Ukata wa Fedha waziponza Mamlaka za Miji Midogo Rulenge na Ngara kutojiendesha. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, May 16, 2018

Ukata wa Fedha waziponza Mamlaka za Miji Midogo Rulenge na Ngara kutojiendesha.


Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza May 15,2018.

Mamlaka za Miji Midogo  Rulenge na Ngara mjini  wilayani Ngara mkoani Kagera zinaidai Halmashauri ya wilaya hiyo kiasi cha Shilingi milioni 25.5 kwa ajili ya kuendesha vikao vya viongozi  wa Mamlaka hizo ambao wanatakiwa kujadili na kuibua miradi ya Wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili.

 Hayo yamebainishwa na Diwani wa Kata ya Ngara mjini  Mhe.Marthon Gwihangwe wakati akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Kata kwenye kikao cha Baraza  la Madiwani cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2017/2018 kilichofanyika May 15,2018 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Mhe.Gwihangwe alisema mamlaka ya Ngara mjini  inadai  Shilingi milioni 17 ambapo Wenyeviti na Wataalamu hawatimizi majukumu yao huku Wananchi wakihitaji kuanzisha Miradi ya Maendeleo na kutatua changamoto za elimu, afya  na maji.

Alisema kukosekana kwa fedha za kuwalipa posho Wenyeviti wa Vitongoji na Wataalamu  waweze kufanya vikao vya kisheria kunachangia kuzoroteza mipango ya Maendeleo licha ya Halmashauri kukusanya mapato  na kutoza ushuru wa aina mbalimbali.

Kwa mwaka huu wa fedha mamlaka imefanya kikao kimoja cha mipango ya fedha  na mwenyewe nimefanya mikutano minne na Wenyeviti wa vitongoji lakini kilio kikubwa ni kuhitaji fedha za vikao vya kisheria

Naye  Mtendaji wa Mamlaka ya mji wa Rulenge Silialis Ruhimingunge alisema Mamlaka hiyo inadai Halmashauri Shilingi milioni 8.7 tangu kuanzishwa Mamlaka hiyo ,miaka mitatu sasa na kwa muda huo imelipwa Shilingi milioni 1.7 kwa wahusika 30 wa mji huo.

Alisema kinachosikitisha na kukatisha tamaa ni Halmashauri ya wilaya hiyo ya Ngara kufika kwa Wananchi na Wafanyabiashara kukusanya Mapato lakini asilimia inayopaswa kurejea kwa walipa kodi haiwafikii kutatua changamoto katika  huduma za kijamii.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo , Mhe.Georgina Munyonyera aliitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha kila mwezi katika makusanyo ya Shilingi milioni 80 ipunguze  Shilingi milioni 4 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani na kuzilipa Mamlaka hizo ili kuondoa malalamiko yaliyopo.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri,  Aidan Bahama alisema  tatizo kubwa la kifedha ni upungufu wa  vyanzo vikubwa vya mapato  hali inayosababisha  Watumishi wake hata Madiwani  kudai fedha za vikao vya kisheria.

Alisema Halmashauri hiyo haina nia mbaya ya kudidimiza Maendeleo ya Mamlaka zake ,hivyo kadri ya ukusanyaji  wa fedha utakavyoongezeka atazingatia ushauri wa Wajumbe wa Baraza  kupunguza kiasi cha madeni ya mamlaka ili zifanye kazi.

Habari /Picha Na-Shaaban Ndyamukama.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad