Mabingwa wa Africa ya Mashariki na kati Yanga hoi Kaitaba dhidi ya Kagera sugar. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, October 08, 2012

Mabingwa wa Africa ya Mashariki na kati Yanga hoi Kaitaba dhidi ya Kagera sugar.

Bao pekee la mchezaji Themi Felix katika dakika ya 67, jioni ya leo limewapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Mabingwa wa Africa ya Mashariki na kati  Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.



Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.



Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC. 


Aidha, hii ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.
   

Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na leo imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.


Katika mechi hiyo, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete. 


Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti.  


Katika mechi zilizochezwa jana, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.


Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.


Kiemba alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa kulia.


Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.


Katika mechi nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Polisi Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad