‘900 Itapendeza Zaidi’ yayazima Matukio 5. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, November 16, 2017

‘900 Itapendeza Zaidi’ yayazima Matukio 5.

Dkt. Louis Shika maarufu kama ‘900 Itapendeza’ akiwa katika ofisi za Global Publishers zilizoko Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.

Watanzania wamegeuka kuwa ‘walevi’ wa mitandao. Wanahamishwa tu na upepo uliopo. Inawezekana kabisa kupitia upepo wa mitandao, wananchi wakajikuta wamepoteza kabisa usikivu katika masuala mengine ya msingi.

Iko hivi, sasa hivi kuna ‘kurasa’ za watu maarufu mitandaoni ambazo nyingi zina wafuasi kuanzia milioni moja na kuelendea.

Wanapoposti kitu katika kurasa hizo, ndani ya muda mfupi kinasambaa kwa mamilioni ya Watanzania.

Tukio la Dk. Louis Shika aliyejinasibu kununua nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi zilizokuwa zikipigwa mnada, lililotokea Novemba 9, mwaka huu,2017 liligeuka kivutio kutokana na namna dokta huyo alivyoonekana siku ya tukio.

Aliingia kwa mbwembwe, akaonesha kwamba anaweza kuyanunua majumba mawili ya Lugumi yaliyopo Mbweni JKT ambapo nyumba moja alifika dau la Sh. Milioni 900 na nyingine kwa Sh. 1.1 bilioni.

 Baada ya kuwashinda wanunuzi wote, alipotakiwa atoe asilimia 25 ya malipo ya kila nyumba, Dk. Louis akaonekana hana, akataitiwa na polisi.
…Akiwa na Sifael Paul na Mhariri Mwandamizi wa gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli (kushoto) wakati wa mahojiano kuhusu yaliyompata.

‘Klip’ya mnada huo ilianza kuwa maarufu mtandaoni. Kipande cha video alichosikika Dk. Louis akisema ‘milioni 900 itapendeza,’ ndicho kilikuwa gumzo zaidi.

Kila mtu akawa anaweka vituko mbalimbali kwa kuchombeza na ‘milioni 900 itapendeza’.

Mitandao yote ya kijamii ‘ikachafuka’ na watu wote wakayatupa mambo yote yaliyokuwa yanaendelea nchini, hii ndiyo Tanzania yetu.

Amani linakuletea baadhi ya matukio makubwa ambayo kama si Dk. Louis yangeweza kushika hatamu katika mitandao na vyombo vya habari.

NDOA YA UWOYA, DOGO JANJA 

Kabla ya tukio la Dk. Louis ndoa ya Mbongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ na muigizaji Irene Uwoya ilikuwa gumzo.

Watu wengi walikuwa wakijadili tofauti wengine walikuwa wakisema kwamba ni ndoa ya kweli au feki.

Uwoya alisema si ndoa ya kweli lakini Dogo Janja alikomaa kuwa ni ndoa ya kweli. Ghafla tu, upepo ukageuka na kila mmoja akawa anajadili ‘mia tisa itapendeza.’

NAPE NA MIRADI YA SERIKALI 

Kutoka Bungeni Dodoma, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ‘alikinukisha’ kwa kuikosoa serikali kwa kutoshirikisha sekta binafsi katika miradi mikubwa. Akaeleza kwamba kama serikali itaendelea kuikumbatia miradi yote ya fedha nyingi, kuna hatari kubwa ya kuwepo kwa anguko la uchumi kutokana na ongezeko la deni la taifa.

Nape ambaye ni mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliicharukia vilivyo serikali inayoongozwa na chama chake hali ambayo isingekuwa Dk. Louis, angejadiliwa sana.

MAGUFULI UGANDA 

Ziara ya Rais Dk. John Pombe Magufuli nchini Uganda ilikuwa na mambo mengi makubwa likiwemo suala zima la uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Hoima – Tanga wenye urefu wa kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania, uliogharimu dola za Marekani bilioni 3.55 lakini kwa Dk. Louis, ishu hiyo haikujadiliwa kwa uzito wake.

TUKIO LA LISSU 

Bungeni pia suala la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu liliibuliwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Mbowe alilibua katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka kuruhusiwa kwa wachunguzi wa kutoka nje.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Majaliwa alisema ni vyema suala hilo likazungumzwa kwa ujumla wake na matukio mengine na kusisitiza kuwa vyombo vya dola havijashindwa kuchunguza tukio hilo. Tukio hilo nalo halikujadiliwa kwa upana wake.

NYALANDU KUANZA KAZI CHADEMA 

‘Bilionea’ huyo pia amezima tukio la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kuanza kazi kwa mara ya kwanza akiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ‘Chadema,’ mkoani Mtwara ambako alitambulishwa na Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe.

Nyalandu alijitokeza rasmi kwenye kampeni za udiwani za chama hicho katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kata ya Reli, Jumapili iliyopita.

NENO LANGU 

Watanzania wanapaswa kujikita zaidi katika masuala ya msingi katika kipindi husika kwani kuna uwezekano tukawa tunashabikia vitu visivyoleta tija, tukashindwa kutatua changamoto kubwa za taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad