Aliongeza kuwa wauza vipodozi wengi, hawana uelewa katika jambo hilo, ndiyo maana vidonge vya malaria aina ya mseto vimekuwa vikitengenezwa mkorogo, ambao unachanganywa na sabuni aina ya “Jaribu”, iliyokatazwa.

MADHARA.

Wakati wataalamu hao wakionya hayo, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeendelea kupiga marufuku vipodozi visivyo na ubora, vikiwemo vyenye viambato vyenye sumu inayoathiri afya ya binadamu.

Madhara yatokanayo na matumizi ya vipodozi vyenye viambato vya sumu ni kupata mzio wa ngozi na athari kwenye ngozi inapopata mwanga wa jua. Athari hizo husababishwa na kiambato sumu kiitwacho bithional.

Kwa mujibu wa Ofisa Mwandamizi wa TFDA, James Ndege, madhara ya kiambato sumu kijulikanacho kama hexachlorophene, ni kupenya hadi kuingia kwenye mishipa ya fahamu na kusababisha ugonjwa, hasa kichwani.

Pia husababisha ugonjwa wa ngozi na kuiathiri mtu anapokuwa juani. Kwa watoto wachanga, hexachlorophene huathiri ubongo. Pia, husababisha ngozi kuwa laini, kiasi cha kukaribisha ugonjwa wa fangasi au maambukizo ya vimelea vya maradhi.

TFDA inataja madhara ya zebaki kuwa ni pamoja na kuharibu ngozi, ubongo, figo na viungo mbalimbali vya mwili. Mjamzito akitumia vipodozi vyenye zebaki humwathiri mtoto tumboni, ikiwa ni pamoja na kusababisha azaliwe akiwa na mtindio wa ubongo.

Matumizi ya zebaki husababisha pia ngozi kuwa laini na mabaka meusi na meupe. 

Husababisha pia mzio wa ngozi na muwasho, ugonjwa wa mishipa ya fahamu na madhara ya upofu, uziwi na upotevu wa fahamu mara kwa mara.

Vinyl chloride: Hiki ni kiambato chenye sumu kinachosababisha magonjwa ya kansa ya ini, ubongo, mapafu na mfumo wa damu. Sumu yake pia humsababishia mtumiaji kuumwa kichwa, kuhisi kizunguzungu na kupoteza fahamu.

Kiambato sumu aina ya zirconium husababisha kansa ya ngozi na mapafu. Athari kubwa za kiambato sumu aina ya halogenated salicylanilide katika afya ya binadamu ni ugonjwa wa ngozi na mzio wa ngozi mara inapopata mwanga wa jua.

Kwa upande mwingine, kiambato cha hydroquinone husababisha muwasho na mzio wa ngozi, kansa, kuchubuka kwa ngozi na kusababisha mabaka meusi na meupe.

Kadhalika, kiambato aina ya steroids cha kundi la homoni, husababisha madhara mbalimbali yakiwamo ugonjwa wa ngozi, chunusi, kulainisha ngozi kupindukia, kuchelewesha kidonda kupona na magonjwa ya moyo.

Chloroform ni kiambato chenye sumu ambacho husababisha kansa ya utumbo mpana na kibofu cha mkojo. Husababisha pia ugonjwa wa akili na mishipa ya fahamu, ngozi kuungua, maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu na kuota vipele.

Madhara kwenye mishipa ya fahamu yanayosababisha mtu kutopumua vizuri husababishwa na kiambato chenye sumu, kijulikanacho kama chlorofluorocarbon (halogenated chlorofuoroalkanes).

Kiambato sumu aina ya ethylene chloride husababisha kansa, madhara kwenye mishipa ya kati ya fahamu, ini na mishipa ya moyo. Pamoja na madhara ya kiafya yaliyotajwa hapo juu, pia kuna madhara ya kiuchumi yanayotokana na matumizi ya vipodozi visivyo bora na salama.

UNGANANASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Contact Form

Name

Email *

Message *