CHADEMA- Serikali wekeni Hadharani ripoti za Madini ili Kila Mtu Azisome. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, July 31, 2017

CHADEMA- Serikali wekeni Hadharani ripoti za Madini ili Kila Mtu Azisome.

Mbowe akiongea na Waandishi wa Habari.

Serikali ya Tanzania imetakiwa kuweka hadharani ripoti zote mbili za madini zilizoandaliwa na kamati zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza uendeshaji wa Sekta ya Madini nchini humo.

 Hayo yamesemwa jijini dar es Salaam leo,Julai 31,2017 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika mkutano na vyombo vya habari ambao ulijikita kuelezea masuala ya uchumi.

Mbowe amesema Tanzania imegeuka kituko baada Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuipatia kampuni ya Acacia ankara ya malimbikizi ya kodi yanayozidi Sh400 trilioni.

"Serikali iziweke hadharani ripoti zote za madini ili kila mtu asome na kujua kuna nini kwenye ripoti hizo. Kiasi cha kodi wanachodaiwa Acacia ni bajeti ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 20. Hiki ni kituko," amesema.

Mbowe amesisitiza kwanza chama chake ndicho kilikuwa cha kwanza kudai mabadiliko katika sekta ya madini lakini kile kilichofanywa na serikali hakilingani na mabadiliko ambayo waliyapendekeza.

Akifafanua, amebainisha kuwa mabadiliko yaliyofanyika bungeni yamefanyika kwa papara na hayatalinufaisha taifa.
Katika hatua nyingine,Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Serikali haiwezi kujenga viwanda peke yake bila kuihusisha sekta binafsi ambayo ndiyo mdau mkuu katika uwekezaji nchini.

Mbowe amepinga kusudio la Rais John Magufuli kuwanyang’anya wawekezaji viwanda walivyobinafsishiwa kwa madai kwamba Serikali ilitakiwa kutafuta chanzo cha kufungwa kwa viwanda hivyo kabla ya kufikia uamuzi wake.

Mwenyekiti huyo amebainisha sababu mbalimbali zilizofanya viwanda hivyo visifanye kazi kuwa ni pamoja na kutopatiwa ruzuku na Serikali, teknolojia ya zamani ya viwanda hivyo na wakati viwanda hivyo vinajengwa kulikuwa na mfumo hodhi wa soko.

Amesema Rais Magufuli hana mapenzi na sekta binafsi kwa kuwa anaamini kwamba kila mtu aliye kwenye sekta binafsi ni “mpiga dili.”

Post Bottom Ad